Iringa. Wakazi wa Manispaa ya Iringa wamelalamikia ongezeko la wizi wa mita za maji unaoendelea katika manispaa hiyo, hali inayosababisha hasara kubwa kwa kulazimika kununua mita nyingine kila wakati.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Agosti 13, 2024, wananchi hao wamesema wizi huo umekuwa ukitokea katika mitaa ya Mawelewele, Kihesa, Mkwawa, Gangilonga na maeneo mengine, hali inayowalazimu kununua mita mpya.
Omari Nurdin mkazi wa Mawelewele amesema hali hiyo inawaathiri kwa kulazimika kununua mita mpya kwa gharama ya Sh100,000 mara kwa mara.
“Mimi hadi sasa nimeibiwa mita mara tatu nyumbani kwangu na sielewi wanaoiba ni kina nani,” amesema Nurdin.
Frank Nyalusi, mkazi wa Mtaa wa Mawelewele Kata ya Mwangata, amesema ili Iruwasa iondokane na hasara, lazima wabadilishe utaratibu wa kufunga mita hizo ndani ya nyumba badala ya nje.
Amesema utaratibu wa sasa wa kuzifunga mita za maji nje ya nyumba ni hatari na kwamba mamlaka inawaibia wananchi kwa kuwalazimisha kulipa mita hizo mara mbili.
“Mita ya maji ikifungwa ndani ya nyumba, mwananchi atawajibika kuilipia ikiibiwa kuliko kuifunga nje ya nyumba ambako usalama ni mdogo na huwezi kujua mwizi anaiba saa ngapi,” amesema Nyalusi.
Amesema mamlaka hiyo iachane na mfumo wa mita za zamani badala yake wawafungie wateja mita za malipo ya kabla zinazoweza kufungwa ndani ya nyumba na sio nje ili kuepuka wizi.
“Watufungie mita za kabla ya malipo, hizi ni rahisi hata kuzilinda. Mita za zamani ni vigumu kulinda kwani zinakaa nje ya nyumba ya mteja,” amesema Nyalusi.
Mwananchi Digital ilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Iruwasa, Restituta Sakila ili kupata ufafanuzi zaidi, alikiri kupokea malalamiko hayo na amesema wizi huo wa mita umeathiri na kusababisha hasara kubwa kwao.
Hivyo, amesema ili kukabiliana na tatizo hili, Iruwasa inatoa rai kwa wananchi kuwa makini na kuripoti matukio yote ya wizi au uharibifu wa mita za maji kwenye maeneo yao.
Sakila amesema zaidi ya mita 30 za maji zimeripotiwa kuibwa kuanzia mwisho wa Julai hadi mwanzoni mwa Agosti mwaka huu.
Amesema Iruwasa inaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha wahalifu wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
“Nawaomba wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha vitendo hivi vya uharibifu wa mali za umma,” amesema ofisa huyo.
Amesema wizi wa mita za maji umekuwa changamoto kubwa kwa mamlaka hiyo, ambayo tayari inakabiliwa na jukumu zito la kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wakazi wa Iringa.
Takribani wakazi 47,000, wanapata huduma ya majisafi na salama katika Manispaa ya Iringa, huku wateja waliofungiwa mita za maji ya malipo ya kabla ni 6,000, lakini lengo nikuwafikia wateja wote.