KILA nikitazama Kikosi cha Azam FC na kile cha Yanga, nagundua kabisa kazini kwa Simba msimu huu kuna kazi.
Ni vigumu sana kujua kama Simba inakwenda mbele au inarudi nyuma. Ni kama mwendo wa kinyonga. Timu haina haraka.
Inakwenda hatua tatu mbele na kurudi tano nyuma. Ni Mwendo unaochanganya sana. Klabu kubwa zote duniani, malengo yao siku zote ni kushinda makombe yote makubwa. Mambo ya kusema wacha wachezaji wazoeane ni habari za timu ndogo. Mambo ya kusema wacha tuwape muda, sio malengo ya timu kubwa.
Mechi dhidi ya Yanga, mashabiki wengi pamoja na kufungwa lakini walau waliona mwanga. Kuna namna Simba ilionyesha ushindani na kuimarika, lakini dhidi ya Coastal Union, walichemsha. Ilikuwa timu inayojitafuta sana.
Mashabiki wengi wamepata wasiwasi kutokana na kiwango walichoonyesha licha ya kushinda. Walipata matumaini mechi dhidi ya Yanga, wakavunjika moyo dhidi ya Coastal Union. Simba imekuwa haitabiriki. Mambo yamekuwa ya kubahatisha bahatisha. Mashabiki hawajazoea kuwa na timu ya kinyonge namna hii. Kila ukiitazama Simba, unatamani msimu mpya usianze. Kila ukiitazama Simba, unatamani michuano ya Kimataifa isianze leo wala kesho. Bado haikupi matumaini. Bado inachechemea.
Simba ni kama bado inahitaji usajili. Ni kama bado inahitaji kuwa ‘Pre season’.
Ukitazama mechi mbili za Ngao ya Jamaii, unaona kabisa bado inahitaji kusajili, unaona ni kama Simba inatakiwa kurudi tena kambini Misri. Mechi dhidi ya Yanga, kulikuwa na mwanga mkubwa. Nilidhani Simba wanaanzia pale kuimarika. Kulikuwa na pasi nyingi zinazofika, muunganiko mzuri wa idara ya kiungo na ushambuliaji, lakini kulikuwa na kazi eneo la mwisho la ushambuliaji.
Nadhani Debora Fernandez na Steven Mukwala wangechangamka kidogo mechi ingekuwa mikononi mwa Simba. Mechi dhidi ya Wagosi wa Kaya, ni kama Simba ilianza upya. Simba kapelekewa moto sana wa Wagosi wa Kaya. Hakukuwa na muendelezo wa uchezaji baina ya wachezaji. Hakukuwa tena na kasi kama mechi dhidi ya Yanga. Hiki ndicho kinacholeta wasiwasi kwa baadhi ya mashabiki. Kiungo Fabrice Ngoma ni kama mtu mwenye mawazo sana. Simba imeanza msimu kwa kumuweka benchi, nadhani imemchanganya. Amecheza kitoto sana mechi ya Coastal Union na kujikuta akiondolewa kwa Kadi Nyekundu.
Steven Mukwala anaonekana ni mshambuliaji mzuri lakini bado hajapata huduma ya kutosha. Mechi zote anaonekana kurukaruka tu na hakuna wa kumuwekea mipira kwenye njia. Simba ina suasua!
Ukitazama washindani wa Simba kwenye mbio za ubingwa wa ligi yetu, unaogopa. Yanga wana bonge la timu kwa kufanya mambo mawili tu. Kwanza, wamefanikiwa sana kuwabakisha wachezaji wake wote muhimu. Hapa ndipo waliposhinda kila kitu. Stephen Aziz KI, Khalid Aucho na Djigui Diarra wamekuwa roho ya timu.
Pili, Yanga wameongeza nguvu sana kwa wachezaji wapya. Cloatus Chota Chama, Duke Abuya, Prince Dube, Jean Baleke na Boka ni chuma juu ya chuma.
Ukitazama Azam FC, unarudi chini kukaa. Azam FC wanazidi kuwekeza kila siku zinavyozidi kwenda mbele. Ni usajili wa maana tu. Ni ngumu sana kumpata mchezaji wa Azam FC lakini afanye uhuni kama Prince Dube.
Kwa sasa Azam FC imeamua mpaka kuvuka bahari. Wachezaji kutoka nje ya Bara la Afrika utawapata pale. Ni kama Azam FC wamekuwa Mamelod Sundowns ya Kibongo. Hawa ndiyo washindani wa kweli kwenye mbio za Ubingwa wa Simba. Hapa napo unakuja wasiwasi mwingine. Njia ya kupata ubingwa ni lazima upambane na Azam FC na Yanga. Nadhani kuna maamuzi pia mbaya Simba lazima wakubali kufanya. Nimemwoma Kelvin Kijili, ni mtu hasa. Bado ana Nishati ya kutosha mwilini na Kiu ya kufanikiwa atakuwa msaada mzuri sana kwa Shomary Kapombe.
Nimemwona Moussa Camara, ni kipa wa daraja la juu. Simba wanaonekana kuwa salama Langoni. Ni Kipa wa kisasa kabisa. Kwa timu yenye ukubwa wa Yanga, haina muda wa kupoteza.
Kipindi cha nyuma kidogo, mechi ya Watani wa Kariakoo ilikuwa haitabiriki lakini naona miaka ya karibuni mambo yamebadilika. Mwenye timu bora amekuwa anashinda.
Yanga katika Kipindi hiki imekuwa bora na imeshinda karibu zote. Huku tunaelekea pazuri sana kama nchi. Mambo ya nje ya uwanja yanapungua. Kazini kwa Simba kuna kazi
Simba inahitaji Debora azoee mazingira haraka sana. Ubunifu wake ni muhimu sana kwa sababu ndiye roho ya ushambuliaji.
Timu inahitaji sana mapambano yake. Joshua Mutale naye bado hajachangamka. Mipira yake ya mwisho bado haijawa na msaada mkubwa kwa timu. Ni mchezaji mzuri lakini bado naona kila anapofika eneo la mwisho ubunifu unakosekana. Mashabiki wanataka kuona maamuzi yake ya mwisho yenye tija kwa timu. Timu kubwa hazina muda wa kusubiri. Presha ni kubwa ndani ya Simba kabla hata ya msimu kuanza. Timu inayotaka ubingwa wa ndani, timu yenye ndoto ya kutwaa kombe la Afrika huwa haina muda wa kusubiri. Ikifika dirisha dogo la Usajili, kuna watu wataliwa vichwa. Mutale alitambulishwa mapema tu kama mtu na nusu wa kuokoa Jahazi. Ni muda wa wachezaji wa Simba kujua msimu umeanza na kazini kwao kuna kazi.