LONDON, ENGLAND: MASTAA wa Bayern Munich, Matthijs de Ligt na Noussair Mazraoui wamepanda ndege kwenda England kukamilisha dili lao la Pauni 60 milioni la kujiunga na Manchester United.
Mastaa hao wawili wapo kwenye rada za kocha Erik ten Hag baada ya uhamisho wa Pauni 34 milioni wa beki Mfaransa, Leny Yoro na usajili wa straika wa Kidachi, Joshua Zirkzee, aliyenaswa kwa Pauni 34 milioni. Na dili za De Ligt na Mazraoui zinaonekana kwenda kutiki muda wowote baada ya wawili hao kuonekana wakielekea uwanja wa ndege wa Munich jana Jumatatu asubuhi kuelekea England.
Mastaa hao wawili walionekana kuwa kwenye tabasamu pana, wakikodi gari kuelekea uwanja wa ndege. De Ligt alielekea uwanja wa ndege akiwa peke yake, akibeba begi kubwa. Na staa wa Morocco, Mazraoui alionekana kuwa na begi dogo tu.
Man United inatarajia kulipa Pauni 45 milioni kwenye usajili wa beki wa kati De Ligt, wakati Mazraoui – ambaye aliwahi kucheza chini ya Ten Hag huko Ajax, yeye ataigharimu miamba hiyo ya Old Trafford, Pauni 15 milioni.
Wakati dili hizo zikisubiriwa kwa hamu huko Man United, huu hapa usajili mkubwa wa mastaa 20 uliofanyika kwenye dirisha hili.
1) Dominic Solanke (Bournemouth – Tottenham) Pauni 55milioni
Ilishangaza kuona amekosekana kwenye kikosi cha England kilichokwenda kwenye fainali za Euro 2024, lakini mkali huyo aliyefunga mabao 19 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, alifanikiwa kunasa uhamisho wa kujiunga na Tottenham kwenye dirisha hili. Usajili huo utakwenda kuongeza nguvu kubwa kwenye fowadi ya miamba hilo ya London kwa ajili ya ligi ya msimu ujao.
2) Leny Yoro (Lille – Man United) Pauni 52milioni
Mashabiki wa Man United wanatamba kwamba waliwabwaga Real Madrid kwenye usajili wa beki Leny Yoro. Kinda huyo ni mmoja wa mabeki wanaochipukia kwa kasi kwenye mchezo wa soka huko Ulaya kwa sasa, kiasi cha kumvutia bilionea wa Man United, Sir Jim Ratcliffe kupambana kunasa huduma yake. Atakosa mechi za mwanzo wa msimu kutokana na kuumia kwenye michezo wa pre-season.
3) Pedro Neto (Wolves – Chelsea) Pauni 51milioni
Imekuwa kitu cha kawaida kwa Chelsea kutumia pesa kwenye usajili wa mastaa wapya, ambapo kwenye dirisha hili ililipa zaidi ya Pauni 50 milioni kunasa huduma ya mkali Pedro Neto kutoka Wolves. Wasiwasi mkubwa wa kuhusu mchezaji huyo ni kuhusu rekodi zake za kupata majeruhi ya mara kwa mara ambapo kwa misimu minne iliyopita, amekosekana uwanjani kwenye mechi 100 za klabu na timu yake ya taifa.
4) Joao Neves (Benfica – PSG) Pauni 50milioni
Umri wake ni miaka 19 tu, lakini tayari staa huyo ni mmoja wa mastaa hatari sana kwenye soka la dunia kwasasa. Paris Saint-Germain imefanikiwa kunasa saizi yake ikilipa ada inayozidi Pauni 50 milioni ukijumlisha na nyongezo nyingine. Joao ni moja ya wachezaji wa Kireno wenye vipaji vikubwa ndani ya uwanja na hakika PSG itakuwa kwenye wakati mzuri kwa kufanikiwa kunasa saini yake hasa ushindani uliokuwapo katika dirisha hili.
5) Amadou Onana (Everton – Aston Villa) Pauni 50milioni
Aston Villa imeamua kufanya kweli kwenye dirisha hili kwa ajili ya kuandaa kikosi chake ili kikapambane kikamilifu kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa kitendo cha kumsajili Onana hilo limeifanya Aston Villa kuwa timu iliyotumia pesa nyingi kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
6) Moussa Diaby (Aston Villa – Al-Ittihad) Pauni 50milioni
Ilionekana kama bonge la usajili wakati Aston Villa iliponasa saini ya Mfaransa Moussa Diaby, lakini mkali huyo alianzishwa kwenye mechi 25 tu za Ligi Kuu England na baada ya hapo akajikuta akiwekwa benchi kutokana na makali ya Leon Bailey. Mwaka mmoja baaadaye, aliona anahitaji kwenda Saudi Arabia, ambako atakwenda kukipiga kwenye kikosi cha Al-Ittihad kwa dili la uhamisho wa Pauni 50 milioni.
7) Dani Olmo (Leipzig – Barcelona) Pauni 47.2milioni
Winga, Nico Williams ndiye mchezaji aliyekuwa namba moja kwenye rada za Barcelona kwenye dirisha hili la usajili, lakini badala yake walitua kwa Mhispaniola mwingine na kunasa saini yake, Dani Olmo. Kiungo huyo mshambuliaji amerejea kwenye kikosi hicho cha Nou Camp muongo mmoja baada ya kuondoka, ambapo kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 16. Olmo alikuwa kwenye rada za timu nyingi dirisha hili.
8) Michael Olise (Crystal Palace – Bayern Munich) Pauni 45milioni
Dili la Olise linaweza kuzidi Pauni 50 milioni, lakini kama tu winga huyo atakwenda kupata mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Bayern Munich. Pesa iliyotangulizwa kulipwa huko Crystal Palace ni Pauni 45 milioni, lakini kama staa huyo wa Ufaransa atakwenda kutamba huko Allianz Arena atafungua milango ya kuifanya Crystal Palace kuvuna pesa nyingi zaidi kutokana na uhamisho wake.
9) Joao Palhinha (Fulham – Bayern Munich) Pauni 43milioni
Hiki ndicho kinachotokea Bayern Munich inaposhindwa kubeba ubingwa, yenyewe inasajili kila staa ambaye wanaamini atakuja kuleta kitu kipya kwenye kikosi chao. Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi miamba hiyo inayonolewa na Vincent Kompany ilibisha hodi huko Fulham na kwenda kunasa huduma ya kiungo matata kabisa Palhinha na kufanya moja ya usajili moto kabisa uliofanyika kwenye dirisha hili.
10) Douglas Luiz (Aston Villa – Juventus) Pauni 42.35milioni
Aston Villa imefuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini ililazimika kuuza baadhi ya mastaa wake matata ili kuweka sawa vitabu vyao vya hesabu kwenda sawa na kanuni ya mapato na matumizi kwenye Ligi Kuu England. Kwenye hilo ilifungua milango ya kumpiga bei Luiz kwenda klabu ya Juventus kwa ada ya Pauni 42.35 milioni na kufanya kuwa mmoja ya uhamisho wa kibabe kwenye dirisha hili.
11) Endrick (Palmeiras – Real Madrid) Pauni 40milioni
Ada hiyo inaweza kuwa tofauti na kuzidi kuwa kubwa zaidi baada ya ripoti kufichua kwamba Real Madrid kiasi ambacho ilikubali kulipa kunasa saini ya Mbrazili huyo miezi 18 iliyopita ilikuwa kati ya Pauni 30 milioni na Pauni 50 milioni. Lakini, kinachodaiwa ni kwamba Pauni 40 milioni zilitangulizwa kulipa kunasa saini ya staa Endrick, ambaye anatazamiwa kwenda kufanya mambo makubwa huko Santiago Bernabeu.
12) Max Kilman (Wolves – West Ham) Pauni 40milioni
West Ham United ghafla tu imekuwa timu ya tatu iliyotumia pesa nyingi kwenye usajili wa dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kumnasa Kilman. Wanaweza kushuka kwa nafasi kadhaa wakati dirisha litakapofungwa, lakini Kilman ni moja ya usajili makini kabisa baada ya staa huyo kuhusishwa na klabu kubwa kadhaa zilizokuwa zikihitaji saini yake kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
13) Willian Pacho (Frankfurt – PSG) Pauni 38.6milioni
Zao jingine kutoka kwenye akademia ya Independiente del Valle, iliyomtoa pia Moises Caicedo. Beki wa kati Pacho ameifanya Frankfurt kupata faida kubwa baada ya kusajiliwa kwa pesa ndogo sana kutoka Royal Antwerp, Juni 2023. Na sasa beki huyo atakuwa kwenye kikosi cha miamba ya Ufaransa, Paris Saint-Germain baada ya kunasa kwenye dirisha hili kwa ada inayokaribia kufikia Pauni 40 milioni.
14) Ian Maatsen (Chelsea – Aston Villa) Pauni 37.5milioni
Alikuwa kwenye kiwango bora sana huko Borussia Dortmund, ambapo aliifikisha timu hiyo kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, wakati alipokuwa akichezea kwa mkopo kwenye timu hiyo ya Bundesliga akitokea Chelsea. Msimu ulipomalizika, alirejea Stamford Bridge, ambako miamba hiyo imeamua kumpiga bei jumla kwenda Aston Villa, hivyo kumfanya akipige kwenye Ligi Kuu England msimu ukianza.
15) Joshua Zirkzee (Bologna – Man United) Pauni 36.5milioni
Usajili wa kwanza wa Man United kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya ulikuwa wa Mdachi, Zirkzee. Man United imelipa zaidi ya Pauni 33.6 milioni iliyokuwa imebainishwa kwenye mkataba wake kwa timu inayotaka saini yake, hivyo miamba hiyo ya Old Trafford inatarajia mambo matamu kabisa kutoka kwa mkali huyo wakati atakapoanza kuitumikia timu hiyo kwenye Ligi Kuu England na michuano mingine.
16) Elliot Anderson (Newcastle – Nottingham Forest) Pauni 35milioni
Pesa nyingi sana zimelipwa kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 21, aliyecheza mechi 44 tu za Ligi Kuu England, huku mara 13 tu ndizo alizokuwa ameanzishwa. Ni mchezaji ambaye bado hajapata nafasi ya kuitumikia timu yake ya taifa ya Scotland, lakini Anderson ameonekana ana kitu na Nottingham Forest na kuamua kutoa pesa nyingi hivyo kunasa saini yake. Hakuwa na msimu mzuri alipokuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo.
17) Riccardo Calafiori (Bologna – Arsenal) Pauni 33.6milioni
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta imedaiwa kwamba kwa muda mrefu alikuwa akimfukuzia mchezaji huyo na hakika alipata nafasi ya kumwona vyema kwenye fainali za Euro 2024 huko Ujerumani na kufanikiwa kunasa huduma yake. Mtaliano huyo alicheza kwa kiwango bora kabisa, ikiwamo kuasisti kwenye mechi dhidi ya Croatia. Ada yake iliyotangulia kulipwa ni Pauni 33.6 milioni, lakini inaweza kupanda hadi Pauni 42 milioni.
18) Alessandro Buongiorno (Torino – Napoli) Pauni 30.1milioni
Baada ya kuwa na msimu mbaya, ambapo Napoli ilimaliza ligi ya Serie A iliwa chini ya Torino, miamba hiyo imeamua kufanya usajili wa maana kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kuandaa timu ya kushindana msimu ujao. Miamba hiyo ilifanya pia mabadiliko kwenye benchi lao la ufundi ambalo ilimchukua kocha Antonio Conte, ambaye amefanikisha usajili wa Buongiorno kwa ada zaidi ya Pauni 30 milioni.
19) Archie Gray (Leeds United – Tottenham) Pauni 30milioni
Leeds United imeweka wazi yenyewe kwamba imevunjika moyo baada ya kumshuhudia kinda wao Gray akiondoka kwenye kikosi chao. Lakini, machungu yalipoa baada ya Tottenham iliyomchukua mchezaji huyo, kuamua kuwauzia Joe Rodon katika dili tofauti kabisa. Gray ni moja ya wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
20) Yankuba Minteh (Newcastle – Brighton) Pauni 30milioni
Lyon ilifanya jaribio la kumsajili Minteh, katika kipindi ambacho kinda huyo wa miaka 19 akili yake ilikuwa kwenda kuitumikia Everton. Hata hivyo ni Brighton ndiyo iliyofanikiwa kunasa saini yake na hivyo kumbakiza kwenye Ligi Kuu England. Newcastle iliona ni vyema kufanya dili la pesa nyingi la kumuuza kinda huyo kwa ada ya Pauni 30 milioni kwenda Seagulls, ambao wamekuwa na desturi ya kusajili makinda ya kupandisha viwango vyao.