ILIPOPIGWA Simba katika nusu fainali kwa bao 1-0, Azam FC nayo ikajipanga kuja kulinda heshima, lakini kilichowakuta hadi unavyosoma gazeti hili hawajui kilichotokea wakipoteza kwa kipigo kizuto cha mabao 4-1, huku mabingwa wakiuliza ‘kuna mwingine huko?’
Yanga jana ikitoka nyuma kwa bao 1-0 na kupindua meza na kushinda kibabe ikilirudisha taji la Ngao ya Jamii ililopokonywa msimu uliopita na Simba pale Tanga, mabingwa hao wakianza msimu kibabe.
Katika mchezo wa jana timu zote zilicheza soka tamu lenye kasi na ushindani, lakini ni Yanga iliyoendelea kuonyesha ubora kwa namna ilivyocheza kwa kujiamini na kufanya mashambulizi mwanzo mwisho, huku Azam ikijichanganya eneo la ulinzi, hasa kipindi kwa kwanza kabla ya kutulia kipindi cha pili.
Azam iliyotoka kuifumua Coastal Union kwa mabao 5-2 katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa visiwani Zanzibar, hiki ni kipigo cha kwanza kikubwa kukipokea kutoka kwa Yanga tangu ipande daraja, huku Yanga ikilipa kisasi ilichowahi kupewa cha idadi kama hiyo ya mabao katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Mechi hiyo ya jana ilizikutanisha timu zote zitakazowakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na pia timu zilizomaliza nafasi mbili za juu ya Ligi Kuu msimu uliopita na hata katika Kombe la Shirikisho (FA), huku Yanga wakiwa wababe kotekote.
Yanga imerejesha taji hilo ililolipoteza kwa Simba msimu uliopita kwa kufungwa katika fainali iliyopigwa jijini Tanga, baada ya kulishikilia kwa misimu miwili mfululizo nyuma.
Alikuwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ kiungo wa zamani wa Yanga akitangulia kufungua ukurasa wa mabao akifunga bao safi la dakika ya 13 akipokea pasi ya winga Djibril Sillah, wakati Azam ikifanya shambulizi la haraka langoni kwa wapinzani wao.
Bao hilo linakuwa la tatu kwa Fei Toto dhidi ya Yanga tangu atue Azam akitokea Wananchi hao ambapo jana baada ya kufunga aliwatambia mashabiki wa timu hiyo ya zamani akiwaambia watamtambua huku akiwaonyesha namba ya jezi yake mgongoni, lakini mashabiki hao wakatulia na kuwapongeza wachezaji wao kwa kuwapigia makofi, wakiwarudisha mchezoni.
DUBE AMEANZA, BAO LA AZAM
Wakati Azam wakifurahia bao hilo, furaha yao ikaishi kwa dakika tano tu, kwani dakika ya 19 mshambuliaji wao wa zamani Prince Dube akawarudisha kati akiisawazishia timu hiyo mpya katika pambano hilo la kwanza dhidi ya mabosi hao wa zamani.
Bao hilo litawauma sana Azam sio tu kwamba limefungwa na Dube lakini pasi iliyotengeneza goli ilitoka kwa kiungo wao wa zamani pia Mudathir Yahya, akiipenyeza asisti ya kiufundi kutoka katikati ya uwanja.
Wakati Azam wakirudi kati baada ya bao la Dube, mshambuliaji huyo akakutana na Fei Toto kisha kiungo huyo kumpongeza raia huyo wa Zimbabwe kwa kumpa mkono.
Baada ya bao hilo wakati Azam ikijiuliza ikajikuta inaruhusu mabao mawili ya haraka, lakini yote mabeki wake wawili tofauti wakishiriki kuyasindikizia wavuni kufuatia krosi na shuti kali la wachezaji wa Yanga.
Beki Yoro Diaby akaitengenezea Yanga bao la pili akijifunga katika dakika ya 28 kufuatia krosi kali ya beki Chadrack Boka aliyepandisha mashambulizi kwa kasi kubwa na katika dakika ya 30, Yannick Bangala aliyewahi kuichezea Yanga misimu miwili iliyopita naye akausukumia wavuni kwa kifua mpira wa shuti kali la kiungo Stephanie Aziz KI, shambulizi lililotokana na mpira wa kona.
Kocha Youssouf Dabo ambaye hivi karibuni alitoka kujiongezea ujuzi wa taaluma yake, alianza mchezo huo na mfumo wa 3-5-2 akiwapanga mabeki watatu Bangala, Diaby ya Fuentes Mandoza ambao walionekana kupata shida dhidi ya Yanga ambao waliwashambulia kwa nguvu.
Baada ya kugundua hilo Dabo akafanya mabadiliko ya haraka akimtoa Diaby aliyeanza kuonekana kuumizwa na bao lake la kujifunga na kumuingiza winga Frank Tiesse na kubadilisha mfumo wakirudi kwenye ule wa 4-4-2.
Licha ya mfumo, lakini Azam katika kipindi cha kwanza walicheza bila nidhamu hasa baada ya kupata bao na kujiachia, hali iliyoacha mashimo mengi ya kupenya kwa safu inayotisha kwa mashambulizi ya Yanga ikiongozwa na Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Prince Dube waliokuwa wakiisumbua kwa muda mrefu.
Huu ni ushindi wa tano kwa Yanga mbele ya Azam katika Ngao ya Jamii tangu zilizopoanza kukutana 2013 zikiwa zimekutana mara sita, Wanalambalamba wakishinda mara moja tu, pia ni Ngao ya nane kwa Vijana wa Jangwani tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 2001 ikiwa nyuma ya Simba iliyotwaa mara 10.
Msimu uliopita timu hizo zilikutana katika mechi ya nusu fainali kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Yanga kulala 2-0.
Mara baada ya mchezo huo wa fainali ya jana timu hizo sasa zinaenda kujiandaa kwa mechi za kwanza za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazopigwa wikiendi hii, Yanga ikitarajiwa kuvaana na Vital’O ya Burundi, huku Azam ikivaana na Wanafainali ya Kombe la Kagame 2024, APR ya Rwanda.
Timu hizo zitarudiana na wapinzani wao hao kisha ndipo waanze kuliamsha katika Ligi Kuu Bara inayoanza Ijumaa hii kwa pambano la Pamba Jiji iliyopanda daraja msimu huu itakayoialika Tanzania Prisons, jijini Mwanza, zikipangwa kuanzia ugenini.
Yanga ambao ndio watetezi wa ligi hiyo imepangwa kucheza na Kagera Sugar Agosti 29, siku moja baada ya waliokuwa washindi wa pili, Azam kuifuata JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, jijini Dar es Salaam.
Kocha Dabo wa Azam alikiri kulikoroga kwa kuanzisha mabeki watatu dhidi ya safu ya wakali kibao ya Yanga.
“Pengine nilikosea kuanzisha mabeki watatu nyuma. Lakini tumejifunza na tunapaswa kujifunza. Hatupaswi kuendelea kucheza hivi. Unapokuwa na uongozi wa bao dhidi ya timu kama Yanga unapaswa kucheza kwa tahadhari zaidi,” alisema Dabo.
Kocha wa Yanga, Gamondi aliwapongeza wachezaji wake na mashabiki.
“Yanga ina wachezaji wenye njaa ya makombe, tutaendelea kuwa hivi. Sisi ndio Yanga,” alisema Muargentina huyo.
YANGA: Diarra, Yao, Boka, Job, Bacca, Aucho, Maxi, Mudathir/Mwamnyeto, Dube/Mzize, Aziz Ki/Chama na Pacome
AZAM: Mustafa, Lusajo, Sidibe/Msindo, Fuentes, Bangala, Yoro/Tiesse, Mtasingwa, Akaminko/Chilambo, Blanco, Fei Toto na Sillah