15 mbaroni wakituhumiwa kuliteketeza gari lililogonga, kuua

Musoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia watu 15 kwa tuhuma za kuchoma moto gari mali ya Malieta Warioba eneo la Buhare Manispaa ya Musoma.

Watu hao wanadaiwa kuliteketeza gari hilo lililohusika na ajali iliyotokea jana Jumatatu Agosti 12, 2024 na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wanne kujeruhiwa.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumanne Agosti 13, 2024 mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase amesema watu hao wanatuhumiwa kuchoma gari aina ya Toyota Nadia.

“Gari hilo ni mali ya Malieta Warioba, lililokuwa likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Lucas ambaye ni fundi magari. Inaelezwa gari hilo liliacha njia kisha kugonga pikipiki zilizokuwa zimeegeshwa pembezoni mwa barabara katika Barabara ya Mtakuja,” amesema kamanda huyo.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva ambaye pia alikuwa akiliendesha kwa mwendokasi huku akipita sehemu yenye tuta, likaacha njia na kuwagonga watu waliokuwa kando mwa barabara.

Kamanda Morcase amesema baada ya ajali kutokea dereva alilitelekeza gari hilo na kukimbia kusikojulikana na watu waliokuwapo eneo la tukio wakajichukulia sheria mkononi na kulichoma moto gari hilo.

Amemtaja mtu aliyefariki dunia kwenye ajali hiyo ni Kabichi John (38) dereva bodaboda mkazi wa Buhare.

Amesema majeruhi wa ajali hiyo ni Flora Mabunda (51) ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa.

Wengine ni Magoti Mussa (26), Rashidi Hamisi (28) na Davo Bosco (24) wote ni madereva bodaboda na wakazi wa Buhare ambao kwa pamoja wamelazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Musoma.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema ipo haja ya kuangalia namna bodaboda wanavyoegesha pikipiki zao ili kuepuka ajali zisizokuwa za lazima.

“Yaani kuna vijiwe vingine vya bodaboda wanapaki hadi barabarani kabisa na hawana wasiwasi kabisa hii ni hatari sana kwao na kwenye hili mimi nawalaumu bodaboda kwa kuwa usalama wao unatakiwa kuanza na wao mwenyewe,” amesema Agostino John.

Related Posts