Neema Olomi aanza vyema gofu Mombasa

VIWANJA vya mchezo wa gofu vya miji ya mwambao wa Kenya vimekuwa ni rafiki kwa Mtanzania, Neema Olomi kutoka klabu ya Arusha Gymkhana baada ya kufanya vizuri tena katika mashindano ya mwaka huu ya wanawake kwenye viwanja vitano vya mjini Mombasa nchini humo.

Olomi alishika nafasi ya pili nyuma ya mwenyeji Mercy Nyanchama katika mchezo wa mashimo 18 yaliyofanyika kwenye viwanja vya Vipingo Lodge karibu ya jiji la Mombasa baada ya kutandika mikwaju 78.

Olomi ambaye hucheza kwa kiwango cha -4, alikuwa nyuma ya Nyanchama, aliyeibuka mshindi kwa fimbo tano.

Nyanchama, ambaye hucheza kwa kiwango cha -2, alimaliza juu ya Olomi kwa  fimbo tano akiwa na 73.

“Nilipambana sana kwani nilicheza dhidi ya mabingwa kama Mercy Nyanchama wa Kenya na Martha Babirye, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda,” alisema Neema Olomi.

Tanzania ilipeleka washiriki watano katika mashindano ya mwaka huu.

Wengine ni Vicky Elias kutoka TPDF Lugalo ambaye alimaliza katika nafasi ya 7 baada kupiga mikwaju 82.

Wengine walikuwa ni Shazz Myombe, Loveness Mungure kutoka Arusha na Yasmin Chali, ambaye pia ni katibu wa chama cha gofu ya wanawake nchini (TLGU).

Ni mashindano marefu ya mashimo 90 yanayoshirikisha viwanja vitano tofauti vilivyopo mwambao wa Kenya.

Chama cha Gofu ya Wanawake cha Kenya (KLGU), ndio walioandaa mashindano haya kwa kushirikiana na klabu tano ambazo viwanja vyake hutumika kwa mashindano.

Mwaka huu mashindano haya yameshirikisha zaidi ya wacheza gofu wanawake 120 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususan Uganda, Tanzania na wenyeji Kenya.

Mfululizo wa michuano hii ya wazi ya mwambao wa Kenya ilianzia viwanja vya Malindi.

Mara nyingi wacheza gofu wa Tanzania wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano yanayofanyika kwenye viwanja vya mikoa ya Pwani ya Kenya.

Mchezaji Madina Iddi ambaye hakushiriki katika mashindano ya mwaka huu kutokana na kutingwa na majukumu ya kikazi, amekuwa akishinda mara nyingi yakiwamo mashindano ya mwaka jana ambayo aliibuka mbabe.

Wengine waliofanya vizuri kwenye viwanja hivyo ni Angel Eaton, Ayne Magombe na Hawa Wanyeche.

Related Posts