DPP amfutia mmoja kesi ya kusafirisha kilo 58.62 za heroini

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemfutia kesi na kumwachia huru, Paulina Mwanga (38), aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 58.62

Mshtakiwa huyo amefutiwa kesi hiyo, leo Jumatatu Agosti 12, 2024, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DDP), kuieleza Mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Mwanga ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi ya uhujumu uchumi namba 15/ 2023 amefutiwa kesi hiyo, huku wenzake wawili wakiendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wake kutokamilika.

Washtakiwa ambao hawajafutiwa kesi hiyo ni Goodness Remy (33) mfanyabiashara na mkazi wa Salasala na Emmanuel Chigbo (42) maarufu kama Charles au Chasi, mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi- Goba.

Mwanga amefutiwa kesi hiyo na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Maximilian Malewo, baada ya Wakili wa Serikali, Judith Kyamba kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia kuendelea mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.

Mshtakiwa huyo amefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

“Mshtakiwa wa tatu katika kesi hii, Paulina umefutiwa kesi na umeachiwa huru na Mahakama hii kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka, hana nia ya kuendelea na shauri hili dhidi yako,” amesema Hakimu Malewo.

Hakimu Malewo baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27, 2024 itakapotajwa. Washtakiwa Remy na Chigbo wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa Aprili 19, 2023 eneo la Salasala, Wilaya ya Kinondoni walikamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 58.62 kinyume cha sheria.

Related Posts