NHIF yasitisha huduma kwenye vituo vya Aga Khan nchini

Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema umepokea taarifa kutoka Taasisi ya Aga Khan kuwa imekusudia kutoendelea na mkataba kati yake na mfuko huo,  kwa vituo 11 kati ya 24 kutokana na changamoto za kiuendeshaji kuanzia Agosti 14,2024.

Miongoni mwa vituo vilivyositisha huduma kwa wateja wa NHIF ni pamoja na Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam na kliniki zilizo maeneo mbalimbali nchini.

Taarifa iliyotolewa na NHIF Agosti 7, 2024 na kusainiwa na Hipoliti Lello kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, imeeleza wakati majadiliano na mtoa huduma yakiendelea, ili kuepusha usumbufu kwa wanachama wake wametoa taarifa kuanzia Agosti 14, 2024 utasitisha huduma katika vituo vya Aga Khan nchini.

Hata hivyo, Mwananchi ilipomtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Aga Khan Tanzania, Sisawo Konteh kuhusiana na taarifa hiyo amesema majibu rasmi atayatoa kesho Jumatatu.

“Kwa sasa bado sijaiona hiyo taarifa, lakini mpaka kesho Jumatatu nitatoa taarifa rasmi,”amesema Konteh.

Miongoni mwa changamoto zilizolalamikiwa ni pamoja na kiasi kidogo cha malipo ambayo NHIF wamekuwa wakiilipa Aga Khan hasa kwa wagonjwa wa upasuaji.

Kwa mujibu wa NHIF katika kuhakikisha mwendelezo wa huduma kwa wanufaika wake hususan waliokuwa wanapata huduma katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam mfuko umefanya makubaliano na kituo hicho katika yafuatayo;

Wajawazito wanaohudhuria kliniki katika hospitali ya Aga Khan ambao wametimiza majuma 35, wataendelea kupata huduma katika hospitali hiyo hadi watakapojifungua na kuruhusiwa.

Taarifa hiyo imeeleza kwa wajawazito ambao hawajatimiza majuma 35 wanashauriwa kutumia vituo mbadala vilivyosajiliwa na mfuko, ambapo pia baadhi ya madaktari katika vituo hivyo walikuwa wanawahudumia wakiwa Aga Khan.

Wagonjwa watakaokuwa wamelazwa kufikia Agosti 13 wataendelea kupata huduma katika Hospitali ya Aga Khan hadi watakapopata nafuu na kuruhusiwa.

“Wagonjwa wengine wote wakiwemo wa kliniki za saratani na kusafisha damu watapata huduma katika vituo vingine vilivyosajiliwa na mfuko.”

“Tayari mfuko umewasiliana na wagonjwa wa kliniki ya kusafisha damu na kuwahamishia kupata huduma hiyo katika vituo vinavyopendekezwa kwao,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha mfuko huo umeeleza kuwa umesajili vituo vingine vyenye hadhi sawa au zaidi ya Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam ambazo ni Saifee Hospitali na Shifaa Pan African Hospitali zote zipo jijini humo.

Vilevile wanachama pamoja na wategemezi wao wanaweza kupata huduma za haraka katika vituo vingine vikiwemo vile vikubwa kama Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya mifupa (Moi) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Kwa mikoa mingine, mfuko umehakikisha kuna vituo vilivyosajiliwa katika maeneo jirani ili kuwaepushia usumbufu wanachama.

Related Posts