PUMZI YA MOTO: Bodi ya Ligi haitaki watu wafurahi?

TANZANIA ni ya 131 duniani kwenye korodha ya nchi zenye furaha, kati ya nchi 143 zilizopo duniani.

Kwa tafsiri rahisi, Tanzania ni ya 12 duniani kwa nchi zisizo na furaha…hatari sana!

Na hii ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2024 ya taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mtandao wa Suluhisho la Maendeleo Endelevu (The UN Sustainable Development Solutions Network).

Umoja wa Mataifa unasema Tanzania haina furaha, Watanzania hawana furaha.

Umoja wa Mataifa unasema Watanzania wana makasiriko.

Mbaya zaidi, Tanzania inazidiwa hadi na Palestina (103), nchi iliyoko vitani ambako watu wake wanakufa kila siku, kama kuku wa mdondo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyofanyiwa utafiti na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza, Tanzania inashika nafasi ya 30 barani Afrika, ikizidiwa na nchi kama Nigeria ambayo ni 14 Afrika na ya 109 duniani.

Gambia, kanchi kadogo kaliko kandokando ya mto Gambia, ambako ni sawa na watu wa Rufiji tu, eti kametuzidi kakiwa nafasi ya 17 Afrika na ya 112 duniani.

Yaani hata nchi kama Chad ambayo ina matatizo kila kona, imetuzidi furaha, ikiwa ya 18 Afrika na ya 113 duniani.

Unaweza kujiuliza, wenzetu wanatoa wapi hiyo furaha licha ya matatizo waliyonayo kutuzidi sisi?

Lakini jibu la msingi hapa ni moja tu, watu wao wako huru kufurahi.

Watanzania hawana uhuru wa kufurahi, wanaminywa na mamlaka, tamaduni pamoja na mila na desturi.

Nitautumia mpira kuelezea hili kwa undani.

Hivi karibuni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Almasi Kasongo, amenukuliwa akisema kuanzia msimu mpya wa 2024/25, kutakuwa na adhabu kwa maofisa habari wanaochekesha.

Picha inaanza, Bodi ya Ligi haitaki watu wachekeshwe…haitaki watu wacheke…haitaki watu wawe na furaha.

Yaani Bodi ya Ligi imekaza fuvu kabisa kudhamiria kumuadhibu mtu kwa sababu ya kuchekesha?

Kwani Ofisa Habari akichekesha mashabiki wa timu yake, kuna sheria namba ngapi ya mpira itakuwa imevunjwa au kukiukwa?

Ofisa habari akichekesha mashabiki wa timu yake, ni kwa kiasi gani mpira utakuwa umeingizwa kwenye hali ya mtafaruku?

Katika hali kama hii utategemea Watanzania watakuwa na furaha? Ni lazima watajaa makasiriko moyoni hadi mwilini kwa ujumla.

Unakutana na mtu ana mambo mengi moyoni kayalimbikiza kwa muda mrefu na kwa kuyatolea hakupo.

Hivi Bodi ya Ligi haijui kwamba kucheka kunaongeza siku za kuishi?

Kuna hasada gani kwa mpira ofisa habari akiwachekesha mashabiki wa timu yake?

Hili jambo linaweza kuchukuliwa kiwepesi lakini ni kubwa sana.

Bahati mbaya watu wa mamlaka yoyote duniani huweka sheria halafu tafsiri yake hubaki nayo wao.

Kisha hutumia sheria hizi kuwahukumu wasiowataka.

Usishangae msimu ujao maofisa habari wasiotakiwa wakafungiwa kwa kosa la kusema kitu halafu watu wakacheka.

Au utakuta kwenye mkutano na waandishi wa habari au hata mahojiano tu ya kawaida, ofisa habari akaanza kwa kuwaomba wanaomsikiliza wasicheke maana asije akafungiwa.

Wakati Bodi ya Ligi inafikiria kuwafungia watu wanaochekesha, yenyewe inafanya madudu.

Ratiba ya Ligi Kuu wameitoa wiki moja kabla ya msimu kuanza…kituko!

Huu ni ugonjwa wao wa kila msimu, hasa tangu bodi hiyo iwe chini ya Kasongo.

Badala ya kutumia muda ilionao kutafuta majibu ya maswali magumu kama kuchelewa kutoka kwa ratiba ya ligi, bodi inatumia muda na raslimali zake kupambana na maofisa habari wanaowachekesha mashabiki wa timu zao.

Mapenzi ya mpira hujenga hisia kubwa sana kiasi kwamba timu inapopoteza mashabiki wake huwa kwenye wakati mgumu.

Anapotokea ofisa habari anayeweza kuwachekesha na wakacheka, anakuwa amewasaidia sana kurudisha furaha yao iliyopotea kwenye mpira.

Sasa ofisa habari kama huyu badala ya kutiwa moyo kwamba anafurahisha watu, eti anatungiwa sheria ya kudhibitiwa.

Mpira ni mchezo wa dakika 90 tu, baada ya hapo unahamia midomoni.

Na hakuna mdomo unaosikilizwa na wengi kama wa ofisa habari ya timu husika.

Na anapotokea aofisa habari anayeweza kuwafanya watu wakacheka, huyo atavutia wengi na kuwafanya waliwazike licha ya matokeo mabaya ya timu yao.

Hapo kwani kuna ubaya gani nyie wenzetu Bodi ya Ligi?

Wakati Jose Mourinho anaichukua Chelsea kwa mara ya kwanza mwaka 2004, timu hiyo ilikuwa inacheza mpira wa matokeo tu, bila kujali soka burudani.

Golikipa Petr Cech atapiga mpira mrefu mbele, Drogba ataruka na mabeki wa timu pinzani…mpira utaangukia kwa Lampard, anafunga.

Dakika 90 zinaisha na Chelsea wameshinda lakini watu hawajaburudika…sasa kazi ya kuburudisha watu ikawa ya Mourinho mwenyewe kwa kutumia mdomo wake.

Waandishi watamfuata, naye kama aliwapanga, atafanya mbwembwe zake pale…waandishi watacheka, mashabiki wa timu yake watacheka, na hata mashabiki wa timu pinzani watacheka…siku imeisha.

Kwenye mpira tunatafuta furaha, tunatafuta kucheka na kuchekana.

Sasa bodi ya ligi ikituzuia kucheka, inataka tunune tu!

Related Posts