Sengerema. Bahati Kanfumu, mkazi wa Kijiji cha Kabusuli, Kata ya Nyamatongo, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza ameeleza jinsi alivyonusurika kushambuliwa na kundi la fisi.
Akizungumza jana Agosti 11, 2024, amesema wakati akielekea kutafuta mahitaji ya familia asubuhi, alikutana na kundi hilo la fisi linalosadikika kuwaua watu wawili.
Amesema alilazimika kushuka kutoka kwenye baiskeli aliyokuwa akiendesha na kuitumia kama kinga, ili fisi hao wasimdhuru.
Amesema alijaribu kuwatishia kwa kutumia baiskeli yake, huku akipiga kelele kuomba msaada na alizungushana na fisi hao kwa takriban saa tatu, huku baadhi waliondoka baada ya kuchoka na mwishowe alibaki akipambana na fisi mmoja aliyekuwa akimzonga.
Hata hivyo, amesema baada ya muda fisi huyo naye alichoka na ndipo alipopata upenyo wa kuondoka eneo hilo akiwa salama.
“Nilitumia baiskeli yangu kuwatishia, ili waondoke huku nikipiga kelele nikiomba msaada. Walikuwa wanauma tairi la baiskeli, tulizungushana nao eneo hilo kwa saa tatu hadi fisi hao walichoka na kuondoka,”amesema.
Bahati ameiomba Serikali kupiga kambi katika Kijiji cha Kabusuli, Kata ya Nyamatongo, ili kuwawinda wanyama hao ambao wanahatarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Matukio ya fisi kuvamia na kuua watu yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika kata mbalimbali za Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza. Kata ambazo zimeshamiri kwa matukio hayo ni Chifunfu, Kasenyi, Katunguru, Busisi, Bitoto, Buyagu na Tabaruka.
Katika tukio la usiku wa kuamkia Agosti 11, 2024, watu wawili wameuawa baada ya kushambuliwa na fisi katika Kijiji cha Kabusuli, Kata ya Nyamatongo walipokuwa wakielekea Kijiji cha Kalumo kwa kutumia pikipiki.
Waliouawa ni Yohana Andrea, mkazi wa Kijiji cha Nyamatongo, Kitongoji cha Lwabi na David Thobias, mkazi wa Kijiji cha Kalumo, Kata ya Nyamatongo. Tukio hili lilishtua wengi na kuzua hisia tofauti miongoni mwa wananchi wa kijiji hicho.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kabusuli, Alfred Kombo amesema wameitisha mkutano wa wananchi wa kitongoji hicho kujadili jinsi ya kukabiliana na kudhibiti wanyama hao wanaovamia na kuwadhuru watu.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga, amesema Serikali itashirikiana na wananchi kuhakikisha wanyama hao wanauliwa.
Ameeleza kuwa katika kata ambazo matukio kama hayo yalitokea awali, Serikali ilishirikiana na wananchi na kufanikiwa kuwaua wanyama hao katika Kata ya Chifunfu na Kasenyi na sasa wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa amani.
“Tutafanya hivyo tena kwa tukishirikiana na wananchi, ili tudhibiti hali hii ambayo imekuwa tishio,” amesema Ngaga.
Maziko ya Yohana Andrea na Devid Thobias, waliopoteza maisha kwa kushambuliwa na fisi, yalifanyika jana Agosti 11, katika maeneo mawili tofauti. Yohana Andrea alizikwa nyumbani kwao Kitongoji cha Lwabi, Kijiji cha Nyamatongo na David Thobias alizikwa nyumbani kwao Kijiji cha Kalumo, Kata ya Nyamatongo, wilayani Sengerema.
Katika maziko hayo, Diwani wa Nyamatongo, Yanga Makaga, alitoa msaada wa mchele kilo 100 na jeneza moja, huku Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabsamu akitoa rambirambi ya jeneza moja, mchele kilo 200 na mafuta lita 20 kwa familia hizo.
Kwa upande wa Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga, aliwasilisha rambirambi na kuahidi kuwasiliana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) kufika eneo la tukio na kuwasaka fisi hao ambao wamekuwa tishio.