Kiungo Simba Queens atambulishwa Burundi

BAADA ya kupewa mkono wa kwaheri na Fountain Gate Princess siku nne zilizopita hatimaye kiungo wa zamani wa Simba, Joelle Bukuru amejumuishwa kwenye kikosi cha PVP Buyenzi ya Burundi.

Simba Queens ilimtoa kwa mkopo wa miezi sita kiungo huyo kwenda Fountain katika dirisha dogo la usajili msimu uliopita baada ya kocha kutokuwa na mpango na mchezaji huyo.

Kiraka huyo raia wa Burundi alicheza Simba kwa misimu mitano tangu alipojiunga nayo mwaka 2019 akichukua mataji matatu ya Ligi na kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Michuano ya CECAFA kwa wanawake itaanza Agosti 17, Addis Ababa nchini Ethiopia na PVP Buyenzi imepangwa kundi B na Simba Queens, FAD Djibouti ya Ethiopia na Kawempe Muslim Ladies ya Uganda.

Kwenye kikosi cha wachezaji 20 cha PVP kiungo huyo amejumuishwa kuongezea nguvu kikosi hicho ambacho huu ndio msimu wake wa kwanza kucheza mashindano hayo.

Kikosi cha timu ya PVP Buyenzi kitasafiri kwenda Ethiopia kushiriki michuano ya CAF Women’s Champions League CECAFA itakayoanza rasmi Agosti 17.

Katika hatua nyingine winga wa zamani wa Simba Queens, Olaiya Barakat amejiunga na ASA Tel Aviv inayoshiriki Ligi Kuu nchini Israel kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Mchezaji huyo raia wa Nigeria aliichezea Simba Queens misimu mitatu akijiunga nayo Desemba, 2021 akitokea Bayelsa Queens ya nchini kwao.

Barakat ataungana na beki wa Yanga Princess, Noela Luhala aliyetambulishwa hivi karibuni na klabu hiyo inayoshiriki Ligi nchini Israel.

Msimamizi wa mchezaji huyo (hakutaka jina litajwe) aliliambia Mwanaspoti kuwa ni suala la muda tu kutambulishwa kwa winga huyo ambaye msimu uliopita hakuwa na msimu mzuri akikumbana na changamoto ya namba.

“Mteja wangu aliniambia mapema sana kabla hata hajapewa ‘Thank You’ na Simba anahitaji changamoto sehemu nyingine baada ya kuona hayuko kwenye mipango ya kocha hivyo tulipata timu huko na muda wowote anaweza kutambulishwa,” alisema msimamizi wa mchezaji huyo.

Related Posts