SERIKALI KUJENGA DARAJA LA KALEBE NA KYANYABASA – BUKOBA VIJIJINI – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inakamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa Madaraja makubwa mawili ya Kalebe katika barabara ya Kyaka – Katoro – Kyetema na Daraja la Kyanyabasa katika Mto Ngono ili kukidhi mahitaji ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Bukoba Vijijini.

 

 

 

Bashungwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Katoma Wilaya ya Bukoba Vijijini katika ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, Mkoani Kagera.

 

 

 

Bashungwa ameeleza kuwa katika eneo la Kyanyabasa litakapojegwa daraja, Wananchi walikuwa wanapata huduma ya usafiri kwa Kivuko cha TEMESA ambacho kilikuwa kinatoa huduma kwa kusua sua na kupelekea Serikali kufanya maamuzi ya kujenga daraja kubwa.

 

 

“Mheshimiwa Katibu Mkuu kwenye Wilaya ya Bukoba Vijijini katika eneo la Kyanyabasa kulikuwa na kivuko cha TEMESA kilichokuwa kinatoa huduma kwa kusua sua, lakini habari iliyo njema Serikali inakwenda kuanza ujenzi wa daraja katika eneo hilo na Mkandarasi atafika kabla ya mwezi Disemba mwaka huu”, amesema Bashungwa.

 

 

 

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Kyaka – Katoro –Kyetema yenye urefu wa kilometa 60.7 kwa kiwango cha lami kwa kuanza na kipande cha kilometa 10 kitakachojengwa sambamba na ujenzi wa Daraja la Kalebe na kueleza kuwa Makandarasi atafika eneo la mradi kufika mwezi Disemba, 2024.

 

 

 

Bashungwa amesisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha inaweka miundombinu wezeshi na bora kwa Wananchi ili waweze kusafiri kwa njia ya barabara na kuondoa adha za usafiri hasa katika maeneo yenye vivuko.

 

 

 

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Bukoba Vijijni, Dkt. Jasson Rweikiza ameiomba Serikali kukamilisha taratibu za manunuzi ili kumuwezesha Mkandarasi kuanza ujenzi wa barabara ya Kyaka – Katoro –Kyetema yenye urefu wa kilometa 60.7 kwa kiwango cha lami, kipande cha kilometa 10 pamoja na Daraja la Kalebe.

Related Posts