Tanzania Prisons yatanguliza saluti Pamba

TANZANIA Prisons imesema pamoja na ubora na uzoefu ilionao kwenye Ligi Kuu, lakini haitawadharau wapinzani wao Pamba Jiji watakapokutana uwanjani Agosti 16.

Timu hizo zinatarajia kufungua pazia ya Ligi Kuu katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, huku rekodi zikiibeba Prisons dhidi ya wenyeji hao waliopanda daraja msimu huu.

Mara ya mwisho wapinzani hao kukutana katika Ligi Kuu ilikuwa mwaka 1997, ambapo katika mechi ya mzunguko wa kwanza Kirumba, walitoshana nguvu ya bila kufungana, huku Prisons ikishinda 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine.

Juzi Mwanaspoti ilishuhudia kocha mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata na benchi zima la ufundi pamoja na mtendaji mkuu, Ajabu Kifukwe wakiwa katika mazoezi ya mwisho Sokoine kabla ya kusafiri kwenda jijini Mwanza.

Kocha msaidizi wa Prisons, Shaban Kazumba alisema pamoja na ugeni walionao Pamba, lakini hawawezi kuwabeza isitoshe watakuwa nyumbani hivyo wataenda kwa umakini na tahadhari kubwa.

Alisema wanachojivunia ni maandalizi mazuri waliyofanya na benchi lao la ufundi ndilo lililoipandisha Pamba Ligi Kuu hivyo wanaijua nje ndani.

“Tumekuwa na muda mzuri wa maandalizi kwani kambi yetu Dar es Salaam michezo mitano ya kirafiki tulishinda minne na sare moja, kiujumla tuko fiti na matarajio ni ushindi” alisema Kazumba.

Nyota huyo wa zamani wa timu hiyo, aliongeza kuwa usajili waliofanya umekidhi mahitaji na ndio kitu kinawapa kujiamini wanapoenda kuianza Ligi Kuu na kwamba msimu huu nafasi nne za juu hawakosi mojawapo.

Related Posts