Dk Biteko azindua kituo cha kupokea, kupooza umeme GGML

Geita. Mgodi wa Uchimbaji Madini ya Dhahabu wa Geita (GGML), umeandika historia baada ya  kuanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha kupokea na kupooza umeme.

Kituo hicho kimejengwa kwa gharama ya Dola 25.8 milioni (Sh67.08 bilioni).

Mgodi huo ulioanza kufanya kazi mwaka 2000, umekuwa ukitumia nishati ya umeme unaotumia mafuta, hivyo kuongeza gharama za uzalishaji na kuzalisha hewa ukaa ambayo ni hatari kwa mazingira.

Akizindua kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 33/11 leo Jumanne Agosti 13 2024, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema mgodi wa GGML hutumia gharama ya Dola5 milioni za Marekani (Sh13.4 bilioni) kwa mwezi kuendeshea mitambo.

“Ujenzi wa kituo hiki cha kupoozea umeme umegharimiwa na GGML na Serikali ambayo imejenga laini ya urefu wa kilomita sita kutoka Mpomvu kufika hapa, nataka niwahakikishie mradi huu ni mradi muhimu na ambao ni wa historia kwenye nchi yetu,” amesema Dk Biteko.

Amesema uamuzi wa Serikali kupeleka umeme GGML sio kwa sababu Serikali haitaki kupeleka umeme kwa wananchi, bali inatokana na ukweli kuwa GGML ni mchangiaji mkubwa wa mapato nchini na sehemu kubwa ya gharama za uendeshaji zipo kwenye gharama ya mafuta.

Amesema mgodi huo hutumia Dola 50 milioni za Marekani (Sh135 bilioni) kwa mwezi ikiwa ni gharama za uendeshaji na gharama za umeme pekee ni Sh13.4 bilioni kwa mwezi.

Kutokana na gharama hizo, Serikali iliamua kujenga laini ya kilomita sita iliyogharimu zaidi ya Sh8 bilioni ili kupeleka umeme kwenye mgodi huo na kupunguza gharama za uendeshaji.

“Maana yake ni kuwa, kila tunapokuwa tunafanya ukokotoaji wa matumizi, GGML iondoe gharama za uzalishaji na kidogo kinachobaki ndio tunagawana. Unapomsaidia kupunguza gharama za uendeshaji, tutapata fedha nyingi,” amesema Dk Biteko.

Hata hivyo, amesema kazi inayofanywa na GGML kwa kutumia umeme unaozalishwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ni zaidi ya umeme unaotumiwa na mikoa kama Tabora, Katavi, Mtwara, Pemba na Singida, ambayo matumizi yake ni chini ya Megawati 34 iliyochukuliwa na GGML.

Awali, Makamu wa Rais wa Anglo Gold Ashanti anayeshughulikia uhusiano na uendelevu wa mgodi, Simon Shayo amesema uzinduzi wa mtambo huo wa kupooza umeme utapunguza gharama za uzalishaji wa umeme kwa asilimia 92.

Amesema mradi huo pia utasaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa zaidi ya tani 700,000 iliyokuwa ikizalishwa kutokana na matumizi ya mafuta na hivyo kufanikisha malengo ya kampuni mama ya kutokuwa na uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050.

Mhandisi Abubakar Issa, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Tanesco katika uzinduzi huo, amesema utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa KV 33 kutoka kituo cha kupoza umeme cha Mpomvu hadi kwenye mgodi wa GGML ulijengwa kwa awamu mbili tofauti.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi katika Kampuni Tanzu ya Tanesco (ETDCO), Dismas Massawe amesema ujenzi wa njia za umeme ulivyopatiwa makandarasi wazawa, umeongeza ujuzi na mapato kwa shirika la Tanesco.

Related Posts