UGENI wa ligi na ukata vimetajwa kuwa sababu zilizoifanya Mbeya Unity Queens kutofanya vizuri katika Ligi Kuu ya Netiboli nchini, huku uongozi ukieleza mikakati ya msimu ujao.
Mbeya Unity ilishiriki Ligi Kuu ya Netiboli kwa mara ya kwanza iliyofanyika jijini Arusha, ambako haikuwa na matokeo mazuri ikiishia hatua za awali huku ikiwa timu pekee iliyowakilisha Mbeya kufuatia ndugu zao Mbeya Uwsa kutofika uwanjani.
Mkurugenzi wa timu hiyo, George Mackona alisema pamoja na sapoti ndogo waliyopata kwa wadau, lakini hali ya uchumi iliwapa wakati mgumu kuweza kushiriki vyema pamoja na ugeni waliokuwa nao.
Alisema wanachojivunia ni kushiriki ligi hiyo na kuacha alama na kwamba msimu ujao wataanza maandalizi mapema ikiwamo kutafuta vyanzo vya mapato ili kuwaondoa kwenye ukata.
“Pamoja na changamoto hizo, lakini tunajivunia kufika uwanjani kucheza mechi, vijana wetu wakihitajika sehemu nyingine tutawapa fursa kuondoka kwakuwa michezo ni ajira na uchumi.
“Tutaenda kujipanga mapema kuanzia sehemu ya fedha kwa kubuni vyanzo vya mapato, tutasajili na kuweka kambi nzuri ili msimu ujao tuweze kushindana rasmi,” alisema Mackona.
Mackona aliongeza kuwa pamoja na juhudi za uongozi, aliwaomba wadau jijini Mbeya kujitokeza kuisapoti timu hiyo kama ilivyo kwa upande wa soka ili kuwasaidia vijana kuendeleza vipaji vyao.
“Uongozi unaendelea kupambana, lakini tuwaombe wadau kutushika mkono kama wanavyofanya kwa timu za soka wanaume ili kuwainua vijana kiuchumi na kuendeleza vipaji,” alisema.