WHO yaalika wazalishaji chanjo za dharura kupambana na homa ya nyani

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limewataka watengenezaji wa chanjo ya ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) kuwasilisha nyaraka kuhusu chanzo zilizoleta mafanikio ya kukinga ugonjwa huo  kwa ajili ya tathmini ya dharura (EUL).

WHO imesema virusi vya clades 1 vinavyosababisha ugonjwa huo vinavyosambaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), vimejibadilisha na kuibuka vingine vya clade 1b ambavyo husababisha ugonjwa mkali zaidi.

Hatua hiyo imemlazimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalamu ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika wanaosimamia afya, lishe, idadi ya watu na udhibiti wa dawa, Ummy Mwalimu kutoka Tanzania kuwatangazia mawaziri wote wa afya barani Afrika, wanatakiwa kukutana mwishoni mwa Agosti 2024 kujadili mlipuko huo ulioenea katika nchi tisa.

Akitoa taarifa mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus ametangaza kwamba wameanzisha mchakato wa EUL ya chanjo ya Mpox, kutokana na mienendo inayotia wasiwasi katika kuenea kwa ugonjwa huo.

“Kuna mlipuko mbaya na unaokua katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao sasa umeenea katika nchi jirani. Aina mpya ya virusi, ambayo iliibuka kwa mara ya kwanza Septemba 2023, imegunduliwa nje ya DRC,” ameeleza Dk Tedros.

Amesema utaratibu wa EUL ni mchakato wa kuidhinisha matumizi ya dharura, iliyoundwa mahususi ili kuharakisha upatikanaji wa bidhaa za matibabu zisizo na leseni, kama vile chanjo zinazohitajika katika hali za dharura za afya ya umma.

Dk Tedros amesema hilo ni pendekezo la muda mfupi, kulingana na mbinu ya faida ya hatari.

WHO inaomba watengenezaji kuwasilisha takwimu ili kuhakikisha kuwa chanjo hizo ni salama, zinafaa na zina  ubora uliohakikishwa na zinafaa kwa walengwa.

Utoaji wa EUL utaharakisha ufikiaji wa chanjo hasa kwa zile nchi za kipato cha chini ambazo bado hazijatoa idhini yao ya udhibiti wa kitaifa. EUL pia huwezesha washirika ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (Unicef) na Shirika la uzalishaji chanjo duniani (Gavi), kupata chanjo kwa ajili ya usambazaji.

Mpox ni ugonjwa wa virusi unaosababishwa na virusi vya monkeypox, aina ya Orthopoxvirus ya jenasi. Mpox inaweza kuambukizwa kwa binadamu kwa kugusana kimwili na mtu ambaye ameambukizwa, kwa nyenzo zilizoambukizwa au wanyama walioambukizwa.

Kwa sasa kuna chanjo mbili zinazotumika dhidi ya ugonjwa huo, ambazo zote zimependekezwa kutumiwa na kikundi cha wataalamu wa ushauri wa kimkakati wa WHO.

WHO imesema kwa miaka mingi clade 1 vimekuwa vikisambaa nchini DRC, huku clade 2 vilisababisha mlipuko kimataifa kuanzia mwaka 2022.

Shirika hilo limesema mlipuko wa sasa mashariki mwa DRC unasababishwa na kujibadilisha kwa virusi vya clade 1 na kuibuka vya clade 1b ambavyo husababisha ugonjwa mkali zaidi kuliko clade 2.

Mawaziri wa Afya kukutana

Kufuatia mlipuko huo, mawaziri wa afya wa nchi za Afrika wanatarajiwa kukutana kwa dharura kabla ya mwishoni mwa Agosti kujadiliana, kupitisha mikakati pamoja na kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na mlipuko huo barani Afrika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalamu ya Mawaziri wa Umoja wa Afrika wanaosimamia afya, lishe, idadi ya watu na udhibiti wa dawa, Ummy Mwalimu ametoa uamuzi huo Agosti 9, 2024 wakati wa kufunga kikao cha tano cha kamati mahususi ya kitaalamu ya mawaziri wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) Jijini Addis Ababa, Ethiopia.

“Nimefikia uamuzi huu baada ya kikao hiki kupokea taarifa ya Taasisi ya African (CDC) kuhusu hali ya ugonjwa wa Mpox barani Afrika ambapo ilielezwa kuwa takriban nchi tisa za Afrika zina wagonjwa na hivyo kuwepo hatari ya kusambaa katika nchi nyingine za Afrika,” amesema Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya, Tanzania.

Amesema, taarifa ya African CDC ilionyesha kuwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai, 2024 jumla ya watu 14,250 wameathirika na ugonjwa huo na kati ya hao watu 456 wamefariki.

Tanzania ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Agosti, 2024 hadi Agosti, 2026.

Related Posts