ACT WAZALENDO WALAANI NA KUKEMEA KUKAMATWA KWA VIONGOZI WA CHADEMA – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

 

Chama cha ACT Wazalendo kimelaani na kukemea kwa nguvu zote kile walichokiita kuwa ni vitisho vya Jeshi la Polisi kwa kuwakamata viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuzuiwa kwa kongamano la vijana wa chama hicho (BAVICHA) katika kuadhimisha siku ya vijana Duniani lililopangwa kufanyika leo, Agosti 12.202 mkoani Mbeya.

 

 

Taarifa ya ACT Wazalendo iliyotolewa na Kiongozi wa chama hicho Dorothy Manka Semu leo, Jumatatu Agosti 12.2024 imeeleza kuwa chama cha ACT Wazalendo kinapinga vikali kitendo hicho kwa kuwa kinakiuka Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa watu kukusanyika.

 

 

Aidha, ACT Wazalendo imeeleza masikitiko yake kuona kile walichodai kuwa ni hila zinazofanywa na Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini vya kuwakamata viongozi wakuu wa chama CHADEMA, kuzuia zaidi ya vijana 150 wakiwa njiani kuelekea Mbeya na leo Polisi kuzingira uwanja wa Ruanda Nzovwe ulioko jijini Mbeya.

 

 

Taarifa imeendelea kudai kuwa, vitendo hivyo vinafufua hofu ya kurejeshwa kwa kasi mazingira kandamizi kwa vyama vya siasa vya upinzani kufanya shughuli zao kwa uhuru

 

 

“ACT Wazalendo tunachukulia kwamba hila hizi zinazofanywa na Jeshila la Polisi dhidi ya viongozi wa CHADEMA ni tishio kwa vyama vyote makini vya upinzani na demokrasia ya vyama vingi nchini, tukio hili na mengine yanayofanywa na dola yanakinzana na falsafa za R4 (Ustahimilivu, Naridhiano, Mabadiliko na Kujenga Taifa jipya) za Rais Samia” – ACT Wazalendo.

 

 

Aidha, wamedai kuwa vitendo hivyo vinaonesha hatua vhache za kuimarisha uhuru wa kujumuika, kukusanyika na kujieleza vipo mashakani

 

 

Kufuatia hilo, ACT Wazalendo imetoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kuwaachia huru viongozi wote wa CHADEMA inaowashikilia bila masharti yoyote na sambamba na kuacha kutumika na CCM (chama tawala) kuzuia kazi za vyama vya siasa vya upinzani, hiyo ikienda sambamba na kutoa wito kwa wadau wote na wapenda amani na demokrasia nchini kuungana kukataa kurejeshwa kule tulikotoka kama Taifa

Related Posts