Mwinyi Zahera ataka mechi 3 Namungo

KOCHA Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera amesema timu yake ipo tayari kwa asilimia 80, atatumia mechi tatu za kwanza za Ligi Kuu Bara kutengeneza kikosi cha kwanza.

Namungo wamecheza mechi tatu za kirafiki wakishinda mbili na kufungwa moja, walianza na Singida Black Stars walishinda mabao 2-0, walifungwa na Dodoma Jiji 3-0 na walishinda dhidi ya ACA Eagle 2-1.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema hawezi kufurahishwa na matokeo ya mechi za kirafiki na kuamini timu yake ipo tayari hivyo asilimia 20 zilizobaki atatumia kwenye mechi za mwanzo za ligi kuunda kikosi chake cha kwanza.

“Mechi za kirafiki wachezaji wanatumia nguvu nyingi na sio akili mchezaji anatoka kukimbia asubuhi na jioni anacheza mechi hakiwezi kuwa kipimo sahihi nimeshindwa kupata kikosi cha kwanza huku lakini naamini mechi tatu za mwanzo zitanipa mwanga,” alisema na kuongeza;

“Pia sikuanza mazoezi na wachezaji wote kuna wengine walichelewa kujiunga na kambi, alafu ili kupata kikosi lazima ucheze mechi kuanzia sita na ndio maana nimesema mechi tatu za mwanzo za ligi zitanipa kikosi.’’

Zahera alisema licha ya kukosa kikosi cha kwanza bado anaamini anawachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu ambao watampa matokeo mazuri na kumpa changamoto ya kupata kikosi cha kwanza kutokana na kila mmoja kuonyesha na kuwania nafasi kikosi cha kwanza.

“Kupata kikosi sio kuchagua tu wachezaji bila kuzingatia ubora na sasa timu yangu ina wachezaji wengi bora hivto sio rahisi kuwajenga kwa mechi tatu za kirafiki naamini mara baada ya mechi tatu za ushindani nitakuwa na mwanzo mzuri na bora wa kupata wachezaji wa kikosi cha kwanza.”

Namungo inaanza na Singida Black Stars mechi yake ya kwanza ya ligi inayotarajia kuchezwa Agosti 17 na Agosti 25 watakuwa nyumbani tena dhidi ya Tabora Uniten na Septemba 12 wataenda ugenini dhidi ya Dodoma Jiji.

Related Posts