Dar es Salaam. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, imeajiri watumishi wa afya 120 wa kada mbalimbali kwa mapato ya ndani, kutokana na uhaba wa watumishi unaoikabili hospitali hiyo.
Hospitali hiyo ina idara 13 zenye jumla ya watumishi 467, wakiwemo madaktari bingwa 26 ambapo wana kada za kibingwa 12, wauguzi 228 na watumishi wengine 214.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 12, 2024 na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Joseph Kimaro wakati wa uzinduzi wa huduma ya usafishaji damu kwa wagonjwa sugu wa figo ‘dialysis’ katika hospitali hiyo.
Amesema ili kukabiliana na upungufu wa watumishi, wameajiri 120 wa mkataba.
“Ili kukabiliana na upungufu wa watumishi wakati wa utoaji wa huduma, tumeajiri watumishi 120 kupitia mapato ya ndani yanayotokana na malipo ya huduma kwa wagonjwa wanaokuja hospitalini hapa,”amesema Dk Kimaro.
Amesema watumishi waliowaajiri kwa mkataba ni madaktari, wauguzi, wataalamu wa maabara, wataalamu wa mionzi pamoja na wataalamu wa mifumo ya kompyuta (ICT).
Pia, amesema katika kuongeza hali na motisha ya utoaji huduma, wameweka mbele maslahi ya watumishi na katika uboreshaji huo mwaka 2024/25 jumla ya watumishi 175 wamepandishwa madaraja na wengine wamebadilishwa kada.
Akielezea huduma ya usafishaji damu, Dk Kimaro amesema mwaka 2023/24 hospitali hiyo ilitoa huduma kwa wagonjwa 11,175 ambao walikuwa na magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema kati ya wagonjwa hao, 412 walipatikana na magonjwa ya figo na kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kati yao walipoteza wagonjwa 74.
“Wagonjwa hao 412 walikuwa wanahitaji huduma ya usafishaji wa damu, japokuwa tuliona hili ni changamoto, lakini iwe ni fursa ya sisi Temeke kuweza kuanzisha huduma hizi hapa ili kusaidia wananchi wa Temeke, Kigamboni na Mkuranga,” amesema Dk Kimaro.
Kutokana na ongezeko la takwimu za matatizo ya figo, amesema menejimenti imenunua mashine 10 zenye thamani ya Sh412 milioni kwa kutumia mapato ya ndani.
Pia katika kuboresha huduma hiyo, tayari wameshapanga mwaka wa fedha 2024/25 kumsomesha daktari mmoja bingwa bobezi wa magonjwa ya figo katika Chuo Kikuu Shirikishi cha Afya Muhimbili (Muhas).
Akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema kuwepo kwa huduma ya usafishaji wa damu katika Hospitali ya Temeke itasaidia kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuwapunguzia umbali wa huduma wananchi wa Temeke na maeneo ya jirani.
“Mkakati wa wizara ni kuziwezesha hospitali zote za rufaa za mikoa kutoa huduma za kusafisha damu, ili kuwasogezea wananchi huduma hii kwa karibu zaidi,” amesema.
Amesema mwaka 2022/23 hospitali hiyo ilihudumia wagonjwa 9,566 wenye magonjwa yasiyoambukiza. Wagonjwa 396 walipewa rufaa ya kwenda Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya figo, ikilinganishwa na mwaka 2023/24 ambapo walihudumia wagonjwa 11,175 na wagonjwa 412 walipewa rufaa ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.2.
“Nasisitiza kwa watoaji wa huduma za afya kutoa elimu kwa jamii, ili kujiepusha na viashiria vya hatari vinavyosababisha magonjwa yasiyoambukiza, hivyo kupunguza kasi ya magonjwa hayo katika jamii yetu,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam (TPA), Abed Gallus amesema kupitia sera yao ya kutoa msaada kwa jamii, wametoa viti mwendo 20, kukarabati jengo la usafishaji damu kwa gharama ya Sh251.26 milioni, vitimwendo 20, vifaa vya kupokelea watoto 10 vyenye thamani ya Sh10 milioni.