Fainali Ngao ya Jamii mtasema mlikujaje!, mabeki mtegoni

YANGA iko moto. Azam ndio usiseme. Makocha wote wamesisitiza kwamba mechi ya leo ni zaidi ya fainali na ni kipimo sahihi cha kukoki silaha zao tayari kwa msimu wa ndani na kimataifa.

Lakini tathmini ya tambo za mashabiki wa timu hizo mitandaoni wanadai kwamba, hii ni mechi ya kibingwa itakayochezwa na wawakilishi wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Ingawa wenye mizuka wameenda mbali na kuwatambia wenzao wakidai kwamba; “Mtasema vizuri, mlikujaje fainali.”

Ni mechi ngumu ambayo huenda ikawa na ufundi mkubwa na idadi kubwa ya mabao pengine kuliko misimu iliyopita kutokana jinsi vikosi vilivyosukwa na kile kilichotokea kwenye mechi za mazoezi.

Yanga na Azam zinakutana katika pambano la fainali ya Ngao ya Jamii 2024 ya kibabe zaidi kwa timu hizo kutokana na upinzani uliopo baina yao. Mechi itaanza kupigwa saa 1:00 usiku mara tu baada ya Coastal Union na Simba kumalizana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu utakaopigwa kuanzia saa 9 alasiri.

Ni sahihi kusema maji na mafuta yamejitenga na sasa ni muda sahihi wa kupima yapi maji au mafuta yenye ubora baina ya timu hizo nne.

Kujitenga kwa maji na mafuta ni kwa vile Yanga na Azam zilizotinga fainali ndizo zilikutana katika fainali ya Kombe la Shirikisho, pia ndizo zilimaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu uliomalizika na hivyo kukata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Na inajidhihirisha pia kwa Simba na Coastal zitakazokutana katika kuwania mshindi wa tatu kwa vile zilimaliza katika nafasi ya tatu na ya nne katika msimamo wa ligi msimu uliopita na zote zitashiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Azam ilitinga hatua ya fainali baada ya kuifunga Coastal Union kwa mabao 5-2 katika mchezo mmojawapo wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Agosti 8, siku ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani wao Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.                                              

Fainali ya Yanga na Azam ndio inaonekana kusubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na ubora wa hali ya juu ulioonyeshwa na vikosi vya timu hizo mbili kuanzia msimu uliopita hadi sasa.

Ubora ambao kila moja imekuwa nao kwenye safu ya kiungo, umekuwa silaha muhimu kwa Azam na Yanga kupata matokeo mazuri katika mechi tofauti ambazo timu hizo zimekuwa zikicheza.

Lakini pia timu hizo kila moja inajivunia kuwa na kipa wa daraja la juu na hivyo kuwa na uhakika wa ulinzi imara wa lango ambapo Yanga itamtegemea Djigui Diarra na Azam, Mohamed Mustafa.

Yanga imekuwa na historia nzuri ya ubabe dhidi ya Azam na hilo linajidhihirisha katika michezo mitano ya mashindano tofauti ambayo timu hizo zimecheza siku za hivi karibuni.

Katika mechi hizo tano zilizopita baina ya timu hizo, Yanga imeibuka na ushindi mara nne na Azam imepata ushindi mara moja tu.

Mchezo mmoja kati ya minne ambayo Yanga ilipata ushindi, uliamriwa kwa mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa na matokeo ya sare tasa na mechi nyingine tatu, ilipata ushindi wa ndani ya dakika 90 kama ilivyo kwa ushindi wa mechi moja ambao Azam iliupata.

Yanga ina wastani mzuri wa ufungaji wa mabao katika mechi hizo kwani imepachika mabao saba ikiwa ni wastani wa bao 1.4 wakati Azam imefunga mabao manne tu ikiwa ni wastani wa bao 0.8.

Uwezo wa kufumania nyavu ambao umeonyeshwa na timu hizo katika mechi mfululizo ambazo zimecheza hivi karibuni unalazimisha makipa na mabeki wa kila upande kuhakikisha wanafanya kazi ya ziada ili kuhakikisha milango ya timu zao inakuwa salama katika mechi hiyo.

Katika mechi tano mfululizo zilizopita, Azam imefunga mabao 10 ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mchezo na ni mara moja tu kati ya mechi hizo tano, ambapo ilimaliza bila kufunga bao lolote.

Yanga kwenye michezo mitano mfululizo iliyopita, imefumania nyavu mara tisa ikiwa ni wastani wa bao 1.8 kwa mechi.

HUKU AZIZ KI, KULE FEI TOTO

Kulikuwa na ushindani mkubwa msimu uliopita baina ya Stephane Aziz Ki na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambao mwishoni Aziz Ki aliibuka mshindi.

Nyota huyo wa Yanga kutoka Burkina Faso alimuacha kwenye mataa Fei Toto kwa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu na kisha kuibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi kisha kuchukua tuzo ya kiungo bora wa ligi.

Ushindani wao unaonekana unarudi upya msimu huu kutokana na kile ambacho wamekifanya kwenye mechi za hivi karibuni za timu zao.

Fei Toto amefunga mabao matatu katika mechi sita zilizopita za Azam kama ilivyo kwa Aziz Ki ambaye amefunga idadi hiyo ya mabao kwa Yanga katika mechi tano zilizopita.

Mambo mawili yanaweza kuifanya mechi kati ya Simba na Coastal ya kuwania mshindi wa tatu ikawa na mvuto na ushindani wa aina yake.

Kwanza ni hamu ya kupoza machungu kwa kila upande baada ya kushindwa kutinga fainali ya Ngao ya Jamii na hivyo kupoteza fursa ya kushinda taji la kwanza msimu huu.

Lakini la pili ambalo ni kubwa zaidi ni hamu ya kulipa kisasi ambayo kila moja itakuwa nayo kwa mwenzake kutokana na sababu tofauti.

Simba ina hasira ya kupokonywa mchezaji Lameck Lawi ambaye ilimsajili kutoka Coastal, lakini katika hali ya kushangaza, timu hiyo ya Tanga ilibadilisha uamuzi ghafla na kurudisha fedha ilizopewa katika mauzo ya mchezaji huyo na kumuuza Ubelgiji katika timu ya KAA Gent.

Coastal yenyewe bila shaka inataka kulipa kisasi cha kupoteza mechi mbili za ligi msimu uliopita dhidi ya Simba ikifungwa mabao 3-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza ugenini na kisha ikapoteza kwa mabao 2-1 nyumbani.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema; “Napenda kucheza aina hii ya mechi, tumecheza na Simba sasa Azam ni kipimo sahihi kuelekea msimu mpya, tumekuwa na mwendelezo mzuri tangu tumecheza fainali Zanzibar, unapocheza na wapinzani wagumu unaimarisha zaidi kikosi chako kiushindani, nina matumaini kesho (leo) tutacheza vizuri.”

Kwa upande wa Youssouf Dabo wa Azam amekiri haitakuwa mechi nyepesi kutokana na timu hizo zilivyo na kukiri, Yanga ni timu nzuri, lakini hata wao (Azam) ni wazuri na watapambana kwa muda wote ili kushinda.

Kocha wa Simba Fadlu Davids alisema mechi ya leo kikosi hicho kitakuwa na mabadiliko makubwa licha ya kutoka kucheza mechi ngumu ndani ya siku chache.

“Kuhusu morali, wachezaji wote wapo vizuri kuhakikisha tunashinda mechi ya kesho (leo) baada ya kutoka kupoteza mbele ya Yanga,” alisema Fadlu, huku kocha wa Coastal, David Ouma alisema wamejipanga kufanya vizuri katika mchezo wa leo licha ya kukiri Simba ni ngumu na kibaya timu yake imetoka kupoteza kinyonge kwa mabao 5-2 mbele ya Azam.

“Hatutakubali kuwa wanyonge, nimezungumza na wachezaji na kuahidi kusahihisha makosa,” alisema Ouma.

Related Posts