Mawakili kesi ya Kombo wa Chadema watakavyochuana leo

Dar es Salaam. Kesi ya mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, aliyepotea kwa mwezi mzima, baadaye kupandishwa kizimbani, Kombo Mbwana inatarajiwa kusikilizwa kuhusiana na hatima ya dhamana yake.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa leo Jumatatu, Agosti 12, 2024 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanga, Moses Maroa kuhusiana na zuio la dhamana yake, lililowekwa na Polisi Mkoa wa Tanga.

Kombo alitarajiwa kupewa dhamana Julai 30, 2024 kama angetimiza masharti aliyopewa na Mahakama hiyo, lakini iliyeyuka baada ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa RCO) wa Tanga kuwasilisha mahakamani kiapo cha kuzuia dhamana hiyo.

Siku hiyo kesi ilipoitwa kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi ulikuwa umekamilika na kama mshtakiwa alikuwa ametimiza masharti ya dhamana yaliyokuwa yametolewa na Mahakama, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa RCO amewasilisha kiapo akiomba mshtakiwa asipewe dhamana.

RCO aliwasilisha kiapo hicho akiiomba Mahakama hiyo isimpatie dhamana mshtakiwa huyo, kwa maelezo bado wanaendelea na upelelezi na kwamba wanatarajia kuwaongeza washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wapo maneo mbalimbali nchini.

Mawakili wa mshtakiwa huyo waliokuwepo siku hiyo, Deogratius Mahinyila na Michael Rugina walipinga kuwepo kwa kiapo hicho kuwa kipo kinyume na utaratibu wa kisheria na kwamba RCO hana mamlaka hayo ya kuzuia dhamana, tena Mahakama ikiwa imeshatoa uamuzi wa masharti ya dhamana.

Hivyo, waliiomba Mahakama isizingatie na kuendelea na amri yake iliyokuwa imeshaitoa ya masharti ya dhamana na hatimaye impe dhamana, kwani walikuwa wamejiandaa kutekeleza masharti ya dhamana.

Hata hivyo, Hakimu Maroa aliamua kutengua amri ya masharti ya dhamana na kuahirisha kesi mpaka leo Jumatatu kwa ajili ya usikilizwaji wa kiapo hicho cha RCO.

Pia Hakimu Maroa aliutaka upande wa utetezi kuwasilisha kiapo kinzani kujibu kiapo hicho cha RCO kabla ya leo, yaani tarehe iliyopangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa zuio hilo.

Hivyo, leo hii Mahakama hiyo itasikiliza hoja za pande zote kuhusiana na sababu za zuio hilo la RCO.

Kulingana na msimamo wa mawakili wa utetezi, kama walivyoubainisha siku hiyo baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama kuwepo kwa kiapo hicho, ni dhahiri kutakuwa na mchuano mkali wa hoja za kisheria baina ya mawakili wa pande zote mbili wakati wa usikilizwaji.

Kwa mantiki hiyo, hoja kubwa zitajikita katika uhalali wa kiapo cha RCO, yaani kustahili ama kutokustahili kwake kuwepo mahakamani pamoja na uzito wa sababu za RCO kuomba mshtakiwa asipewe dhamana.

Mpaka saa 5:30 asubuhi kesi hiyo ilikuwa bado haijaitwa na ndugu wa mshtakiwa, wakiwemo wazazi wake walishafika mahakamani kusubiri usikilizwaji wa kei hiyo ili kujua hatima yake.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 19759/2024, Kombo anakabiliwa na mashtaka matatu chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Katika shtaka la kwanza anadaiwa kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume na kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta. Anadaiwa Julai 9, 2024, katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi uliopo Wilaya na Mkoa wa Tanga alikutwa akimiliki laini (kadi ya simu) ya Tigo yenye namba (ICCID) 8925502042093621824, iliyosajiliwa kwa jina la Shukru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umiliki wa laini hiyo.

Pia, anadaiwa kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, na kushindwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya laini ya simu.

Kombo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 16, 2024, na kusomewa mashtaka hayo, ambayo hata hivyo aliyakana.

Mahakama ilisema dhamana yake ilikuwa wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja, wenye barua ya mtendaji wa mtaa wanakokaa pamoja na vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Hata hivyo, alipelekwa mahabusu kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, baada ya kukosa wadhamini kwa kuwa ndugu zake hawakuwa na taarifa wakati anapandishwa kizimbani.

Kabla ya kufikishwa mahakamani, Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Kijiji cha Kwamsala, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga na kupelekwa mahali ambako hata ndugu zake hawakupafahamu.

Julai 14, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zakaria Bernard alitangaza kuwa anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma hizo na Julai 16 akapandisahwa kizimbani.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts