Wawili wapoteza maisha kwa kushambuliwa na fisi

Sengerema. Watu wawili wamepoteza maisha baada ya kushambuliwa na fisi saa tano usiku wa kuamkia leo Jumapili Agosti 11, 2024 katika Kitongoji cha Kabusuli, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kabusuli, Halfan Shindile ameiambua Mwananchi Digital kuwa waliofariki dunia ni pamoja na Devid Thobias (42) mkazi wa Kijiji cha Kalumo na mtu mwingine jina lake halijafahamika.

Amesema taarifa za awali zinaonyesha marehemu walikuwa wakitokea Kijiji cha Igalagalilo wakielekea kijiji cha Kalumo. “Walipofika kijiji cha Kabusuli wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki, walivamiwa na kundi la fisi na kushambuliwa hadi wakapoteza maisha,” amesema Shindile.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kabusuli, Alfred Kombo amesema eneo hilo lina makundi ya fisi yanayohatarisha maisha ya watu na ametoa wito kwa jamii kuchukua tahadhari wanaposafiri usiku.

Amesema miili ya marehemu hao imepatikana umbali wa mita 100 kutoka eneo la tukio, ikiwa imejeruhiwa maeneo mbalimbali.

Tabu Mazigo, mkazi wa kitongoji cha Kabusuli, amesema alisikia watu wakipiga mayowe wakiomba msaada, lakini alipotoka nje aliona kundi kubwa la fisi likiwashambulia akarudi ndani kwa hofu.

“Nikashindwa kutoka, fisi walikuwa wengi, lakini baadhi ya majirani nao kumbe walisikia walioweza wakatoka ila walikuwa wameshachelewa wakakuta tayari wameshawaua na waliwaburuza mbali kidogo kutoka hapa walipowavamia,” amesema Mazigo.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga alipopigiwa simu azungumzie tukio hilo amesema yuko njiani anaelekea eneo la tukio na atatoa taarifa zaidi baada ya kufika.

Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi kwa habari zaidi

Related Posts