Dar es Salaam. Hofu ya kilichotokea nchini Kenya na Bangladesh, ni moja ya mambo yanayotajwa kulisukuma Jeshi la Polisi nchini Tanania, kuliwekea vikwazo Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), kufanya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Kwa mujibu wa wanazuoni wa sayansi ya siasa, tawala katika mataifa kadhaa ulimwenguni zimekumbwa na mtikisiko uliosababishwa na vuguvugu la vijana, hivyo kujenga hofu kwa wengine kutoa mwanya kama huo.
Bavicha ilitangaza kufanya maadhimisho hayo leo Jumatatu Agosti 12, 2024 katika viwanja vya Ruanda Nzovwe, jijini Mbeya, huku Makamu Mwenyekiti wa Chadema- Bara, Tundu Lissu akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Hata hivyo, alipotafutwa kuzungumzia hilo, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji amesema wapo katika mchakato wa kutoa taarifa za kina kuhusu hilo.
Pamoja na mambo mengine, ameeleza taarifa hiyo itahusisha watu wangapi wapo nao kwa kuwa walikaidi marufuku iliyotolewa na jeshi hilo.
“Muda si mrefu tutatoa taarifa tukiwa Mbeya, kueleza wangapi tupo nao kwa kuwa walikaidi marufuku,” amesema.
Shughuli hiyo pia ilikumbwa na vikwazo kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, aliyeiandikia barua Chadema ya kuitaka isitishe shughuli hiyo, ikidai kuna lugha zimetolewa na vijana wa Bavicha zinazokiuka Sheria ya Vyama vya Siasa.
Barua hiyo ya msajili ya Agosti 8, 2024 kwenda Chadema, nakala yake ilitumwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi na Jumapili, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji alizungumza na waandishi na kupiga marufuku mikusanyiko hiyo.
Katika maelezo ya barua ya msajili na ile ya Polisi pamoja na mambo mengine, walidai lugha hizo zinawashawishi vijana kutenda kama vijana wenzao wa Kenya ‘Generation Z’ ama ‘Gen Z.’
Kutokana na kukamatwa kwa viongozi hao wa Chadema, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amemwagiza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo kuzungumza na waziri wake, ili kuonua namna ya kuwaachia viongozi hao wa Chadema.
Dk Nchimbi amebainisha hayo leo Agosti 12, 2024 alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kata ya Katoro iliyopo mkoani Geita anakoendelea na ziara yake akitokea mkoani Kagera.
Amesema alifanya jitihada za kuwatafuta viongozi wenzake wa vyama vingine vya siasa, ili wawe na mazungumzo kama vyama vya siasa, hata hivyo alipata taarifa kwamba wengine wamekamatwa huko Mbeya.
“Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, ongea na waziri, tunaomba muone uwezekano wa viongozi wa vyama vya siasa waliokamatwa kule Mbeya waachiwe huru,’’ amesema.
Ingawa Chadema ilipingana na marufuku hizo, shughuli hiyo haikufanyika, badala yake makundi ya wafuasi na viongozi wake wameishia kutiwa mikononi mwa polisi.
Katika taarifa ya Chadema iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama-Bara, Benson Kigaila leo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amedai viongozi na wafuasi zaidi ya 400 wanashikiliwa na jeshi hilo katika vituo mbalimbali nchini.
Amewataja viongozi wanaoshikiliwa ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu John Mnyika, Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu na viongozi wengine wa baraza hilo.
Wengine wanaodaiwa kukamatwa ni Wakili Deogratias Mahinyila na waandishi wa habari wa Jambo Tv ambao ni Ramadhan Khamis na Fadhil Kirundwa. Pia wamo viongozi wa Bavicha, Twaha Mwaipaya, Moza Ally, Deusdedith Soka na wengine.
Mbowe na Pambalu wamekamatwa leo baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Songwe wakitokea jijini Dar es Salaam, huku Lissu, Mnyika, Sugu na viongozi wengine wa Bavicha walikamatiwa Ofisi ya Kanda ya Nyasa zilizipo Mbeya Mjini jana usiku.
Hata hivyo, Kigaila ametoa wito kwa jeshi hilo kuwaachilia viongozi na wanachama wa Chadema kabla ya usiku wa Agosti 12 kupita, huku akiwataka viongozi wa ngazi mbalimbali kusubiri maelekezo kutoka ngazi ya taifa.
Alipoulizwa watafanya nini iwapo hawataachiliwa, Kigaila amejibu kwa kifupi akisema: “Tutauvuka mto tutakapoufikia.’’
Hatua ya Jeshi la Polisi kuingilia kati shughuli hiyo ya Bavicha, imesababishwa na wasiwasi wa watawala unaotokana na mabadiliko ya mwenendo wa siasa za ulimwengu, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo.
Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, imeshuhudiwa katika mataifa mengi, ikiwemo Kenya na Bangladesh vijana wamewatikisa watawala na hata kuwaondoa madarakani.
“Hii hatua ya kuzuiwa inatokana na wasiwasi walionao viongozi juu ya uwezekano wa maandamano hayo kutengeneza nafasi ya kisiasa ya kufanya wanayotaka kuyafanya.
“Kama ilivyokuwa Kenya ilianza kama operesheni ya muswada wa fedha na baadaye ilibadilika na kuja katika sura halisi ya siasa za taifa hilo, kwa mtazamo wangu hii ndiyo hofu ya viongozi,” amesema.
Katika mazingira hayo, amesema viongozi nchini hawana uhakika kwamba wakitoa mwanya wa maadhimisho hayo, utaishia kwenye kuadhimisha siku hiyo pekee.
Kwa mtazamo wa mhadhiri huyo, siasa hubadilika kutokana na matukio ya wakati husika na kuzuiwa kwa shughuli hiyo ya Bavicha kunaakisi hilo.
“Wakati Chadema wanaruhusiwa kufanya maandamano nchi nzima dunia ilikuwa imetulia, hata siasa hazikuwa na mambo mengi. Lakini sasa kuna matukio mengi yameshuhudiwa yakisababisha mabadiliko na mitikisiko kwa watawala ndiyo maana kuna hofu,” ameeleza.
Hoja inayofanana na Dk Masabo, ilitolewa pia na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Mohamed Bakari aliyesema kuna hofu ya watawala kuepuka yaliyotokea katika mataifa kadhaa duniani.
Amesema matukio katika mataifa kama Kenya na Nigeria yanatumiwa kama rejea na funzo kwa viongozi wa mataifa mengine, ikiwemo Tanzania juu ya umuhimu wa kudhibiti matukio kama hayo mapema.
“Katika nyakati hizi ambapo kuna kumbukumbu ya matukio hatari ya kisiasa yaliyosababishwa na vijana, mtawala huwa na hofu ya kuruhusu uhuru wa shughuli hizo kama ilivyokuwa katika maandamano,” ameeleza.
Kilichotokea Kenya, Bangladesh
Wanachokieleza wanazuoni hao ni maandamano ya vijana waliozaliwa kuanzia mwaka 2000 ‘Generation Z’, yalianzia nchini Kenya Juni 2024, walipoandamana kupinga muswada wa sheria ya fedha, hadi Rais William Ruto akakataa kuusaini.
Licha ya Rais Ruto kuacha kuusaini muswada huo na hatimaye kurudishwa tena bungeni kwa marekebisho, maandamano yaliendelea yakishinikiza kumuondoa madarakani.
Vuguvugu hilo, lilisababisha Rais Ruto alivunje baraza lake la mawaziri na baadaye kuwateua wapya.
Mamia ya watu waliripotiwa kupoteza maisha katika maandamano hayo, huku uharibifu mkubwa wa miundombinu na rasilimali ukishuhudiwa.
Kilichotokea Kenya kiliwaambukiza vijana wa Uganda walioanzisha vuguvugu kama hilo, lakini walidhibitiwa mapema na Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museven aliyepiga marufuku, akisema: “Anayeandamana anataka kucheza na moto.”
Vikosi vya ulinzi na usalama vilitumwa barabarani kudhibiti vijana waliothubutu kuandamana.
Hali kama hiyo ilijitokeza nchini Bangladesh na kusababisha Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Sheikhat Hasina ajiuzulu baada ya maandamano ya vijana katika ikulu ya taifa hilo.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umetoa tamko la kulaani kukamatwa kwa viongozi, wanachama wa Chadema, wanahabari na mawakili, ikisema ni kunavunja Katiba.
Katika tamko lake, THRDC imenukuu Ibara ya 18 na 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa haki na uhuru wa watu kujumuika, kufanya mikutano, maadhimisho na kueleza mawazo yao.
“Haki hizi hazipo kwenye Katiba peke yake bali zipo kwenye mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia,” imeeleza katika sehemu ya tamko hilo.
Ilieleza ukamatwaji huo unafifisha uhalisia wa maridhiano, ustahimilivu na mabadiliko ambayo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akihubiri tangu alipoingia madarakani.
“Tunatoa wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuwaachilia huru watu wote waliokamatwa bila masharti, ili kuadhimisha siku ya vijana duniani kama ambavyo vyama vingine tayari vimekwishaadhimisha na hatukuona wakikamatwa,” imeeleza taarifa hiyo.
Kama ilivyokuwa kwa THRDC, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nacho kililaani ukamataji huo, kikitaja Ibara ya 20 ya Katiba ya nchi kinachootoa uhuru na haki ya kukusanyika.
Taarifa hiyo pia, imeonyesha kinachoendelea kinapingana na kauli za wakati wote za Rais Samia kuwa, anatekeleza R4 katika utendaji wake.
“Hatua ya Polisi kuingilia shughuli halali ya kisiasa inakwenda kinyume na falsafa ya R4 ya Rais Samia zinazolenga kuleta ustahimilivu, kujadiliana, kuvumiliana na kujenga upya,” imeeleza taarifa hiyo.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amelaani kitendo cha viongozi hao wa Chadema na wanachama wao kukamatwa na kulitaka Jeshi la Polisi kuwaachia huru.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Dorothy, imesema wanapinga kitendo hicho kwa kuwa kinakiuka Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa watu kukusanyika.
“Tumesikitishwa kuona hila zinazofanywa na Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa vya kuwakamata viongozi wakuu wa chama hicho, kuzuia zaidi ya vijana 150 wakiwa njiani kuelekea Mbeya na polisi kuzingira Uwanja Ruanda Nzovwe,” imesema.
Dorothy amesema vitendo hivyo vinafufua hofu ya kurejeshwa kwa kasi mazingira kandamizi kwa vyama vya siasa vya upinzani kufanya shughuli zao kwa uhuru.
“ACT Wazalendo tunachukulia hila hizi zinazofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya viongozi wa Chadema, ni tishio kwa vyama vyote makini vya upinzani na demokrasia ya vyama vingi nchini,” amesema.
Amesema tukio hilo na mengine yanayofanywa na dola yanakinzana na falsafa za R4 (Ustahimilivu, Maridhiano, Mabadiliko na Kujenga taifa jipya) za Rais Samia Suluhu Hassan.
“Vitendo hivi vinaonyesha hatua chache za kuimarisha uhuru wa kujumuika, kukusanyika na kujieleza vipo shakani. Tunalitaka Jeshi la Polisi liwaachie huru viongozi wote vya Chadema wanaowashikilia bila masharti yoyote,” amesema.
Jeshi la Polisi limefanikiwa kudhibiti maadhimisho hayo ya vijana, huku ikiimarisha ulinzi na kufanya doria katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Leo mapema Mwananchi lilipita maeneo mbalimbali na kushuhudia ulinzi ulivyoimarishwa katika baadhi ya maeneo, ikiwa Uyole, Ruanda Nzovwe na Ofisi za Chadema Kanda mtaa wa Kadege na kituo kikuu cha polisi Mbeya.
Pia baadhi ya magari ya polisi yakiwa na askari wake yalikuwa yakipita baadhi ya mitaa ya jijini Mbeya kuimarisha ulinzi, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Katika sehemu ya Uyol,e magari yaliyokuwa yakitokea mikoani yalisimamishwa kukaguliwa na haikufahamika wazi sababu za ukaguzi huo, huku baadhi ya watu wakihusisha na uingiaji wa makada wa Chadema.
Kwa upande wa viwanja vya Ruanda Nzovwe, polisi zaidi ya 20 wakiwa na bunduki na gari maalumu la maji ‘washawasha’ waliweka ulinzi, huku wananchi waliofika asubuhi wakiondoka wenyewe kutokana mazingira waliyoyaona.
Wakati Chadema ikikabiliwa na hayo, Chama cha ACT Wazalendo nacho kimekwaa kisiki katika mpango wake wa kufanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Charambe leo Agosti 12, 2024 kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani.
Chama hicho kimekwaa kisiki baada ya Kituo cha Polisi Wilaya ya Mbagala kutoa taarifa ya kuzuia mikutano ya hadhara na ile ya ndani.
Jeshi hilo lilikuwa linajibu barua iliyowasilishwa na chama hicho, likisema: “Pamoja na barua hii napenda kukujulisha kuwa mikutano yote ya hadhara na ya ndani imezuiliwa hadi hapo yatakapotolewa maelezo mengine.”
Hata hivyo, baadaye Jeshi la Polisi, Makao Makuu kupitia taarifa yake iliyotolewa na msemaji wa jeshi hilo, David Misime ilijitenga na taarifa ya Kituo cha Polisi Wilaya ya Mbagala.
“Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa kuwa halijapiga marufuku kufanyika mikutano ya nje ya hadhara na ile ya ndani, ilimradi inafuata matakwa ya sheria ya nchi,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Misime, walichopiga marufuku ni mkusanyiko ulioitishwa na viongozi wa Chadema, huko jijini Mbeya kwa kivuli cha kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani.
Imeandikwa na Juma Issihaka, Victoria Michael, Tuzo Mapunda (Dar).
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.
Nyongeza naVictoria Michael