Dar es Salaam. Kesi ya Bernardo Sepeku ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, imeshindwa kuendelea kutokana na jaji anayesikiliza shauri hilo kuwa na majukumu mengine ya kikazi.
Bernado alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.
Pia, anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.
Mlalamikaji huyo alifungua kesi hiyo ya madai namba 378/2023, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Angilana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Katika shauri hilo, mtoto huyo anapinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja namba 2689 chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke ambacho anadai mwaka 1978, waumini na wakristo wa dayosisi hiyo, walimpa Askofu Sepeku kama zawadi.
Kesi hiyo ya madai ilipangwa kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 13, 2024 hadi Agosti 15, 2024 kwa upande wa mlalamikaji kutoa ushahidi wake kuhusu uhalali wa kiwanja hicho.
Hata hivyo, leo Jumanne Agosti 13, 2024, shauri hilo limeshindwa kuendelea kutokana na Jaji Arafa Msafiri anayesiliza shauri hilo kuwa na majukumu mengine ya kikazi.
Awali, mawakili wa Bernardo kutoka kampuni ya uwakili ya kampuni ya Diakonus Attorneys, Deogratias Butawantemi na Gwamaka Sekela wamedai shauri limeitwa kwa ajili usikilizwaji na tayari wanao mashahidi watatu.
Kwa upande wake, wakili Dennis Malamba, anayewawakilisha wadaiwa katika shauri hilo, naye alikuwa tayari kwa ajili ya usikilizwaji, lakini Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Sara Buya amewaeleza jaji anayesikiliza shauri hilo hayupo hivyo kesi hiyo haitaweza kuendelea.
Akiahirisha kesi hiyo, Buya amesema jaji anayesikiliza shauri hilo hayupo hivyo anaahirisha kesi hiyo hadi Septemba 19, 2024 itakapoanza kusikilizwa.
Mlalamikaji anatarajia kupeleka siku hiyo mashahidi watatu wakiwamo maaskofu wa kanisa hilo.
Madai ya msingi katika shauri hilo:
Katika kesi hiyo, Bernardo ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yake, aliwasilisha maombi saba mahakamani hapo, kwanza akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja namba 2689 chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke ambacho anadai mwaka 1978, waumini na wakristo wa dayosisi hiyo, walimpa askofu Sepeku kama zawadi.
Pili, anaomba Mahakama hiyo iamuru Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo, Askofu Sosthenes na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd kwa pamoja kulipa Sh33 milioni ikiwa ni hasara aliyoipata mlalamikaji kutokana na uharibifu wa mazao yaliyowekezwa katika shamba lililo ndani ya kiwanja hicho.
Mlalamikaji huyo alidai mazao yaliyoharibiwa shambani ni pamoja na miti 200 ya malimao, miti 55 ya mikorosho, hekari mbili za mbaazi, hekari mbili za mihogo na hekari mbili za viazi vitamu.
Mazao mengine yaliyoharibiwa shambani hapo ni miti 30 za mapapai, minazi, miti 60 ya miembe, miti 25 ya michikichi pamoja na miti 45 ya minazi.
Tatu, Bernardo anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi iliyopo katika kiwanja hicho.
Nne, mtoto huyo pia, anaomba alipwe fidia ya Sh 493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.
Tano, anaomba Mahakama iamuru wadaiwa wote katika shauri hilo wamlipe mlalamikaji hasara ya jumla iliyopatikana.
Vile vile, Mahakama hiyo iangalie unafuu mwingine wowote ambao itaona inafaa kutoa.
Pia, Bernado anaomba Mahakama iamuru wadai hao walipe gharama za kuendesha kesi hiyo ya madai.