Chadema yataka waliokamatwa wasilale mahabusu leo, ACT-Wazalendo yalaani

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetaka kuachiwa huru kwa viongozi na wafuasi wake waliokamatwa kabla ya kupita usiku wa leo Jumatatu Agosti 12, 2024.

Kimedai hadi sasa jumla ya watu 443 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wengine ni Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu, John Mnyika, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho, John Pambalu na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu.

Makundi ya wafuasi na wanachama wa Chadema yamejikuta mikononi mwa Polisi kuanzia juzi, wakiwa katika mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), jijini Mbeya na yangefanyika leo Jumatatu, Agosti 12, 2024. Polisi imeyazuia kwa kile ilichokieleza kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.

Kilichosababisha kuzuiwa kwake ni kile kilichoelezwa katika taarifa ya jeshi hilo kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani na vurugu ndani yake.

Msimamo huo wa Chadema, umetolewa leo, Jumatatu Agosti 12, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, Benson Kigaila alipozungumza na wanahabari, makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

“Chadema kinataka viongozi na wanachama wote waliokamatwa waachiwe mara moja na hatutaruhusu wala kuwa tayari viongozi na wanachama walale kwenye mahabusu leo,” amesema.

Amesisitiza kuachiwa huko kunapaswa kufanyika bila masharti yoyote, huku akiwataka viongozi wa chama hicho ngazi mbalimbali watulie kusubiri maelekezo kutoka ngazi ya Taifa.

Wakati hayo yakiendelea, mkoani Iringa zaidi ya vijana 150 waliokamatwa na Polisi wameachiwa huru na kurejeshwa kwenye mikoa waliyotoka kwa kusindikizwa na jeshi hilo.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Iringa, Frank Nyalusi akizungumza na Mwananchi amesema, vijana hao wameachiwa huru saa tisa usiku wa kuamkia leo na kurejeshwa walikotoka kwa kusindikizwa na Jeshi la Polisi.

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amelaani kitendo cha viongozi hao wa Chadema na wanachama wao kukamatwa na kulitaka Jeshi la Polisi kuwaachia huru.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu Agosti 12, 2024 na Dorothy, imesema wanapinga kitendo hicho kwa kuwa kinakiuka Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa watu kukusanyika.

“Tumesikitishwa kuona hila zinazofanywa na Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa vya kuwakamata viongozi wakuu wa chama hicho, kuzuia zaidi ya vijana 150 wakiwa njiani kuelekea Mbeya na leo polisi kuzingira Uwanja Ruanda Nzovwe,” imesema.

Dorothy amesema vitendo hivyo vinafufua hofu ya kurejeshwa kwa kasi mazingira kandamizi kwa vyama vya siasa vya upinzani kufanya shughuli zao kwa uhuru.

“ACT Wazalendo tunachukulia hila hizi zinazofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya viongozi wa Chadema ni tishio kwa vyama vyote makini vya upinzani na demokrasia ya vyama vingi nchini,” amesema. 

Amesema tukio hilo na mengine yanayofanywa na dola yanakinzana na falsafa za R4 (Ustahimilivu, Maridhiano, Mabadiliko na Kujenga taifa jipya) za Rais Samia Suluhu Hassan.

“Vitendo hivi vinaonyesha hatua chache za kuimarisha uhuru wa kujumuika, kukusanyika na kujieleza vipo mashakani. Tunalitaka Jeshi la Polisi liwaachie huru viongozi wote vya Chadema wanaowashikilia bila masharti yoyote,” amesema.

Imeandikwa na Juma Issihaka, Victoria Michael na Tuzo Mapunda (Dar) na Allen Msungu (Iringa)

Related Posts