Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imekizuia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kufanya kongamano la vijana ambalo kimedai kitaweka hatma ya nchi ya Tanzania.
Uamuzi huo wa Ofisi ya Msajili unatokana na kile ilichoeleza, maneno yaliyozungumzwa kuelekea kongamano hilo yanahamasisha uvunjifu wa amani na vurugu na hivyo kukiuka vifungu vya 6A na 9(2) vya Sheria ya vyama vya Siasa.
Hoja ya ukiukwaji wa vifungu hivyo, inajengwa na kauli iliyotolewa na Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana wa Chadema Taifa, Twaha Mwaipaya, katika picha jongefu alipokuwa akiwatangazia vijana juu ya uwepo wa kongamano hilo, kesho Jumatatu, Agosti 12, 2024, katika viwanja vya Ruandazove, jijini Mbeya.
“Siku hiyo tutaweka hatma ya nchi ya Tanzania, kwamba vijana wa Chadema kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, tunaenda kuweka maazimio makubwa ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025,” alisema Mwaipaya katika video hiyo ambayo msajili ameifanyia rejea.
Licha ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukataza kongamano hilo, Chadema kimesema kinaendelea na maandalizi ya kongamano hilo kama ilivyopangwa.
Barua ya kuzuiwa kwa kongamano hilo (ambayo Mwananchi imeiona), imeandikwa Agosti 8, 2024, na Msajili wa Vyama vya Siasa iliyosainiwa na Naibu Msajili, Sisty Nyahoza kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.
Katika barua hiyo, ofisi hiyo imewaasa viongozi wa Chadema kusitisha shughuli yoyote waliyopanga kuifanya Agosti 12, 2024 Mbeya au mahali popote nchini, ambayo wanajua itasababisha uvunjifu wa sheria, amani na utulivu, kwa maelezo ya Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana wa Chadema katika video hiyo.
“…yanakiuka sheria ya vyama vya siasa na yanaashiria, mkusanyiko huo unaweza kutumika kuhamasisha vijana kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kama ilivyotokea Kenya,” imeeleza barua hiyo.
Barua hiyo inasisitiza:“Maelezo ya Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana wa Chadema katika video hiyo, yanakiuka Sheria ya vyama vya siasa na yanaashiria kuwa, mkusanyiko huo unaweza kutumika kuhamasisha vijana kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kama ilivyotokea Kenya.”
Kutokana na hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa, amewaita Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika na Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu kwenda katika ofisi yake Agosti 13, 2024 saa 5:00 asubuhi jijini Dar es Salaam.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, Mnyika amesema maandalizi ya shughuli hiyo yanaendelea kama ilivyopangwa.
Alipoulizwa wamekwisha kuijibu au kutekeleza takwa la barua hiyo, Mtendaji Mkuu huyo wa chama hicho amesisitiza: “Maandalizi yanaendelea kama yalivyopangwa.”
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi