Wahitimu mafunzo ya amali watakiwa kuanzisha vikundi wakopeshwe

Unguja. Wakati Serikali ikiendelea kuongeza vyuo vya mafunzo ya amali, wahitimu wametakiwa kuunda vikundi ili wapatiwe mikopo isiyo na riba kujiendeleza kiuchumi.

Hayo yameelezwa leo Agosti 12, 2024 na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa katika mahafali ya 11 ya Chuo Cha Mafunzo ya Amali (VTA) Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Lela amesema baada ya kuona nchi zilizofanikiwa kupitia mafunzo ya amali Serikali

imekuja na mabadiliko mapya katika mfumo wa elimu kwa kuanzisha mafunzo hayo katika ngazi ya sekondari. 

“Wahitimu wa vyuo vya amali wana fursa nzuri ya kujikusanya na kupatiwa mikopo isiyo na riba kwa ajili ya kuanzisha miradi ya maendeleo, jambo hili ni zuri na mwanzo wa kujikwamua kiuchumi, kwani vijana wengi hukwama kutokana na kukosa mitaji ya  kuanzisha miradi,” amesema. 

Waziri Lela amesema sio vyema kuona wahitimu wanamaliza lakini wanafanya kazi tofauti na kile walichojifunza kwa sababu ya kukosa mitaji.

Hata hivyo, amesema uzoefu unaonyesha   vijana wengi wanapopata mikopo hubadilisha malengo na matumizi sahihi ya fedha hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo Cha Mafunzo ya Amali,  Dk Bakari Ali Silima amesema wahitimu 493 katika fani mbalimbali wametunukiwa vyeti.

Amesema baada ya kufanya tafiti wamebaini kuna mahitaji ya  mafunzo ya amali kwenye jamii hivyo wameongeza kutoka fani 11 hadi 20 sawa na silimia 82, na chuo kinajipanga kuongeza fani nyingine tatu ikiwemo uvuvi, ufugaji na kuanzisha akademi ya michezo.

Kwa mujibu wa Dk Silima tayari kuna vikundi 28 ambavyo vimesajiliwa na kupatiwa mikopo.

Akisoma risala mmoja wa wahitimu hao, Kassim Khamis Khatib amesema taaluma hiyo itasaidia kujiajiri na kuajiriwa katika sekta binafsi na wanapata nafasi  ya kufanya mafunzo kwa vitendo.

“Hii itasaidia vijana kutatua changamoto ya ajira na ushindani katika soko la ajira,” amesema.

Amesema wamejifunza mambo mbalimbali yakiwamo  ya umeme, magari, vifaa vya kielektroniki, ujenzi, utaalamu wa kilimo, utembezaji watalii na utunzaji majumba.

Hata hivyo amesema changamoto kubwa kwao ni kukosa sehemu za kufanyia mafunzo kwa vitendo.

Katika mahafali hayo pia waziri alikabidhi Sh5 milioni kwa kikundi kimoja kilichokamilisha taratibu za usajili ili kuanzisha mradi wao.

Related Posts