Pwani. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax ametaja umuhimu wa mazoezi ya medani yaliyofanyika kwa siku 14 kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (CPLA).
Amesema mazoezi hayo ya Amani, Umoja 2024 yameimarisha uwezo, uzoefu na ujuzi katika sekta ya ulinzi ya Tanzania kwa kuwa yamehusisha teknolojia ya hali ya juu.
Waziri Tax amesema hayo leo Jumapili Agosti 11, 2024 wakati akifunga mazoezi hayo ya medani yaliyopewa jina la Amani Umoja 2024, katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi CTC Mapinga kilichopo Mapinga wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Mazoezi hayo ya pamoja ambayo yalizinduliwa Julai 29, 2024 yamehusisha anga na ardhi huku askari wakitumia magari ya vita (Deraya), shabaha, kuzuia magaidi sambamba na kuokoa watu mashuhuri.
“Mnapoleta nguvu ya pamoja mnabadilishana uzoefu na kama mnavyoona dunia inakwenda haraka sana katika teknolojia kwa hiyo mnapokuwa pamoja mnaona wenzetu wanafanya nini.”
“Kuna matishio ya amani pia yanabadilika kwa hiyo mazoezi kama haya ni muhimu kwa kuwa yameimarisha uhusiano tuliokuwa nao tangu uhuru,” amesema Tax.
Pia, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob Mkunda amesema manufaa ambayo Tanzania imeyapata ni kuongezeka uwezo wa JWTZ.
Amesema kutokana na zoezi hilo wanajeshi wa Tanzania wameimarika katika maeneo kama shabaha, pia wamepata hamasa kwa kuwa hawakufanya muda mrefu na wenzao kutoka nje.
“Tumeweza kutathmini uwezo wa Jeshi letu vijana wana molari, wamefanya vizuri, wamelenga shabaha vizuri, jambo lingine tumeongeza ushirikiano ambao umewekwa na waanzilishi wetu,” amebainisha Jenerali Mkunda.
Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema mazoezi hayo yalikuwa yamegawanyika katika awamu mbili za majini na nchi kavu.
Amebainisha kwa upande wa majini yalifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara, Mafia, Unguja na Pemba.
“Askari wamepata mafunzo ya kukabiliana usafirishaji binadamu, uvuvi haramu na shughuli zote zinazokiuka sheria zinazofanyika ukanda wa Pwani,” amesema Meja Jenerali Mhona.
Aidha amesema mafunzo hayo yameongeza, umahiri kwa askari kukabiliana na matukio ya kigaidi, utekaji na kuongeza ujuzi kwa askari wa majeshi yote mawili.
Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Ukombozi wa watu wa China CPLA, Meja Jenerali Ye Dabin amesema mazoezi haya yanaongeza ushirikiano kati ya majeshi hayo mawili yaliyodumisha umoja kwa zaidi ya miaka 60.
Aidha, mbali na kuhudhuriwa na Waziri wa Ulinzi pamoja na CDF, vilevile waambata jeshi wa majeshi rafiki ikiwemo kutoka Uingereza, India, Rwanda na Marekani wameshuhudia hafla ya ufungaji.
Hata hivyo hii ni mara ya nne Jeshi la Wananchi la Tanzania na Jeshi la Ukombozi wa watu wa China, wanafanya mazoezi, walifanya
mwaka 2014, 2019 kwenda 2020, 2023 na mwaka huu 2024.