TANZANIA imepanda daraja kwa kutinga fainali za Kombe la Dunia kwa mchezo wa Kriketi kwa vijana chini ya umri wa miaka 19 baada ya wikiendi hii kuifunga Rwanda kwa mikimbio 59 katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika kwenye viwanja vya Dar Gymkhana, Dar es Salaam.
Kwa kuingia fainali, Tanzania imejihakikishia moja kwa moja nafasi ya kupanda daraja kutoka Divisheni ya Pili hadi ya Kwanza kwa mujibu wa Sheria za Chama cha Kriketi cha Dunia (ICC), timu nyingine iliyokula shavu ni Sierra Leone iliyoifunga Nigeria katika mchezo mwingine wa nusu fainali.
Tanzania ndio wenyeji wa michuano ya kufuzu kucheza fainali ambayo imeshirikisha mataifa manane ya Kiafrika na hadi kufikia fainali, timu hiyo ilishinda mechi zake zote nne kwa kishindo dhidi ya Nigeria, Ghana, Msumbiji kabla ya kuitoa Rwanda.
Katika mechi dhidi ya Rwanda, Darpan Jobanputra ndiye aliyeibeba Tanzania baada ya kutengeneza mikimbio 56 akisaidiwa na Omary Ramadhani aliyeitengenezea mikimbio 24.
Katika mchezo huo, Watanzania ndio walioshinda kura ya kuanza na jitihada zao ziliwafikisha katika mikimbio 164, huku wakipoteza wiketi 9 baada ya kukamilisha mizunguko yote 50.
Jitihada za vijana wa Rwanda kujaribu kufikia alama hizo ziligota kwenye mikimbio 105 baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 42 kati ya 50 iliyowekwa.
Katika mchezo mwingine wa nusu fainali, Sierra Leone iliifunga Nigeria kwa wiketi 9 na hivyo kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia wakiungana na Tanzania.
Nigeria ndio walioanza kubeti na jitihada zao ziligota kwenye mikimbio 116 baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 31 kati ya 50 iliyowekwa.
Vijana wa Sierra Leone waliweza kuzifukuzia na hatimaye kuzipiku alama za Wanigeria kwa kutengeneza mikimbio 119 huku wakipoteza wiketi moja tu.
Sierra Leone walitumia mizunguko 19 kati ya 50 ili kushinda mchezo huo.
Mohamed Turay aliyetengeneza mikimbio 31 na George Sessay aliyetengeneza mikimbio 29, ndiyo walioibeba Sierra Leone dhidi ya Nigeria.