Wachimbaji Misungwi wagomea fidia ya Sh2 milioni

Mwanza.  Wachimbaji wadogo 32 wanaodai kumiliki eneo la machimbo ya dhahabu ya Shilalo wilayani Misungwi, wamegoma kupokea fidia ya Sh2 milioni kumpisha mwekezaji kutoka kampuni ya ChinaTanjikuangye.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachimbaji hao wamesema fidia hiyo ni ndogo na wanaomba Serikali iweke wazi mkataba ili wajue asilimia watakayoipata kwenye uwekezaji huo.

Mgodi huo uliopo Kijiji cha Shilalo, ulianzishwa na wachimbaji wadogo mwaka 2017 kabla ya kuombewa leseni na kurasimishwa rasmi Desemba, 2022.

Baadaye eneo hilo lilitafutiwa mwekezaji atakayetoa usaidizi wa vifaa na watalaamu kwa lengo la kurahisisha uchimbaji.

Leo Jumatatu Agosti 12, 2024, Mwananchi ilifika katika eneo hilo na kuzungumza na kiongozi wa wachimbaji hao wanaodai fidia, Janeth Bwire ambaye amesema baada ya kuligundua eneo hilo mwaka 2017, walilisafisha na kuliandaa kwa ajili ya uchimbaji.

Hata hivyo, Bwire amesema kwa sababu wachimbaji hao wadogo hawana leseni za uchimbaji, wamiliki wa leseni walioko jirani na eneo hilo waliwafuata na kuwataka wampishe mwekezaji kwa siku 30 ili achukue sampuli na kufanya uchunguzi wa upatikanaji wa kiwango cha dhahabu, kisha wakae mezani na wenye leseni kukubaliana namna watakavyoendeshaji shughuli zao.

Amesema wakati wakisubiri kupata majibu ya uchunguzi huo, wakaanza kulipwa fidia kwa kukadiriwa.

Bwire amesema kila duara (shimo) lenye watu sita mpaka 10 mwekezaji huyo atalipa fidia ya Sh2 milioni jambo ambalo hawajakubaliana nalo na wanataka mkataba uwekwe wazi ili wafahamu wanapata asilimia ngapi kwenye uwekezaji huo.

“Wachina walituambia wakiridhia baada ya kufanya utafiti wa sampuli za udongo wetu tutakaa mezani, lakini tayari wamesharidhia na wameleta vifaa vimeanza kazi na sisi tumetengwa, wamekaa mezani na wenye leseni bila kutuhusisha sisi wachimbaji wadogo tuliolivumbua eneo hili,” amedai  Bwire.

Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Mwanza, Nyaisara Mgaya azungumzie mzozo huo ambaye amesema ofisi yake inautambua mgogoro huo na imeshatoa maelekezo kwa pande zote mbili kukutana ili kumaliza tofauti hizo na kumpa majibu wiki hii.

Pia, amewataka wenye leseni wanapopata wawekezaji, wawafidie wachimbaji waliopo na waondolewe kwa utaratibu maalumu badala ya kufukuzana.

“Kwa taarifa zilizopo ni watu 10 ndiyo naambiwa hawajaridhika na walituandikia barua nikawapa maelekezo viongozi wao na kikundi wakae nao kupata suluhu. Lile eneo lina karibu miaka mitatu halifanyi kazi vizuri, lakini mwekezaji akifika akafanya kazi vizuri hata Serikali tutakusanya mapato, watu watapata ajira na kutakuwa na mzunguko wa uchumi,” amesema Mgaya.

Wakati Mgaya akisema hayo, mchimbaji Antony Madono amesema tangu mwaka 2017 walipoanza shughuli zao, wamefanya uwekezaji mbalimbali ikiwamo kusafisha eneo, kukodi vifaa na kutengeneza barabara wakiwekeza zaidi ya Sh800 milioni ambazo bado hazijazalisha faida.

Amesema mgogoro huo umeanza baada ya kuanza kuhoji mkataba na kutaka uwekwe wazi.

“Hatukatai kulipwa, sisi tunaomba mkataba huu uwe wazi tuko tayari kuondoka hawa Wachina siyo wagomvi isipokuwa hawa wenzetu. Makubaliano yalikuwa kama wakipata mwekezaji sisi wachimbaji wadogo tunapata asilimia mbili ya 10 kitu ambacho hakijafuatwa,” amesema Madono.

Naye, Fatma Ahmada amesema: “Tunaomba haki itendeke, tunavyonyanyaswa hivi hatukubali, wawekezaji wanakuja fedha hazionekani wananufaika wengine halafu tunatishwa wanatuambia kwamba ninyi kama mnaamua chukueni mabomu mmeze mlipuke, hii siyo haki kwa Mtanzania.”

Mchimbaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Haji Seif, amesema: “Tulisema Mchina asifanye kazi mpaka hili suala liishe, lakini tangu Agosti 8, yupo anafanya kazi kwa hiyo tumeshindwa kuvumilia tunaomba Rais Samia Suluhu Hassan aliangalie kwa sababu linaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Leseni (Shilalo Mining Group), Peter Charles amesema wao ndiyo wamepewa dhamana ya kusimamia uchimbaji na wamewalipa wachimbaji 104 kati ya 114 huku 14 wakikataa ambao sasa wameunda kikundi kinachozusha madai hayo huku akiwataka wafike ofisini wachukue fedha zao Sh8 milioni akidai zipo.

“Tuliunda kamati ya tathmini iliyohusisha pande zote ikabainika kuna duara 35 ambazo zilionekana zina thamani ya Sh500,000, Sh1 milioni, Sh2 milioni, unakuta duara ni fupi unalipwa Sh100,000. Baada ya tathmini hiyo wenye maduara wakakubali kulipwa fedha hatukulipa mtu tulilipa duara na zote zililipwa,” amesema Charles.

Related Posts