Watatu walivyombaka na kumlawiti mtoto wa darasa la sita

Moshi. Ni ushetani au ni changamoto ya afya ya akili? Hili ni swali linaloumiza wengi kwa sasa baada ya wanaume watatu wilayani Rombo, kumbaka mtoto anayesoma darasa la sita kwa miezi mitatu mfululizo wakipeana zamu kufanya ufedhuli huo.

Lakini sheria imechukua mkondo wake, baada ya kushindwa kupangua adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela walichohukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Rombo mwaka 2018, baada ya rufaa zao zote mbili kugonga mwamba kortini.

Hukumu ya rufaa ya mwisho ilitolewa Agosti 9, 2024 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambayo ndio chombo cha mwisho cha rufaa katika makosa ya jinai, ambayo ilisisitiza mashitaka dhidi yao yalithibitishwa pasipo mashaka yoyote.

Jopo hilo la majaji watatu, Winfrida Korosso, Lucia Kairo na Amour Khamis limezitupilia mbali sababu zote saba za warufani, Abdul Mramba, Otto Mushi na Annania Massawe, wakisema kifungo hicho ni sahihi kwa kosa walilolitenda.

Majaji hao walisema wanakubaliana na hoja za wakili wa Serikali mwandamizi, Veridiana Mlenza aliyesaidiana na mawakili wa Serikali Peter Utafu na Edith Msenga, kuwa Jamhuri ilithibitisha shitaka hilo katika viwango vinavyokubalika.

Ushetani ulivyogundulika shuleni

Katika hati ya mashitaka, upande wa mashitaka ulieleza katika tarehe na muda usiojulikana wa Mei 2018 katika Kijiji cha Alehi chini Wilaya ya Rombo, mrufani wa kwanza, Mramba alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12.

Shitaka la pili, Jamhuri ilieleza kuwa katika tarehe na muda usiojulikana Juni 2018, mrufani wa tatu Annania Massawe naye alimbaka mtoto huyo na katika shitaka la tatu, mrufani wa pili Mushi alitenda kosa kama hilo Julai 2018.

Julai 18, 2018, kuliitishwa kikao cha wazazi katika Shule ya Msingi Booni ambacho kilijadili masuala ya chakula kwa watoto na masuala mengine ya kitaaluma na ndipo iliibuka hoja ya baadhi ya watoto kuwa na tabia mbaya.

Mmoja wa walimu wa shule hiyo, alimtaja mmoja wa watoto hao kuwa ni huyo aliyebakwa aliyekuwa darasa la sita, na tuhuma zilizoelezwa ni kuwa amekuwa akijihusisha katika vitendo vya kimapenzi na wanaume tofautitofauti kijijini hapo.

Bibi wa mtoto huyo ambaye alihudhuria kikao hicho, aliwaeleza walimu wasiwasi wake juu ya mjukuu wake huyo kutokana na tabia yake, kwani amekuwa akivinjari kijijini hapo pasipo kumsaidia kazi za nyumbani kama watoto wenzake.

Kutokana na maelezo hayo, mtoto huyo pamoja na mdogo wake waliitwa na kuhojiwa ambapo alikiri kufanya mapenzi na wanaume kijijini hapo na kuwataja wabakaji hao watatu kuwa ndio wanahusika kufanya naye mapenzi.

Uongozi wa shule ulifuatilia suala hilo ambapo Julai 2018 uliwaita watuhumiwa shuleni, ukawahoji na kisha kuwakabidhi Polisi kwa hatua zaidi za uchunguzi ambapo baada ya upelelezi kukamilika walifunguliwa mashitaka ya kubaka.

Ushahidi utakaokutoa machozi

Katika ushahidi wake alioutoa kortini, mtoto huyo alieleza kuwa mrufani wa pili, Otto Mushi, ndiye alikuwa wa kwanza kuanza kumbaka.

Alieleza kortini kuwa Mei 2018, akiwa njiani kwenda nyumbani kutoka shuleni, alikutana na mbakaji huyo ambaye alimtaka aende kulala nayo nyumbani kwake, lakini alikataa ombi hilo na kwenda nyumbani kwao moja kwa moja.

Hata hivyo, baada ya kufika nyumbani, babu yake alimtuma kwa Mushi ili kumnunulia sigara aina ya Sonyo na alipofika mbakaji huyo akamtaka aingie ndani ili ampe sigara na alipoingia, badala yake alifunga mlango na kumbaka.

Mtoto huyo alieleza kuwa ndani ya nyumba hiyo kulikuwa hakuna watu wengine hivyo mrufani huyo alimvua nguo kisha na yeye kuvua na kumlaza kitandani na alijaribu kupinga alishindwa, ndipo akambaka na alipomaliza akamlawiti.

Alieleza kuwa alisikia maumivu na kilio chake hakikusikika hadi mbakaji huyo alipomaliza kufanya kitendo chake hicho cha kishetani, na alipotizama kitandani aliona matone ya damu na mkojo wa njano na ni tukio lililochukua dakika 30.

Mushi hakumpa sigara aliyokuwa ameahidi kumpa na aliporudi nyumbani alimweleza babu yake nini kimemtokea lakini hakuchukua hatua yoyote ndipo akamweleza bibi, lakini alimjibu kuwa atamfuta mrufani huyo na kumkanya.

Kulingana na ushahidi wake, Mushi aliendelea kufanya naye ngono na kumlawiti na wakati mwingine alikuwa akiwakaribisha marafiki zake wawili, Abdul Mramba na Annania Massawe, nyumbani kwake kumbaka pamoja na mdogo wake.

Baada ya miezi kadhaa kupita alizoea mchezo huo na alipokuwa akiitwa na Mushi alikuwa akienda na kufanya naye mapenzi, na huo mchezo uliendelea pia kwa marafiki zake hadi walipokamatwa.

Julai 20, 2028, daktari alimfanyia uchunguzi mtoto huyo na kubaini michubuko katika sehemu zake za siri na kwamba uke wake ulikuwa mpana kuliko umri wake na kulikuwa na kitu butu ambacho kilikuwa kimeingia katika uke huo.

Hukumu na rufaa yao ilivyokuwa

Baada ya upande wa mashitaka kumaliza kufunga ushahidi wao, Mahakama iliwaona warufani wote watatu wana kesi ya kujibu ambapo walijitetea na kukanusha kutenda kosa, lakini mwisho walitiwa hatiani na kutupwa jela miaka 30.

Hata hivyo, hawakuridhika na hukumu hiyo wakakata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ambayo ilitupwa kwa maelezo kuwa haikuwa na mashiko lakini hawakukata tamaa, wakakata rufaa Mahakama ya Rufani nayo ikatupwa.

Katika rufaa yao Mahakama ya Rufani, waliegemea hoja nane ikiwamo kuwa kulikuwa na utofauti kati ya hati ya mashitaka na ushahidi uliotolewa, dosari katika hati ya mashitaka na kushindwa kuthibitisha umri wa mtoto huyo.

Mbali na hoja hizo, walidai kuwa mahakama haikuzingatia sheria za mwenendo wa makosa ya jinai (CPA), na sheria ya ushahidi, kushindwa kupima kikamilifu ushahidi wa mashahidi uliokuwa na mkanganyiko na kwamba kesi haikuthibitishwa.

Hata hivyo, katika hukumu yao, jopo la majaji hao watatu walitambua sababu moja baada ya nyingine na kueleza kuwa hazikuwa na mashiko kwani Jamhuri ilithibitisha kesi hiyo kwa viwango vinavyokubalika na bila kuacha mashaka yoyote.

Majaji hao walisema baada ya kupitia mwenendo wa kesi, wamejiridhisha kuwa upande wa mashitaka ulithibitisha mashitaka dhidi yao kutokana na ushahidi wa shahidi wa pili  na  wa tatu na walithibitisha uke wa mtoto huyo ulikuwa umeingiliwa.

Kulingana na majaji hao na kwa kuegemea ushahidi uliotolewa wakati kesi hiyo ikisikilizwa Mahakama ya Wilaya ya Rombo, hakuna watu wengine waliofanya mapenzi na mtoto huyo isipokuwa warufani hivyo adhabu waliyopewa inastahili.

Related Posts