Ubaguzi unavyowarudisha nyuma watu wenye ulemavu

Dar es Salaam. Ubaguzi kwa watu wenye ulemavu katika jamii unatajwa kama moja ya sababu inayofanya kundi hilo kushindwa kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Baadhi ya fursa hizo ni pamoja na upatikanaji wa ajira, kuwezeshwa kiuchumi pamoja na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo elimu.

Hayo yamebainishwa  leo Jumatatu Agosti 12, 2024 na Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Chawata), Hamad Komboza katika mkutano wa kitaifa wa watu wenye  ulemavu, madiwani na wadau wa jiji la Dar es Salaam.

Komboza amesema baadhi ya watu katika jamii wamekuwa wakiwabagua watu wenye ulemavu katika kuwapa ajira, jambo ambalo linawafanya baadhi yao kuendelea kuwa tegemezi.

“Kwenye ajira kuna sheria inayozitaka kampuni binafsi na Serikali zinapokuwa zinatoa ajira kati ya wafanyakazi 20 watatu lazima wawe wenye ulemavu, japo hili kwa walemavu bado haijafahamika sana, lakini imekuwa changamoto kubwa kwa sababu sheria hiyo haifuatwi,” amesema.

Pia amesema pamoja na baadhi ya watoto wenye ulemavu wamekuwa wakikosa fursa za kupata elimu kutokana na wazazi kuwafungia ndani watoto wao.

“Huko ni kuwanyima haki yao ya msingi watoto hao wanaweza kusoma kama wengine na kufikia malengo yao, msiwafungie, wapeni fursa ya kupata elimu,” amesema.

Hivyo, ametoa wito kwa wanajamii kuwapa fursa watu wenye ulemavu kuonyesha uwezo wao na kuachana na dhana potofu kuwa mlemavu hawezi kufanya kazi.

Pia ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kusaidia katika maeneo yenye huduma za kijamii kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu, ili wazipate kwa urahisi.

Akizungumza katika kongamano hilo, mbunge wa viti maalumu, Stella Ikupa amewahimiza waajiri kuajiri watu wenye ulemavu kwa kuwa wapo wenye vigezo na wana uwezo wa kufanya kazi sawa na wasio na ulemavu.

“Waajiri wanapaswa kufuta imani potofu iliyojengeka kuhusu watu wenye ulemavu kuwa hawawezi,” amesema.

Naye Mkuu wa Idara ya Programu kutoka Taasisi ya Foundation For Civil Society (FCS), Nasim Losai amesema kama wadau wa masuala ya kiraia, ikiwemo haki za walemavu wamekuwa wakishirikiana na Serikali kuhakikisha kunakuwa na miundombinu wezeshi kwa watu wenye ulemavu, hususan katika maeneo yanayotoa huduma za kijamii.

Amesema wakati dunia inapita katika mapinduzi ya teknolojia, wadau mbalimbali wa masuala ya walemavu wametakiwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha walemavu hawaachwi nyuma.

Losai amesema watu wenye ulemavu wanaweza kuwezeshwa kwa kupatiwa vifaa, akitolea mfano wa simu janja pamoja na elimu ya matumizi sahihi ya teknolojia ili nao wanufaike.

Amesema walemavu kuwezeshwa kiteknolojia watanufaika na mambo mbalimbali, ikiwemo kuwarahisishia kufanya shughuli mbalimbali, kuokoa muda, kupunguza gharama, kunufaika na fursa za kiuchumi pamoja na upatikanaji wa taarifa mbalimbali kwa urahisi zitakazowasaidia kufanya maamuzi.

“Kupitia teknolojia inaweza kusaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa kundi hilo, kwani walemavu wanaweza kujiajiri pamoja na kuzalisha ajira kwa wengine, pia upatikanaji wa elimu pamoja na taarifa mbalimbali ambazo zitawawezesha kufanya maamuzi sahihi,” amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa ushauri wa masuala ya watu wenye ulemavu, Peter Mwita ametoa wito kwa walemavu kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.

“Wito wangu kwenu ninawaomba mjitokeze kushiriki uchaguzi ama kupiga au kupigiwa kura. Hii ni haki yenu ya msingi. Hakuna mtu mwingine anayeweza kukufanyia uamuzi kwa ajili ya kujenga Taifa bora unalotaka wewe zaidi yako wewe,” amesema.

Related Posts