WAZIRI MCHENGERWA ATOA AGIZO KWA TAMISEMI – MWANAHARAKATI MZALENDO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameweka wazi kuwa serikali haitavumilia vitendo vya udhalilishaji dhidi ya walimu nchini, akisisitiza kwamba anataka kuona walimu wakiwa na furaha na wanathaminiwa katika kazi zao. Kauli hiyo aliitoa jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi magari kwa makatibu wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu, iliyofanyika katika mji wa Serikali wa Mtumba.

Waziri Mchengerwa alieleza kwamba Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha walimu hawakabiliwi na changamoto zozote zinazoweza kuathiri utendaji wao. “Rais Samia hataki kusikia walimu wanapata changamoto yoyote. Kama Waziri mwenye dhamana kwenye sekta hii, nataka nione walimu wanafuraha wakati wote, wakifurahia serikali yao,” alisisitiza Mchengerwa.

Akizungumzia umuhimu wa kutokuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji, Waziri Mchengerwa alitoa wito kwa wakurugenzi wasaidizi na makatibu wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kutumia magari waliyopewa kufuatilia na kuondoa kero zinazowakabili walimu katika maeneo yao. “Nataka tuone walimu wakiwa na furaha. Huu ni ujumbe wangu kwa walimu kote nchini – serikali inayoongozwa na Rais Samia inataka kuona kila mtumishi ndani ya TAMISEMI anafurahi na kutabasamu,” aliongeza.

Pamoja na hayo, Waziri Mchengerwa alitoa maelekezo kwa Tume ya Utumishi wa Walimu kuwa karibu na walimu, kuwasikiliza, na kutatua kero zao kwa haraka. “Tume kazi yake ni kukaa na walimu, na katika kipindi changu sitegemei kusikia mwalimu anapata msongo wa mawazo kwasababu hamjamfikia. Msisubiri mimi nipigiwe simu,” alionya Waziri.

Alisisitiza kwamba Tume sasa haina visingizio kwani tayari imeshapata bodi, na kuwataka watendaji wa TAMISEMI kuhakikisha hakuna mtumishi anayekuwa na hofu na serikali yake. Alizidi kueleza kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa walimu, na hivyo Tume inatakiwa kushughulikia kero hizo kwa haraka.

Katika hotuba yake, Mchengerwa pia alisisitiza juu ya uwajibikaji na utambuzi wa majukumu ya kiutendaji kwa watendaji katika maeneo yao ya kazi, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha ufanisi na kuondoa changamoto zinazowakabili walimu na watumishi wengine wa umma.

Waziri Mchengerwa ametuma ujumbe mzito kwa watendaji na viongozi ndani ya TAMISEMI kwamba suala la furaha na ustawi wa walimu litapewa kipaumbele kikubwa, na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale watakaokiuka maagizo haya.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts