Kagera. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amehitimisha ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Kagera, huku kero kubwa aliyokutana nayo kwenye kila wilaya ni kutopatikana kwa vitambulisho vya Taifa vinavyotengenezwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
Katika ziara hiyo iliyoanza Agosti 6, 2024, Dk Nchimbi aliambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya CCM, akitokea Mkoa wa Kigoma ambako ametembelea Wilaya za Biharamulo, Ngara, Karagwe, Kyerwa, Misenyi, Bukoba na Muleba.
Kagera ni mkoa wa 15 aliotembelea kiongozi huyo wa chama, tangu alipoteuliwa Januari 2024 na Halmashauri Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan na amekuwa akifanya ziara za kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 2024.
Pia, amekuwa akisikiliza kero za wananchi kupitia kwa watendaji wa Serikali wanaotangulia kusikiliza kero hizo na kuziwasilisha kwa mkuu wa mkoa, ili azifanyie utatuzi na kisha kutoa taarifa ya utekelezaji kwake.
Akiwa Kagera, kero kubwa iliyojitokeza kwenye kila wilaya alipotembelea, ni wananchi kukosa vitambulisho vya Taifa, jambo linalowakwamisha kupata baadhi ya huduma muhimu kama vile kusajili laini za simu.
Changamoto hiyo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mengi ya pembezoni ambako kuna mwingiliano mkubwa na raia wa kigeni kutoka nchi jirani, hivyo mchakato wa kusajili unahusisha uhakiki wa uraia wa waombaji wa vitambulisho.
Wananchi wa Kijiji cha Kumunazi kilichopo Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, walieleza kero ya kitopatiwa vitambulisho vya Taifa vinavyotolewa na Nida, jambo linalowakwamisha kupata baadhi ya huduma muhimu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro amesema moja ya changamoto wanayokutana nayo wananchi wa Kumunazi ni kukosa vitambulisho vya Taifa kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
“Wananchi wanakosa vitambulisho vya Nida, imefika mahali watu wanaazima vitambulisho vya ndugu zao kwa ajili ya kusajilia laini za simu. Hii imekuwa kero kubwa kwa wananchi hawa.
“Ombi letu kwako, ni kuwasukuma hawa Nida na Uhamiaji watoe vitambulisho hivyo, ili wananchi waendelee kupata huduma muhimu,” amesema mbunge huyo, huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza.
Akiwa Kyerwa, kero hiyo iliwasilishwa pia na mbunge wa jimbo hilo, Innocent Bilakwate aliyeeleza kwamba wananchi wake wana kero ya kutopatiwa vitambulisho vya Taifa kama Watanzania wengine.
“Changamoto ya wananchi hawa ni pamoja na kupata vitambulisho vya Nida, tunaomba utusaidie kusukuma jambo hili ili wananchi wetu nao wapate vitambulisho hivyo,” amesema Bilakwate, huku wananchi wakimshangilia baada ya kuwasilisha kero hiyo.
Akiwa katika Wilaya ya Misenyi, mbunge wa Nkenge (CCM), Florent Kyombo ameeleza pia kuwa wananchi wake wanakabiliwa na changamoto ya vitambulisho vya Taifa, huku akisema Jeshi la Uhamiaji linawanyanyasa wananchi wanapotafuta vitambulisho hivyo.
“Tunaomba Jeshi la Uhamiaji lihudumie watu kwa weledi, watu wetu wanapata manyanyaso kutoka kwa askari wa Uhamiaji, wanatumia lugha chafu kwa wananchi. Tunataka watu wenye sifa wapewe vitambulisho vyao bila kusumbuliwa,” amesema mbunge huyo.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mikutano hiyo, wameshangazwa Nida kutowapatia vitambulisho hivyo, licha ya kwamba wamekamilisha mahitaji yote muhimu.
“Kwa kweli hili suala la vitambulisho ni gumu kwani kati ya watu 10, utakuta wenye vitambulisho hivyo ni wawili au mmoja. Wote hapa uwanjani ukiwauliza kama wana vitambulisho, watakwambia hawana. Hatujui shida iko wapi huku kwetu,” amesema Marius Kyamoli, mkazi wa Kata ya Nkenda wilayani Kyerwa.
Kutokana na kuibuka kwa kero hiyo kwenye kila wilaya, Katibu Mkuu, Dk Nchimbi amemuelekeza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo kuungana naye kwenye ziara hiyo, ili ajibu kero za wananchi zinazohusu wizara yake, likiwamo suala la vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wa mkoani Kagera.
Jana Jumamosi, Agosti 10, 2024, naibu waziri huyo alitekeleza agizo la Dk Nchimbi kwa kuungana na msafara wake na alishiriki mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mayunga, Bukoba Mjini na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Sillo amesema baada ya maagizo ya Dk Nchimbi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimwelekeza aje kumwakilisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ambaye yuko nje ya nchi na kujibu kero za wananchi katika mikoa ya Kagera na Kigoma.
Amesema kati ya mwaka 2021/22, kulikuwa na tatizo la upatikanaji wa kadi ghafi za vitambulisho. Hata hivyo, amesema Serikali ilitenga Sh42.5 bilioni kwa ajili ya kutengeneza vitambulisho hivyo nchi nzima na Oktoba 2023 walianza uzalishaji.
“Namwelekeza ofisa wa Nida Mkoa wa Kigoma, Ofisa wa Nida Mkoa wa Kagera, maofisa wa Nida katika kila wilaya katika mikoa hiyo, kuhakikisha wanafanya utambuzi, kusajili na kutoa vitambulisho kwa haraka ili wananchi wapate huduma,” amesema Sillo.
Ameongeza kuwa hadi sasa kuna vitambulisho 78,779 havijachukuliwa na wananchi katika mikoa hiyo, hivyo ametoa wito kwa maofisa wa Nida kuhakikisha wananchi wanapata vitambulisho vyao mara moja.
Makumbusho ya vita vya Kagera
Akiwa wilayani Misenyi, Katibu Mkuu, Dk Nchimbi aliwapongeza wananchi wa Kagera kwa ushiriki wao kwenye vita kati ya Tanzania na vikosi vya nduli Idd Amin wa Uganda, huku akiielekeza Serikali kujenga makumbusho maalumu kama kumbukumbu ya vita hiyo.
Lengo la kuwa na makumbusho ni kuhifadhi historia hiyo kwamba, Tanzania iliwahi kupigana vita na adui yake na ikashinda. Pia, amesema lengo lingine ni kuieleza dunia kwamba Watanzania walikuwa wamoja wakati wa vita hiyo iliyopigana mwaka 1978 – 1979.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wilayani humo, Dk Nchimbi amewapongeza Watanzania wote hususani wakazi wa Kagera kwa kujitoa katika vita hiyo hadi walipofanikiwa kumng’oa Amin madarakani na kulinda mipaka ya Tanzania, hasa katika Mkoa wa Kagera.
“Serikali ihakikishe makumbusho ya vita kati ya Tanzania na vikosi vya Amin yanajengwa, ili kulinda historia hii. Lengo la kuwa na makumbusho hii si tu kuonyesha kwamba Tanzania iliwahi kupigana na Amin, bali pia kuonyesha namna Watanzania walivyokuwa wamoja,” amesema Dk Nchimbi.
Amesisitiza wakati wa vita hiyo, Watanzania walionyesha umoja wa hali ya juu kwa kuchangia gharama za vita hiyo.
Pia, amesema wapo waliochangia ng’ombe, wengine walitoa vyakula na hata fedha ili kuhakikisha malengo ya nchi katika vita hiyo yanatimia.
Maagizo Wizara ya Maliasili
Katika hatua nyingine, Katibu mkuu huyo wa CCM, amemuelekeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki kuifanyia kazi na kupata ufumbuzi wa changamoto ya wanyama waharibifu wanaovamia makazi ya watu, kuharibu mazao na kutishia uhai wa binadamu katika Wilaya ya Karagwe.
Akiwa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa, Dk Nchimbi alipokea malalamiko ya wananchi kuhusu kuvamiwa na wanyamapori wanaohatarisha usalama wao na mali hasa mazao.
Malalamiko hayo kuhusu wanyama wakali yametolewa na wananchi wa vijiji vya Kata ya Kihanga (Kihanga, Kibwela na Mshabaiguru), ambako wamedai tembo wanavamia mashamba ya wakulima, kuharibu mazao na kuhatarisha maisha wa wananchi katika maeneo yao.
Dk Nchimbi ametaka changamoto hiyo ishughulikiwe haraka, ikiwamo kutafuta namna ya kudhibiti wanyamapori hao ili wasiendelee kuleta madhara kwa wananchi na katika shughuli zao za kilimo.
Awali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Zainab Katimba amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuondoa changamoto kwenye sekta za afya na elimu, ili kuwawezesha wanafunzi kupata huduma hizo kwenye maeneo yao.
“Serikali imetoa fedha za kutosha kwenye kila wilaya katika mkoa huu, vituo vya afya vinajengwa, shule zinajengwa kila kona na pia barabara hadi vijijini,” amesema Katimba.
Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Organaizesheni, Issa Gavu Haji amewataka wananchi wa Kagera kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura ili waweze kuchagua viongozi wanaowataka uchaguzi ukifika.
“Mwaka huu tuna uchaguzi wa Serikali za mitaa, jitokezeni kujiandikisha kwenye daftari la ukaazi na daftari la wapigakura, ili mpate haki yenu ya kuchagua viongozi mnaowataka,” amesema Gavu.
Kutokana na kupaa kwa bei ya kahawa mkoani Kagera, Dk Nchimbi ameipongeza Serikali kusimamia jambo hilo kwa masilahi ya wakulima mkoani humo, huku akiitaka iendelee kusimamia ili isishuke.
Pongezi hizo zilitolewa baada ya mbunge wa Kyerwa (CCM), Innocent Bilakwate kueleza namna wakulima wanavyonufaika na kahawa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuelekeza kahawa kuuzwa kwenye minada.
Amesema kahawa ilikuwa inaporomoka lakini wakulima walipoanza kuuza kwenye minada, bei ya zao hilo imepanda kutoka Sh1,300 kwa kilo mwaka 2022, Sh2,300 mwaka 2023, hadi kufikia Sh5,000 mwaka huu.
“Wananchi wangu wa Kyerwa wanaishukuru Serikali kwa kuwasaidia kupandisha bei ya kahawa na sasa wakulima wanauza kahawa zao kwenye mnada kwa bei ya Sh5,000 kwa kilo, hii ni hatua kubwa,” amesema Bilakwate.
Akizungumzia suala la kahawa, Dk Nchimbi ameeleza kuongezeka kwa bei ya kahawa ni matokeo mazuri ya usimamizi wa Serikali katika zao hilo, ili iwanufaishe wakulima.
“Serikali iendelee kusimamia biashara ya kahawa ili bei iendelee kuwa nzuri,” amesema Dk Nchimbi wakati wa mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi.
Katika hatua nyingine, mkazi wa Kata ya Nkenda, Amon Kamala amesema changamoto yao kubwa ni ubovu wa barabara unaowakwamisha kufanya biashara kwa haraka na kuifungua wilaya hiyo kwa kuruhusu watu wengi kwenda kufanya biashara.
“Barabara yetu inayounganisha Wilaya za Kyerwa na Karagwe ni mbovu sana, tunaomba Serikali itujengee barabara hii kwa kiwango cha lami ili maisha yetu yawe rahisi,” amesema Kamala.
Akizungumzia barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa amesema mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika na mkandarasi amepatikana, kilichobaki ni kumkabidhi eneo atakaloweka makazi yake ya kuhifadhia vifaa.
“Ndugu Katibu Mkuu, nikuahidi baada ya ziara yako, nitarejea hapa Nkenda kwa ajili ya kumkabidhi mkandarasi eneo atakalojenga kambi yake ili aanze kazi,” amesema Bashungwa.