Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini Mhe. Daniel Sillo amewaelekeza Maafisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA Mikoa ya Kagera na Kigoma kuhakikisha wanafanya utambuzi, usajili na usambazaji wa vitambulisho hivyo kwa wananchi katika Wilaya, Kata na Vijiji hakara iwezekanavyo.
Wito huo ameutoa Agosti 10, 2024 akiwa Mkoani Kagera kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, katika Mkutano wa hadhara uliyofanyika kwenye uwanja wa kumbukumbu Mayunga Manispaa ya Bukoba.
Naibu Waziri Sillo, amesema kuwa kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Serikali ilitenga Shilingi 42.5 milioni kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa vitambulisho hivyo vya Taifa (NIDA), ambapo kuanzia Oktoba 2023 vilianza kusambazwa nchi nzima.
“Naelekeza Maafisa Nida Mikoa ya Kagera, Kigoma na Wilaya zote katika Mikoa hii kuhakikisha wanafanya uhakiki, utambuzi na usambazaji wa vitambulisho hivyo kwa wananchi wenye sifa za kuvipata washuke hadi ngazi za chini wananchi wapate haki zao”Alisema Mhe. Sillo
Mhe. Sillo, amemhakikishia Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi, kuwa Mkoa wa Kagera kuna vitambulisho vya taifa 78,766 ambavyo havijakabidhiwa kwa wananchi hivyo amewataka Maafisa uandikishaji wote kutoka Wilaya zote kusambaza kadi hizo zilizoko tayari kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sillo, amesema Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini, Mhe. Stephen Byabato, amekuwa akifuatilia kwa karibu kuhusu lini Serikali itaboresha majengo ya makazi ya Askari Polisi wanaoishi mtaa wa Buyekera Kata Bakoba hivyo amesema Serikali kupita Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika mwaka wa fedha wa mwaka 2024/25 tayari wametenga kiasi cha Shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kujenga na kuboresha majengo hayo ya makazi ya Askali Polisi.