Ndugu wa Kombo wa Chadema, wanahabari wazuiwa kuingia mahakamani

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Tanga inaendelea na usikilizwaji wa kesi ya mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, aliyepotea kwa mwezi mzima, Kombo Mbwana baadaye kupandishwa kizimbani na Jeshi la Polisi Tanga.

Hata hivyo, ndugu wengine wa Kombo waliofika mahakamani hapa kufuatilia mwenendo wa shauri hilo pamoja na wanahabari wamezuiliwa na polisi kuingia katika chumba ambacho kesi hiyo inasikilizwa.

Kombo anakabiliwa na kesi ya jinai, ameshtakiwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA – Electronic and Post Communications Act), kuhusiana na kutotoa taarifa za usajili wa kadi yake ya simu ya mkononi.

Kesi hiyo inasikilizwa leo Jumatatu, Agosti 12, 2024 mchana huu na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Moses Maroa kuhusu zuio la dhamana yake lililowekwa na Polisi Mkoa wa Tanga.

Baada ya kesi hiyo kuitwa, askari Polisi aliwazuia ndugu wa Kombo waliotaka kuingia mahakamani kusikiliza kesi hiyo, huku akiwaita wazazi wa Kombo pekee kwa madai kuwa chumba ilimosikilizwa kesi hiyo ni kidogo.

Ndugu hao wa Kombo wamelalamikia hatua hiyo kuwa wanaonewa, huku wakihoji iweje chumba kiwe kidogo kwenye kesi ya Kombo, wakati kesi za washtakiwa wengine zilipoitwa waliingia wanafamilia pamoja na ndugu wengine.

Hata hivyo, wameishia kunung’unika tu na kulalamika na hatimaye wakatoka na kusubiri nje ya jengo hilo.

Wakati ndugu hao wa Kombo wakizuiliwa kuingia kwa madai kuwa chumba hicho ni kidogo, wanahabari wamezuiliwa kuingia na kuripoti kesi hiyo kwa madai hawatakiwi kabisa kuonekana kwenye kesi hiyo.

Baada ya ndugu wa Kombo kutoka nje, Mwananchi limejitambulisha kwa askari huyo ili kuruhusiwa kuingia ndani kusikiliza na kuripoti mwenendo wa kesi hiyo, ndipo askari huyo akang’aka na kusema Mahakama hiyo imepiga marufuku waandishi wa habari kwenye kesi hiyo.

“Enhee, tena ninyi (waandishi wa habari) ndio hamtakiwi kabisa kwenye kesi hii, hiyo ni amri ya Mahakama,” amesema polisi huyo.

Hata hivyo, askari huyo hakueleza sababu ya wanahabari kutotakiwa kwenye kesi hiyo.

Mpaka saa 9:15 alasiri kesi hiyo ilikuwa inaendelea kusikilizwa ndani na haijulikani kinachobishaniwa.

Related Posts