Moloko afichua kilichomzuia Namungo | Mwanaspoti

WINGA wa zamani wa Yanga, Jesus Moloko amefunguka kilichomzuia asirudi Tanzania baada ya kutakiwa na Namungo kisha kujiunga na timu ya Diyala SC iliyopo Ligi Daraja la Kwanza ya Iraq, akisema dau kubwa la usajili alilopewa na timu hiyo aliyompa mkataba wa mwaka mmoja ndio sababu iliyomfanya aende huko.

Moloko alikuwa anatajwa kujiunga na Namungo na winga huyo raia wa DR Congo alikiri alipelekewa ofaya kutaka aitumikie timu hiyo ya Ligi Kuu Bara, lakini ameshindwa kuungana nao baada ya kupata ofa kubwa kutoka klabu ya Diyala akitokea klabu ya Al Sadaqa ya Libya aliyomalizana nao mkataba na kuwa huru.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema mpira ndio unaendesha maisha yake hivyo sio rahisi kwake kuangalia uzoefu wa Ligi badala yake anaangalia fedha ambazo ndio zitamfanya ajitume zaidi ili kutunza familia yake.

“Ni kweli Tanzania nimecheza tena kwa mafanikio na nafahamu ligi, lakini nisingeweza kuja kwasababu hiyo dau la Namungu lilikuwa dogo kuliko huku ambapo nimesaini mkataba mpya naamini ntacheza na kuzoea,” alisema Moloko na kuongeza;

“Hata Tanzania nilianza kwa ugeni lakini baadae nikazoea mchezaji anaweza kucheza nchi yoyote kikubwa ni usalama na mazingira mazuri hivyo ndio vitu vya msingi tunazingatia.”

Moloko amecheza Tanzania akiitumikia Yanga kwa misimu miwili na nusu tangu alipotua Agosti 2021, kabla ya msimu uliopita kuondoka kwenda Libya kujiunga na Al Sadaqa huku akiwa tayari amefanikiwa kutwaa mataji mawili ya Ligi, Kombe la Shirikisho la Azam mara mbili na Ngao ya Jamii alitwaa mara mbili.

Pia alikuwa miongoni mwa mastaa waliocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika wakikosa Kombe dhidi ya USM Alger.

Related Posts