ILIKUWA wikiendi njema kwa timu ya Caravans C baada ya kutwaa ushindi wa wiketi 3 dhidi ya Specialised K&P katika mchezo wa Ligi ya Kriketi ya Mkoa uliopigwa kwenye Uwanja wa Leaders, jijini Dar es Salaam.
Ni Ligi ya Kriketi ya mizunguko 30 kwa timu za daraja B kwa mujibu wa msemaji wa Chama cha Kriketi nchini (TCA), Atif Salim.
Katika mchezo huo, Specialised K&P ndio walioshinda kura ya kuanza na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 144 baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 27 kati ya 30 iliyopangwa.
Baada ya jitihada kubwa, vijana wa Caravans waliweza kuzifikia alama hizo kwa kutengeneza mikimbio 148 huku wakipoteza wiketi 7 na kutumia mizunguko 27 kati ya 30 iliyopangwa.
Arjun Kumar wa Caravans ndiye aliyeng’ara kwa utengezaji wa mikimbio baada ya kupiga mikimbio 34 akifuatiwa na mwezake Abhishek Sinha aliyeiletea timu yake mikimbio 26.
Lakini mambo yalikuwa tofauti kwa Caravans D ambayo siku hiyo hiyo ilipoteza kwa Dar Tigers pia ya jijini.
Ikicheza kwa ujasiri mkubwa, Dar Tigers iliizima Caravans D kwa mikimbio 23 katika mchezo mkali wa Ligi hiyo ya Kriketi ya Mkoa.
Dar Tigers walishinda kura ya kuanza na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 170 huku wakiangusha wiketi 8 katika mchezo ambao walitumia mizunguko yote 20 iliyowekwa.
Licha ya juhudi kubwa ya vijana wa Caravans kutaka kuzifikia alama za wapinzani wao, mambo hayakuwa mazuri kwao kwani waliweza kufikia mikimbio 147 baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 19 kati ya 20 na hivyo kushindwa kwa mikimbio 23.
Christopher Van De Merwe alipata mikimbio 46 na Ani Zat aliyetengeneza mikimbio 31 walichangia sana katika kuifranya Dar Tigers kushinda mchezo huo.
Chama cha Kriketi nchini ndiyo waandaji wa ligi zote za kriketi zinazoendelea kwenye viwanja mbalimbali jijini Dar es Salaam.