Kauli ya Kingu baada ya kuchaguliwa kuongoza kamati ya Bunge

Dodoma. Mwenyekiti Mpya wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu amesema mkakati wa mkubwa wa kamati yake ni kuishauri Serikali  ihakikishe Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unakuwa himilivu kwa miaka mingi.

Kingu amesema hayo leo Jumanne Agosti 13, 2024 wakati akizungumza na jijini Dodoma muda mfupi baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.

Mbunge huyo wa Singida Magharibi (CCM) amechaguliwa leo kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo ambaye Juni 6,2024, aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji.

Akizungumza Kingu amesema Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHC), imeshasainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu Desemba mwaka jana, hivyo wao kama Bunge wanayo nafasi kubwa ya kuwawezesha Watanzania kunufaika na bima hiyo.

“Mimi kama mwenyekiti mpya wa kamati ninaona tunajukumu kubwa kama kamati ya kuisaidia Serikali katika kuishauri na kuisimamia kwenye suala zima la utekelezaji wa mpango mzima wa bima ya afya kwa wote,”amesema.

Amesema kama Taifa wanafahamu kuwa wanayo mambo mengi na changamoto kubwa ya udumavu unaotokana na masuala ya lishe pamoja na magonjwa ya lishe ambayo yamefanya mfuko wa Bima ya Afya kuyumba.

Amesema magonjwa yanayotokana na lishe yanahitaji uelewa na elimu ya masuala ya lishe kwa jamii ili kuepukana na changamoto hiyo na hivyo kuisaidia Serikali kupunguza mzigo wa fedha za matibabu.

Amesema kama mwenyekiti anaona jukumu la kuishauri Serikali kuhakikisha Mfuko wa Bima ya Afya unakuwa himilivu (sustainable) ili kuhakikisha wanachama wa mfuko huo wanakuwa na uhakika wa matibabu yao ya kesho kwa kile wanachokichangia.

“Hili litawaondolea watumishi wa Serikali stress (msongo wa mawazo) kwa kuhakikisha wanakuwa na uhakika wa matibabu wakiwa wanaumwa. Kwa hiyo lazima tuje na mkakati wa kushauri Serikali kuhakikisha mfuko wetu unakuwa sustainable (himilivu) hili ni jambo la msingi sana,”amesema.

Amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya kuanzia ngazi za chini hadi kwenye ngazi ya rufaa lakini wanaona Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unazidiwa.

Pia Kingu amesema kwa kuwa Tanzania inakwenda katika suala zima la bima ya afya kwa wote ni lazima kuja na mapinduzi makubwa na ya kizalendo ambayo yatafanya NHIF kuwa himilivu.

Amesema mapinduzi hayo yaufanye mfuko huo uwe himilivu ili uweze kuleta matumaini kwa umma, binafsi pamoja na wananchi wote ili waweze kuwa na ari kubwa ya kujiunga na mfuko huo kwa ajili ya kusaidia Taifa.

Amesema kwa mageuzi makubwa yaliyofanywa na Rais Samia katika sekta ya afya hakuna sababu ya kutokuja na mbinu (mechanism) za majibu kwa nini wananchi wawe na imani kubwa na NHIF.

Kingu amesema ni wakati sasa wa Bunge kuja na ushauri wa kimkakati wa kuhakikisha msongo wa mawazo (stress) ambao mfuko huo ulikuwa unabeba na mtikisiko (shock) za kiuchumi zinakoma.

Amesema hiyo itafanya mfuko kuwa himilivu ambao wanachama wake watatarajia kuwa na uhakika wa matibabu kwa miaka 40 hadi 100 mbele na hivyo watu wengi kuhamasika kujiunga na mfuko huo.

Aidha, amesema licha ya mikakati waliojiwekea Serikali katika suala la lishe nchini, lazima wao kama kamati ya Bunge waje na mkakati wa kuhakikisha wanaisimamia Serikali ipasavyo.

“Kwa sababu tukiacha kundi la watoto wakateseka na utapiamlo ina maana kuwa mnatengeneza Taifa ambalo hawatakuwa wazalishaji kwa nchi, hawatakuwa na uwezo wa kufikiria ubunifu, hatutapata wanasayansi kwa hiyo lazima tutengeneze mikakati,”amesema.

Ameishukuru Serikali imekuja na programu ya kitaifa ya lishe ambayo itakuwa na usimamizi mzuri baada ya kuifuta Taasisi ya Lishe na kuwa kamati yake imeridhika na hatua hiyo.

“Sasa tunachotaka kukiona ni utekelezaji unafanyika kwa lengo la kuona namba za utapiamlo zinashuka kutoka asilimia 30 irudi hata ikiwezekana kwenye tarakimu moja kwa lengo la kuisaidia nchi,”amesema.

Related Posts