Kauli ya Samia kuhusu fidia ya ardhi yaibua wadau, Serikali yafafanua

Dar es Salaam. Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwataka wananchi wanaoidai Serikali fidia baada ya kupitiwa na miradi kusubiri mpaka itakapokamilika, imewaibua mawakili na watetezi wa haki za binadamu wakisema kauli hiyo ni kinyume cha sheria na Katiba ya nchi.

Wamesema suala la fidia lipo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali haiwezi kuchukua eneo la mtu bila kutoa fidia, wakisisitiza fidia inapaswa kutolewa ndipo wananchi wapishe mradi.

Kwa mujibu wa mawakili hao, Ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaeleza kila mtu ana haki ya kumiliki mali na kwamba mtu huyo ana haki ya kulindiwa mali yake kwa mujibu wa sheria.

Sehemu ya pili ya Ibara hiyo, inaeleza pale ambapo mali ya mtu inalazimika kutwaliwa na Serikali kwa matumizi yenye maslahi kwa umma, sharti mmiliki wa mali hiyo alipwe fidia stahiki.

Tofauti na Katiba, wamesema kifungu Na.11 (i) cha sheria ya utwaaji ardhi kinaelekeza pale ardhi inapotwaliwa, Serikali inawajibika kulipa fidia.

Aidha, Kifungu Na. 3(1) (g) cha Sheria ya Ardhi (Sura 113) kinaelekeza fidia hiyo ni lazima iwe kamilifu, ya haki na ilipwe kwa wakati.

Akifafanua kauli ya Rais Samia, Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) juzi, amesema kumekuwa na upotoshaji wa kauli ya kiongozi mkuu huyo wa nchi.

“Rais Samia ni muumini wa utawala wa sheria kama ambavyo amekuwa akisisitiza, tunapenda kusisitiza kulingana na Katiba yetu iliyotoa haki ya kumiliki mali, ikiwemo ardhi kwa wananchi wote pale ambapo miradi mikubwa ya maendeleo inapotaka kufanyika, wananchi watakaopisha miradi hiyo ni haki yao kikatiba na kuzingatia sheria zote kulipwa,” amesema.

Makoba amesema alichowataka Rais wananchi ni kuwa wazalendo na wenye subira, wakati Serikali ikishughulikia stahiki zao na fidia.

Amesema kulingana na kauli ya Rais Samia, hakuna mwananchi atakayepisha mradi wa maendeleo asilipwe fidia yake, huku akisisitiza watu kuepuka upotoshaji wa kauli za viongozi.

Agosti 5, 2024 Rais Samia alipohutubia wananchi wa Wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya ziara yake ya siku sita mkoani humo, aliwataka wananchi wanaoidai Serikali fidia baada ya kupitiwa na miradi, wasubiri miradi hiyo ikamilike kwanza, kisha utaratibu utafanyika kuhakikisha wanalipwa.

Uamuzi huo ni kutokana na kile alichoeleza ni umuhimu wa miradi hiyo kwa wananchi, hivyo Serikali inaona ianze kuitekeleza kwanza kwa manufaa ya wengi, ndipo ichakate utaratibu wa fidia.

Mkuu huyo wa nchi aliibua hoja hiyo baada ya malalamiko ya wananchi wa wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro kudai malipo ya fidia, baada ya kupitiwa na mradi wa umeme wa Kihansi.

“Kwa hiyo kwa wale wanaotudai fidia zao kwa maendeleo yao wenyewe tunaomba muwe na subira. Tuacheni tumalize miradi ya maendeleo wananchi wengi wafaidike, halafu tutaangalia masuala ya fidia,” amesema.

Katika maelezo yake amegusia uwepo wa baadhi ya watu wanaoweka vikwazo vya utekelezwaji wa miradi husika kwa sababu hawajalipwa fidia.

“Tuacheni tufanye miradi, mambo ya fidia mimi nawahakikishieni hatonyimwa mtu haki yake.

“Tukiwa tayari tutalipa fidia, kwa hiyo niwaombe sana wananchi achieni miradi ijengwe kwa manufaa yenu, fidia itakuja kulipwa,” amesema.

Kutokana na kauli hiyo ya Rais Samia, wakili Sigrada Mligo kutoka Njombe kupitia mtandao wa X, amesema fidia ipo kwa mujibu wa Katiba na Serikali haiwezi kuchukua eneo la mtu bila kutoa fidia, hivyo inapaswa kutolewa ndipo wananchi wahame.

“Rais anasema miradi ipite kwanza, ifanyike kwanza ndipo wananchi walipwe fidia, hata sheria inayoruhusu mtu kuchukua ardhi kwa lazima imeeleza wazi ni lazima mtu apewe kwanza fidia, ndipo ahame akatafute makazi mengine,” amesema.

Amesema maeneo mengi ambayo wamepisha miradi bila kulipwa wanahangaikia fidia kwa muda mrefu na wanapokwenda kudai halmashauri hupigwa kalenda.

Kwa kauli hiyo ya Rais Samia, wakili huyo amesema ni ukiukwaji wa sheria na hata miradi inayotekelezwa si hisani, bali ni haki ya wananchi na hata fidia ni haki ya wananchi kwa sababu ipo kwa mujibu wa sheria.

Hoja hiyo inaungwa mkono na rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi akisema ulipaji wa fidia ni suala la kikatiba na kisheria.

“Fidia ilipwe ndani ya kipindi cha miezi sita. Lengo ni kuhakikisha maendeleo ya vitu hayaathiri maendeleo ya watu. Usipoidai fidia yako kwa wakati, sheria itakunyima haki yako ya kudai nje ya wakati na hutakuwa na la kufanya,” amesema.

Wakili Mwabukusi amesema kabla ya eneo la mtu kutwaliwa na Serikali, linapaswa kufanyiwa tathmini na alipwe fidia na baadaye apewe muda wa kuondoka kwenye eneo hilo na si kuondolewa bila kulipwa fidia.

Hoja hiyo ya kisheria inafafanuliwa pia na wakili Edson Kilatu anayesema kauli ya Rais Samia haipo kisheria.

“Kama wananchi kwa hiari yao wamekubali kupisha mradi bila kudai fidia sio dhambi, lakini utaratibu wa kisheria unaeleza ulipaji wa fidia unapaswa kuwa wa namna gani, watu walipwe ndipo waondoke,” ameeleza wakili Kilatu.

Naye mkurugenzi mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijobi Simba amesema kilichotamkwa na Rais Samia hakipo sawa.

“Rais amekosea, wananchi walipwe fidia ndipo waondoke, sheria ndivyo inavyoelekeza na si vinginevyo,” amesema.

Mwanaharakati wa haki za binadamu kupitia mitandao ya kijamii, Martin Masese kupitia ukurasa wake wa X aliandika, “fidia inapaswa kulipwa kwa mujibu wa sheria siyo kwa huruma ya Rais.”

“Kifungu Na.11 (i) Sheria ya utwaaji inaelekeza pale ardhi inapotwaliwa serikali inawajibika kulipa fidia, watu walipwe fidia, wakaendeleze makazi mapya, Serikali iendelee na ujenzi wa miradi. Kuwataka wananchi waondoke maeneo yao bila kuwalipa fidia ni ukoloni,” ameandika.

Akichangia hoja hiyo, aliyewahi kuwa rais wa TLS, Dk Rugemeleza Nshala amesema haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa.

Amesema Serikali haijui watu wake wataishi kwa miaka mingapi, hivyo kuwaondoa kwenye makazi yao na kuwaahidi kuwalipa fidia baadaye si sahihi.

Related Posts