Sababu panda shuka idadi ya wanafunzi sekondari binafsi

Dar es Salaam. Mchujo, idadi ya wanafunzi wanaohitajika katika shule husika na wazazi kukosa fedha za kugharamia mahitaji na ada zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea kupanda na kushuka kwa idadi ya wanafunzi sekondari binafsi.

Pia ongezeko la shule za Serikali nayo imetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazofanya shule hizo kukosa wanafunzi.

Sababu hizi zimetolewa baada ya Ripoti ya Takwimu Muhimu ya mwaka 2023 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni kuonyesha kupungua kwa wanafunzi wa sekondari wa shule binafsi kati ya kidato cha kwanza hadi sita.

Uchambuzi unaonyesha idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne ilishuka kwa asilimia 2.67 kati ya mwaka 2019 hadi 2023 na kidato cha tano hadi sita ikipungua kwa asilimia 12.35 mtawaliwa.

Hiyo ikiwa na maana, kidato cha kwanza hadi cha nne idadi ilishuka kutoka wanafunzi 270,302 hadi 263,010 huku kidato cha tano na sita idadi ikitoka 44,950 hadi 39,398.

Hata hivyo, idadi ya wanafunzi hao katika mwaka 2023 ilikuwa ni ongezeko kidogo baada ya anguko la wanafunzi mfululizo kati ya mwaka 2019 hadi 2022.

Wakati sekondari zikisuasua, upande wa shule za msingi binafsi mambo ni mazuri kwani idadi ya wanafunzi inazidi kupaa kila mwaka.

Takwimu zinaonyesha idadi ya wanafunzi katika ngazi hiyo iliongezeka kutoka 431,193 mwaka 2019 hadi kufikia wanafunzi 601,108 mwaka jana.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (Tamongsco), Aman Lyimo amesema wakati mwingine nafasi zilizopo katika shule ndiyo huakisi idadi ya wanafunzi watakaopokelewa.

Hiyo ni kutokana na madarasa yao kuwa na wanafunzi kati ya 25 hadi 30 ikiwa ni kuhakikisha ubora wa elimu unapatikana kama ilivyokusudiwa.

“Pia mchujo, mara nyingi mtu anaamua kuwa na watoto wachache ili wawe bora. Kila mtu anaangalia namna ya kutoa wahitimu wenye sifa na vigezo,” amesema Lyimo.

 “Huwezi kuchukua mwalimu hajui Kiingereza aje kufundisha Kiingereza, sisi tunaangalia utendaji kazi na si vyeti, hii inafanya wakati mwingine unaacha mwalimu wa shahada unachukua wa astashahada ila anayekupa kile unachokitaka,” amesema Lyimo.

Idadi ya wanafunzi kwa darasa aliyoitaja Lyimo inaendana na Mwongozi wa uanzishaji na usajili wa shule wa mwaka 2020 uliotolewa na Serikali ambao unaelekeza idadi ya wanafunzi kwa mkondo mmoja isizidi 40 kwa kidato cha kwanza hadi cha nne, na wanafunzi wasiozidi 30 kwa mkondo kidato cha tano hadi sita.

Kuhusu uwekezaji wa Serikali katika ujenzi wa shule mpya na uwekezaji uliofanyika nao unatajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa katika kuchochea upungufu wa wanafunzi katika shule zao.

“Sasa hivi kuna shule kila kata, wamewekewa walimu na hata vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kujifunzia, hii inafanya wazazi wengi wanaokosa fedha kuwapeleka watoto wao huko ili waendelee na elimu ya sekondari, baada ya kusoma kwetu elimu msingi,” amesema Lyimo.

Amesema uchumi wa wazazi nao ni kikwazo kwani pamoja na kutamani watoto wao kuendelea kusoma shuke binafsi, ila wamekuwa wakikwama kifedha.

“Baadhi wameendelea kujitahidi kidogokidogo ila wanaoshindwa wanachagua kurudisha watoto wao serikalini,” amesema Lyimo.

Kuhusu ongezeko la shule za sekondari za Serikali aliousema Lyimo unathibitishwa pia katika ripoti hii kwani takwimu zinaonyesha hadi Desemba 2023 zilikuwa 96,130  ikiwa ni ongezeko kutoka 84,106 mwaka 2019.

Lakini si shule za Serikali pekee zilizoongezeka hata za binafsi nazo idadi yake ilipaa kidogo hadi 21,779 kutoka 21,140, mtawaliwa.

Mmoja wa wazazi, Ruth Betram mkazi wa Ubungo amesema mara nyingi wazazi hutafuta namna ya kuwajengea msingi mzuri wa lugha watoto wao, ndiyo maana wanapofika sekondari wakichaguliwa shule ya Serikali huwaacha kuendelea huko.

“Kama mtoto akiwa anakimudu Kiingereza vizuri hauwi na mashaka katika maendeleo ya masomo yake sekondari,  maana mtoto anaweza kushindwa kumudu masomo kwa sababu tu haelewi lugha iliyotumika kufundishia,” amesema Ruth.

Lugha ya kufundishia upande wa sekondari ni moja ya jambo ambalo mara zote hupigiwa kelele na wadau wa elimu,  wakiitaja kuwa sababu ya wanafunzi kushindwa kufanya vizuri.

Mmoja wa wanaopinga matumizi ya Kiingereza katika kufundishia ni Mwalimu Richard Mabala ambaye pia ni mtunzi wa vitabu,  mara zote amekuwa akisema iwapo lugha ya Kiswahili itatumika kufundishia wanafunzi wengi watafanya vizuri.

Related Posts