Ndoa yaweza kuwa pepo au jehanamu

Ndoa, kama taasisi yoyote ina pande nyingi, kubwa zikiwa mbili. Inaweza kuwa na mafanikio au maanguko. Ndoa ikifanikiwa hugeuka pepo. Ikishindwa haina tofauti na jehanamu, japo hakuna aliyewahi kufika huko.

Tudurusu namna ya kujua ndoa gani ni pepo au jehanamu kwa kudodosa. Ni wanandoa gani (siyo wa kwenye maigizo) ukiwaona unatamani ndoa yako ingekuwa kama wao au wanakumotisha kuoa au kuolewa kwa wasioa au kuolewa?

Je, wangapi ukiwaona walivyoharibikiwa, hata kama nawe unahanyahanya unasema “kumbe nasi tumependelewa?” Je, ni ndoa gani ukiziona, unatamani kutoolewa au kuoa au kama unasusua unajipa moyo?

Umewahi kuona njiwa wanavyopendana? Japo ni hayawani ambao maisha yao yamepangwa kiasi cha kutohitaji kutofautishwa na mazingira yao kama binadamu, wanakufundisha nini? Mnaowajua fisi jikumbushe.

Hatujui kama ndoa ya fisi ina amani, ikizingatiwa kuwa kikubwa walichojaliwa viumbe hawa ni ubinafsi, uchoyo na uroho sawa na wanadamu wanaofunga ndoa ili kuwachuna au kuwanyonya wenzao kwa faida binafsi na familia zao.
Pia, wapo wanaooa ili kuwanyonya wenzi wao, hasa wanaume wenye nyumba ndogo na wasio waaminifu kwa visingizio mbalimbali kama elimu na kipato. Japo hatujui lugha waongeayo njiwa, ndoa yao ni ya kutamanisha na kupigiwa mfano.

Ukiondoa bata, kuku na mbayuwayu, ndege wengi wana ndoa imara kutokana na uaminifu wao. Hatujui kama ni uchaguzi au majaliwa yao, ikizingatiwa hayawani hawana utashi, japo hatuna uhakika kama ni kweli au ni kutokana na wanadamu kutowaelewa vizuri. Mbona wana wivu na upendo. Hatuwaoni wakigombea majike, hasa majogoo au mabeberu, ingawa hatujui tabia ya majike.

Leo, tutaongelea ndoa kwa kuangalia aina tatu, yaani zilizofanikiwa, zinazosuasua, na zilizoshindwa kabisa. Si utani. Kuna ndoa zinaonyesha kufanikiwa kiasi cha kutamanisha au kuamsha wivu (si wa ubaya bali wa kujenga au wivu wa maendeleo) ambazo zinatupa hakikisho kuwa ndoa siyo ndoana, bali taasisi inayopaswa kuwa ya furaha, mafanikio, na si majuto.

Tutaziita ndoa hizi za njiwa kutokana na njiwa wanavyoaminika kuwa wapole, wapenda amani, na wenye mapenzi kemkem. Ndoa hizi, licha ya kuvutia, zina siri ya amani, upendo, mafanikio kiasi cha waliomo kujiona wenye bahati wakijilinganisha na makundi mengine.

Ndoa hizi ni pepo ndogo, kwani wengi wa wanaoishi katika ndoa hizi wana uwezekano mkubwa wa kuishi maisha marefu ikilinganishwa na wanaoishi kwenye ndoa zinazosuasua au kuharibika. Jarida la Forbes (Mei 10, 2014), kwenye utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Copenhagen, Sweden

“Watu walioripoti kukwaruzana mara kwa mara na wenzi wao au watoto, walikuwa na asilimia 50 hadi 100 ya uwezekano wa kufa mapema kutokana na sababu yoyote.”

Msongo wa mawazo, magonjwa ya akili, moyo, kimwili, uraibu na mengine yahusianayo na hali hii.

Aina ya pili ni zile ndoa zinazosuasua. Leo, zinatamanisha. Kesho, zinakatisha tamaa. Hizi ni nyingi ikilinganishwa na aina ya kwanza. Tutaziita ndoa za ‘mimosa pudica’, mmea ambao ukiukaribia unanywea, na ukiondoka, unaumuka na kuwa kawaida.

Tunatumia mimosa kutokana na kutokuwa na hali thabiti, sawa na ndoa zinazosuasua ambapo wanandoa leo wana furaha na kufurahia ndoa. Kesho wanatishina kutoana roho. Hizi ni nyingi sana duniani, hasa wakati huu ambao maadili yametelekezwa, tamaa za mali zimezidi, ubinafsi na urahisi wa kuvunja ndoa vimeongezeka.

Ndoa aina ya tatu ni zile zilizoharibika zisizoweza kurekebishika. Zinapoendelea kuwapo ni kwa sababu wanandoa hawana uwezo wa kuachana au wanaogopa kufanya hivyo kuepuka kuumia zaidi au kutokana na ujinga, umaskini, umri, mazoea na kulazimika tu kutokana na kukata tamaa kabisa. Tunaita kundi hili jehanam.

Unaweza kukuta wanandoa wanaishi kwenye nyumba moja, lakini wanalala vyumba tofauti. Wanapika vyakula tofauti. Wanaogopana. Asiyejua anashangaa ni kwa nini hawaachani. Ndoa yaweza kuwa pepo au jehanamu.
Kipende na kitunze chako. Kisicho chako si chako. Kama hauko kundi la kwanza, jitahidi uingie. Hakuna miujiza, bali kukubali udhaifu na kujifunza hata kufunza. Tumeishi kwenye ndoa ya kwanza kwa miaka 27. Inawezekana.

Related Posts