Upelelezi kesi ya aliyejitambulisha Profesa Kamugisha wa Muhimbili bado

Dar es Salaam. Uchunguzi bado unaendelea katika kesi ya kutakatisha fedha na kujipatia Sh7.3 milioni kwa udanganyifu inayomkabili mfanyabiashara Ibrahim Bigirwa (33) na wenzake wawili.

Bigirwa na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka 50, yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali.

Bigirwa  pekee, anakabiliwa na mashtaka ya kujitambulisha kwa watu mbalimbali kuwa ni Profesa Kamugisha,  daktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kujipatia fedha kutoka kwa watu hao kwa madai atawasambazia vifaatiba, wakati akijua kuwa ni uongo.

Mbali na Bigirwa, washtakiwa wengine ni Marick Kalimbe (35), mfanyabiashara na mkazi wa Kagera pamoja na Godfrey Fabian (46), mkazi wa Kasindi- Kashai mkoani Kagera.

Leo Jumatatu, Agosti 12, 2024 wakili wa Serikali, Rhoida Mwakamale ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa shauri hilo unaendelea, hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mwakamale ametoa maelezo hayo mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi anayesikiliza shauri hilo.

Hakimu Mushi baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 27, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kisheria.

Kati ya mashtaka 50 yanayowakabili washtakiwa hao; mashtaka 35 ni ya kujipatia fedha kwa udanganyifu, 10 ya kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, mashtaka matatu ni ya kujitambulisha, shtaka moja la kuongoza genge la uhalifu na kutakatisha fedha hizo.

Miongoni mwa mashtaka hayo, shtaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa kati ya ya Februari Mosi, 2024 na Juni 30, 2024 maeneo yasiyojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walianzisha mtandao wa uhalifu wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) wenye kushawishiwa watu mbalimbali na kujipatia Sh 7.3milioni.

Shtaka la pili linamkabili Bigirwa pekee, nalo ni kujitambulisha kwa Segorina Mdegela kuwa yeye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili( Muhas), wakati akijua ni uongo, tukio analodaiwa kulitenda Februari 20, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shtaka la tatu linakabili Bigirwa pekee, nalo ni kujitambulisha kwa Bindiya Sweety Aubroo kuwa yeye ni msaidizi wa Profesa Kamugisha ambaye ni daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili( MNH), wakati akijua kuwa ni uongo, tukio analodaiwa kulitenda Machi 2,2024.

Shtaka la nne linamkabili pia Bigirwa pekee, ambapo April 3, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alijitambulisha kwa Joseph Masanja kuwa yeye ni Profesa Kamugisha kutoka hospitali ya Muhimbili, wakati akijua kuwa ni uongo.

Shtaka la tano hadi 13 ni kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine bila kuwa na ruhusa ya mtoa huduma, yanamkabili Bigirwa na Kalimbe ambapo wanadaiwa kati ya Juni 22, 2024 hadi Juni 24, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina ya Wales Kinkande, Tofulo Swai, Gaitan Mlongamile, Neema Majid na Hakimu Musa, bila kuwa na ruhusa ya mtoa huduma.

Shtaka la 14 hadi 49 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, linalomkabili Bigirwa pekee, ambapo anadaiwa kujipatia fedha kwa watu mbalimbali, huku akiahidi kuwasambazia vifaa vya tiba, kicho ambacho ni uongo.

Miongoni mwa mashtaka hayo, Bigirwa anadaiwa Februari 20, 2024 aliipata Sh 188,000 kutoka katika akaunti ya benki ya CRDB inayomilikiwa na Segorina Mdegela kuwa  madai kuwa atamsambazi vifaatiba, jambo ambalo ni uongo.

Pia anadaiwa kujipatia Sh38,0000 kutoka katika akaunti ya benki ya NMB iliyomilikiwa na Joseph Masanja.

Pia mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia, Sh 670,000 kutoka kwa Masanja, Sh315,000 kutoka kwa Jackline Rugashila, Sh300,000 kutoka kwa Gasaya Mekeya, Sh98,000 kutoka kwa Bibian Komba, Sh142,000 kutoka kwa Flavia Muniga, Sh85,000 kutoka kwa Wdita Abel.

Pia anadaiwa kujipatia Sh1 milioni kutoka kwa Prima Maheshi, Sh24,000 kutoka kwa Sauli Mohamed, Sh300,000 kutoka Gasaya Mekeya, Sh275,000 kutoka kwa Njelika Mwigira.

Pia, Bigirwa anadaiwa kujipatia Sh273,000 kutoka kwa Hawa Kamwela, Sh88,000 kutoka kwa Amon Henry, Sh88,000 kutoka kwa Ester Ndingu, Sh 122,000 kutoka kwa Kelvin Shirima na nyingine kwa madai kuwa atawasambazia vifaatiba, wakati akijua kuwa ni uongo.

Shtaka la 50 ni kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa kati ya Februari mosi, 2024 na Juni 30, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washtakiwa walijipatia Sh 7,345,000, ambazo ni mazalia ya mashtaka ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Related Posts