Dar es Salaam. Vituo vitatu vya kanda vya gridi ya Taifa vinatarajiwa kujengwa nchini ili viweze kukisaidia kile cha Ubungo katika kutoa nishati hiyo pindi hitilafu inapotokea.
Kujengwa kwa vituo hivyo kutaifanya nchi sasa kuwa na uwezo wa kusambaza umeme kupitia kituo kingine pindi hitilafu inapotokea badala ya watu kukaa gizani kusubiri hitilafu ipatiwe ufumbuzi.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Agosti 11, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko wakati akizungumza na wanahabari baada ya kufanya ukaguzi katika kituo cha kudhibiti umeme wa gridi ya Taifa kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kufika kituoni hapo, Dk Biteko alitembelea mitambo mbalimbali katika eneo la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililopo Ubungo na kuangalia matengenezo mbalimbali yanayofanywa na mafundi.
Dk Biteko amesema kwa kawaida kituo cha Ubungo ndiyo kinachoangalia umeme wote nchini kwa sasa, lakini kiu ya Serikali ni kutengeneza vituo vya kudhibiti gridi ya nchi kwenye Kanda tofauti.
“Kujenga vituo hivi itasaidia sana, kama kutatokea tatizo sehemu fulani basi tuweze kuanzisha umeme kwenye kanda nyingine kwenda eneo lililoathiriwa,” amesema Dk Biteko.
Amesema hiyo ndiyo sababu ya kujengwa kwa kituo cha Dodoma ambacho kitakuwa kikubwa nchini na kukamilika kwake kutakifanya kituo cha Ubungo- Dar es Salaam kuwa cha akiba (backup).
“Pia, tutajenga upande wa kaskazini, Tanga Arusha na Kilimanjaro, kusini na kule Mwanza ili ikitokea shida mahali popote basi nchi nzima isiwe giza kwa sababu kituo kimoja kimeharibika,” amesema DK Biteko.
Amesema tayari wataalamu wameshafanya utafiti na hatua iliyopo sasa ni kutafuta wakandarasi ili kazi hiyo ianze kufanyika huku akieleza kuwa utekelezaji wake unahitaji muda na umakini.
DK Biteko amesema msukumo mkubwa uliopo sasa ni kuhakikisha wanachi wanapata umeme wa uhakika wakati wote huku akiwataka Watanzania kuwa wavumilivu wakati umeme unapokatika kwa ajili ya kufanyika matengenezo.
“Mungu ametusaidia tuna ziada ya umeme ndiyo maana mnaona leo kuna mitambo tumezima kwa sababu umeme uliopo unatutosha na hatuhitaji kuwasha mitambo yote,” amesema Dk Biteko.
Amesema mpaka sasa mitambo mitatu ya kuzalisha umeme katika Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere imeshaanza kufanya kazi na mwezi huu mtambo wa nne unatarajiwa kuwashwa.
Wakati hilo likienda kufanyika, tayari kupitia mradi wa maji Rusumo uliopo mkoani Kagera mashine zote tatu zikiwa zimewashwa na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi zinapata umeme kupitia mradi huo.
“Pia, tunajenga mradi mkubwa kutoka Iringa Mbeya, Sumbawanga na Katavi kwa ajili ya kuunganisha Katavi na Kigoma katika gridi ya Taifa. Mpaka sasa mradi umefika asilimia 98. Tunaamini ndani ya muda si mrefu mikoa hii itakuwa kwenye gridi ya Taifa,” amesema Dk Biteko.
Mtambo huu wa nne utakaowashwa ni kati ya ile tisa iliyopo katika bwawa hilo, yote ikiwashwa kwa pamoja megawati 2,115 inatarajiwa kuzalishwa.
Dk Biteko aliendelea kueleza kuwa, wakati mikoa hiyo ikiunganishwa katika gridi ya Taifa, laini nyingine iko katika ujenzi ambayo ni kati ya Songea – Masasi hadi Somanga Fungu ili kuweza kuingizwa katika gridi ya Taifa.
“Awali, mikoa ya kusini kule walikuwa na tatizo la umeme tukachukua mtambo hapa Ubungo tukafunga Mtwara mambo yakawa mazuri,” amesema Dk Biteko.
“Wito wangu kwa Tanesco tusilale, Watanzania wanataka umeme tuwape umeme, raha yetu iwe kuona umeme kila wakati umeme wanawake kama kuna sehemu ina tatizo ituume wote itusumbue kama inavyowasumbua Watanzania.”
Awali, akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Mkuu, Philipo Lalisa ambaye ni Meneja wa Operesheni katika kituo cha gridi Taifa, amesema mpaka sasa Tanzania ina akiba ya umeme kati ya megawati 250 hadi 350.