‘Shule nyingi wanafunzi wanalishwa ugali maharage’

Dar es Salaam. Mhariri wa Afya wa Gazeti la Mwananchi, Herieth Makwetta amesema uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kati ya Februari mpaka Machi 2024, ulibaini wanafunzi katika shule nyingi wanalishwa ugali maharage kwa muda mrefu, wakati mwingine hadi siku sita kwa wiki.

Mbali na Makwetta, Meneja Uchechemuzi na Mawasiliano kutoka Shirika la Save the Children Tanzania, Victoria Marijani amesema ili wanafunzi wale vyakula mchanganyiko, lazima wazazi na shule ziwe na mikakati ya kuwa na njia mbadala za kutafuta vyakula.

Wameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 12, 2024 wakati wa mjadala kwenye Mwananchi X Space, inayoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL)  kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania  pamoja na Taasisi ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC) wenye mada isemayo ‘Umuhimu wa kuwapa chakula mchanganyiko watoto wa shule.’

Makwetta akichokoza mada hiyo amesema uchunguzi huo ulifanyika katika shule za sekondari katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na Mtwara na si shuleni pekee, bali hadi kwa watoto wanaoishi na wazazi wanakula ugali maharage.

Amesema si vibaya kula maharage kwa kuwa ni protini, bali kiafya wanapaswa kulishwa vyakula mchanganyiko kwa kuwa wapo katika kundi rika la balehe.

Amesema hata wanafunzi wa vyuo vikuu, baadhi hawakipi kipaumbele chakula, bali wanavipa kipaumbele vitu vingine.  

Amesema wanafunzi mara chache wanabadilishiwa mbogamboga kama majani, matunda na nyama, lakini kwa kiasi kikubwa wanakula ugali maharage.

Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha lishe kwa watoto shuleni ambapo shule na Serikali itathimini kundi hilo lipewe lishe bora kwa ajili ya afya ya ubongo na kukua vizuri, kwani kipindi cha miaka mitano hadi 19, mtoto anakua katika hatua ya ukuaji.

Naye Marijani akichangia mada hiyo amesema ili wanafunzi wale vyakula mchanganyiko, lazima wazazi na shule ziwe na mikakati ya kuwa na njia mbadala za kutafuta vyakula.

Amesema kamati za shule na wazazi waangalie namna ya kufuga mifugo midogomidogo kama kuku, sungura pamoja na kuzalisha matunda, jambo litakalowafanya watoto wapate virutubisho. Pia faida nyingine ni kuwa itawajengea mazoea watoto kujifunza na kupeleka nyumbani uzalishaji huo.

Sababu ya kusema hivyo inatokana na kile kilichoelezwa watoto wengi wanakula vyakula vya aina moja, jambo ambalo ni changamoto katika ukuaji wao.

Amesema katika ukuaji wa mtoto, vyakula vyenye asili ya wanyama kama dagaa, mayai, maziwa, kuku na nyama ni vyakula vya msingi ambavyo mtoto anatakiwa apate walau mara moja katika mlo wa siku ili apate protini.

“Matunda na mbogamboga ni vyakula vizuri na muhimu kumlinda mtoto dhidi ya magonjwa, lakini wanafunzi wa shule wanalishwa vyakula vya aina moja kutokana na changamoto ya kiuchumi na mazoea.

“Wazazi wanashindwa kuchangia vyakula, pia shule hazina mikakati ya kutafuta namna ya kuzalisha mbogamboga matunda na vyakula vingine kama kufuga kuku, hivyo nashauri kuwe na mikakati ya kuzalisha vyakula hivyo muhimu,” ameshauri Marijani.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Profesa George Msalya amesema uvivu na uzembe, ni changamoto inayowakabili baadhi ya Watanzania kutolipa umuhimu suala la chakula mchanganyiko.

Amesema kutokana na umuhimu wa maziwa, wana mpango wa kupeleka shuleni kwa kuwa yatachangia uwezo kielimu kwa watoto kwa kuwa wamefanya utafiti na kubaini wanafunzi wakitumia maziwa wanakuwa na akili, ikilinganishwa na ambao hawatumii.

“Kuna mpango wa pili wa Taifa wa lishe unaendelea na tumekuwa washirika na tumeahidi kufikia shule 5,000 mwaka 2026 na angalau kuwafikia watoto 1,000,000 kwa miaka hii mitano,” amesema.

Related Posts