Mchengerwa atoa maagizo kumaliza changamoto za walimu

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameiagiza Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), kutembelea walimu kwenye vituo vyao vya kazi na kujua changamoto zao, badala ya kung’ang’ania ofisini.

Mbali na hilo pia ameiagiza TSC kushughulikia  kero na changamoto za walimu nchini ili kuondoa malalamiko yote,  na kama kuna walimu watakuwa na tatizo la kisaikolojia wawape huduma ya ushauri nasaha.

Mchengerwa ameyasema hayo leo Jumapili Agosti 11, 2024 wakati akikabidhi magari 10 kwa makatibu wasaidizi wa wilaya wa TSC jijini hapa na kuwataka kuyatumia magari hayo kuwatembelea walimu kwenye vituo vyao vya kazi ili kujua changamoto walizonazo badala ya kukaa ofisini na kusubiri walimu wawafuate.

Wilaya zilizopata magari ni Rufiji, Nyamagana, Ilala, Bukombe, Tanga, Mbeya, Ruangwa, Kilosa na Kaliua. Huku Serikali ikiahidi kupeleka magari kwa wilaya zote zilizobaki.

Amesema magari hayo ni kitendea kazi cha kuwatembelea walimu kwenye vituo vyao vya kazi na kujua kero, malalamiko na changamoto zao kwani kuna makandokando mengi yanayosababisha walimu wasitimize majukumu yao kwa ufanisi.

“Walimu wanapitia changamoto nyingi sana, unaweza kusikia mwalimu amefanya tukio kwa mwanafunzi mpaka ukajiuliza imekuwaje kumbe ana changamoto ya kisaikolojia kwa sababu anafundisha kwenye majengo yaliyochakaa, nendeni mkazungumze nao na wale watakaobainika kuwa na tatizo la kisaikolojia wapeni huduma ya ushauri nasaha ili wakae sawa,” amesema Mchengerwa.

Amesema anataka walimu wafanye kazi kwenye mazingira mazuri yasiyo na changamoto na watakaoifanya kazi hiyo ni TSC na ndiyo maana Serikali imeamua kuwanunulia magari ili waweze kuwafikia walimu kwa urahisi.

Aidha amewataka kujua taarifa zote zinazohusu sekta ya elimu nchini ikiwemo uchakavu wa majengo ya shule, ukatili unaofanyika mashuleni na unyanyasaji unaofanywa kwa walimu na kuchukua hatua badala ya kuzipata taarifa hizo kwenye vyombo vya habari.

Amesema hategemei kupata simu na ujumbe kutoka kwa walimu wakimweleza kuhusu changamoto wanazozipitia, ilijali ni jukumu la TSC kuhakikisha wanatatua changamoto zote za walimu kabla hazijamfikia.

“Walimu wana changamoto nyingi, waka kero nyingi wana malalamiko mengi nendeni mkazungumze nao myatatue matatizo yao ili kuwajenga vizuri kisaikolojia hili ni jukumu lenu,” amesema Mchengerwa.

Pia amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuwawezesha makatibu wasaidizi wa TSC walioko kwenye maeneo yao, kuendesha ofisi zao kwa lengo la kuwahudumia walimu na kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi anayeshughulikia elimu, Charles Msonde amesema magari hayo yamenunuliwa kwa fedha za Boost ambapo jumla yapo 16, miongoni mwao matano yamepelekwa Tamisemi na 11 yamepelekwa TSC kwa ajili ya usimamizi na uboreshaji wa sekta ya elimu nchini.

Naye katibu msaidizi wa TSC kutoka Wilaya ya Nyamagana, Penina Alphonce amesema watatumia magari hayo kuwatembelea walimu na kujua changamoto zao zikiwamo kunyimwa mishahara, likizo na kupandishwa madaraja kwani ndiyo kilio kikubwa kwa kada hiyo nchini.

Related Posts