Mbowe, Pambalu wadaiwa kukamatwa Mbeya, Polisi, Chadema ngoma nzito

Mbeya/Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linadaiwa kumkamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Vijana wa chama hicho (Bavicha), John Pambalu.

Viongozi hao waliokuwa wanatoka jijini Dar es Salaam kwenda Mbeya wanadaiwa kukamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Songwe leo Jumatatu, Agosti 12, 2024.

Mbowe alikuwa anakwenda kufuatilia viongozi na wanachama wa chama hicho wanaodaiwa kukamatwa na Polisi kutokana na madai ya kukiuka zuio la kutokufanyika kwa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Bavicha walikuwa wanaratibu kongamano hilo ambalo lilikuwa lifanyike leo Jumatatu, Agosti 12, 2024 katika Viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.

Saa 5:45 asubuhi, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema katika akaunti yake ya X (zamani Twitter) ameandika: “Mwenyekiti wa Chama Taifa Freeman Mbowe na John Pambalu walipofika uwanja wa ndege Songwe leo tarehe 12/08/2024 wamekamatwa na Jeshi la Polisi.

Ukamataji huu umeongozwa na RPC wa Mbeya. Tutaendelea kuwapa taarifa kadiri tunavyozipata,” amedai Mrema.


Mbowe atia mguu madai kina Lissu kukamatwa Mbeya

Awali, saa 4:37 asubuhi, Mrema katika akaunti hiyo hiyo aliandika: “Mwenyekiti wa Chama Taifa Mheshimiwa Freeman Mbowe yuko njiani kuelekea Mbeya, kwa ajili ya kukutana na viongozi wa Jeshi la Polisi Mbeya ili kufuatilia; hatima ya viongozi waliokamatwa na kujua walipo na hali zao kiafya. Tutawapa taarifa zaidi akifika uwanja wa ndege Mbeya.”

Hata hivyo, jitihada za Mwananchi kuzungumza na uongozi wa Polisi Mkoa wa Mbeya kuhusu madai ya tukio hili, hazijaweza kuzaa matunda licha ya Kamanda wa Polisi kutafutwa mara kadhaa bila mafanikio. 

Viongozi ambao wanadaiwa kukamatwa usiku wa jana Jumapili, Agosti 11, 2024 wakiwa Ofisi za Kanda ya Nyasa za Chadema ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu.

Mbali na viongozi hao ambao ni wajumbe wa kamati kuu, kuna viongozi wa Bavicha na wanachama wanaodaiwa kukamatwa na wako kwenye mahabusu mbalimbali za polisi jijini Mbeya.

Tangu usiku wa jana Jumapili, Mwananchi limekuwa likimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga kuzungumzia kinachoendelea bila mafaniko kwani alisema anafuatilia.


TAZAMA KAULI YA TUNDU LISSU JANA USIKU BAADA YA KUZINGIRWA NA POLISI MBEYA

“Ndiyo maana nimekuambia kwa sasa hivi kuna kazi nyingine naifanya, mpaka nizungumze na RCO, nitajua kuhusu jambo hilo,” amesema Kuzaga alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Lissu, Mnyika na Sugu.

Hata hivyo, saa 5.52 asubuhi leo Agosti 12, 2024 Mwananchi ilimtafuta tena Kamanda Kuzaga kuhusu kukamatwa kwa Mbowe na Pambalu simu yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alisema RPC yupo kikaoni.

Pia, saa 6.14 mchana Mwananchi katika kutaka kufahamu ukweli wa kukamatwa kwa Mbowe ilimpigia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, naye hakupokea simu.

Saa 6.18 mchana Mwananchi ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime ambaye alituma meseji ya kuomba atumiwe ujumbe ufupi na baada ya kumuuliza kuhusu kukamatwa kwa viongozi hao wa Chadema hakujibu tena.

Baada ya jitihada hizo Mwananchi saa 6.40 mchana ilimtafuta Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Cammilius Wambura kwa njia ya simu, lakini pia hakupokea.

Kilichosababisha shughuli hiyo iingiliwe kati na Jeshi la Polisi ni kauli inayodaiwa kutolewa na Bavicha iliyohusisha mfano wa kilichofanywa na vijana wa nchini Kenya, ikiwasifu wamejitambua, jambo lililotajwa kama dalili ya vurugu.

Kabla ya Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi hao, lilipiga marufuku kufanyika kwa shughuli hiyo, ikisisitiza kuna viashiria vya uvunjifu wa amani na vurugu ndani yake.

Polisi ilitangaza uamuzi huo, ukitanguliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika Agosti 8, 2024 kumtaka kusitisha shughuli yoyote iliyopangwa ufanyia leo Jumatatu, Agosti 12, 2024 kwa kile alichodai lugha za viongozi wa Bavicha zinaashiria uvunjifu wa amani.

HALI ILIVYO MUDA HUU UWANJA WA RUANDA NZOVWE SAKATA LA VIJANA WA CHADEMA

Barua hiyo ambayo nakala ilitumwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), iliwataka viongozi wa Chadema, akiwemo Mbowe, Mnyika na Pambalu kufika ofisi ya Msajili jijini Dar es Salaam, kesho Jumanne, Agosti 13, 2024 saa 5:00 asubuhi.

Related Posts