Kukamatwa vigogo Chadema kwaibua hofu uchaguzi ujao

Dar es Salaam. Wadau wa siasa na wanaharakati nchini wamesema hatua ya Jeshi la Polisi kuwakamata wanachama na viongozi wakuu wa Chadema na kuzuia kongamano lao vijana wametoa maoni tofauti, baadhi yakieleza hofu kuhusu uwanja sawa kwenye chaguzi zijazo.

Vilevile, baadhi ya wadau wame wamekumbushia falsafa ya R4 za Rais Samia Suluhu Hassan – maridhiano, mageuzi, kujenga upya na ustahimilivu – kuwa zimewekwa kwenye majaribio.

Wameeleza hayo Agosti 13, 2024, wakati wakizungumza na Mwananchi kuhusu kukamatwa kwa viongozi na wanachama wa Chadema na baadhi yao kuachiwa kwa dhamana, kisha kusindikizwa na polisi kurudi makwao.

Viongozi hao na wafuasi wa Chadema, wapatao 520, akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu, John Mnyika, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho, John Pambalu na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi “Sugu” walitiwa nguvuni na jeshi hilo kati ya Agosti 11 na 12, 2024.

Mbali na hao, kamata kamata hiyo iliyofanyika mikoa mbalimbali nchini, iliwakumba waandishi wa habari, Ramadhan Hamis na Fadhili Kirundwa wa Jambo TV pamoja na Francis Simba ambaye ni mpigapicha wa Chanzo TV, waliokuwa wakitekeleza majukumu yao kwenye ofisi za Chadema Kanda ya Nyasa, jijini Mbeya.

Kushikiliwa kwa wote hao kunatokana na uamuzi wa kwenda Mbeya kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyopangwa kufanywa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), ambayo Jeshi la Polisi liliyapiga marufuku katika hatua za mwisho, likisema kulikuwa na viashiria vya kuvunja amani.

Kuachiwa kwa viongozi na wanachama hao kulitokana na mashinikizo ya wadau mbalimbali kikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichotoa wito kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, kikisema “si mambo yote yanatatuliwa kisheria, mengine ni kisiasa.”

“Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, ongea na waziri, tunaomba muone uwezekano wa viongozi wa vyama vya siasa waliokamatwa kule Mbeya waachiwe huru. Mtupe nafasi na sisi wanasiasa tuzungumze, siyo mambo yote yanatatuliwa kisheria, mengine ni ya kisiasa,” alisema Dk Nchimbi, katibu mkuu wa CCM, akimweleza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo  aliyeambatana kwenye ziara yake.

Kufuatia hatua hiyo, Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Dk Ananilea Nkya amesema ‘kitendo hicho kinaonyesha hakuna demokrasia imara ndani ya Taifa na kinavunja haki za binadamu.

“Maana ya demokrasia ni wananchi kujiamulia mambo yao bila kuvunja sheria, lakini haya mambo yanatia hofu hasa ukizingatia mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025,” amesema.

“Polisi wahakikishe vyama vyote vinafanya shughuli za kisiasa pasipo kuvunja sheria, siyo kazi kwamba upinzani ukifanya kitu unakamatwa,” amesema Dk Nkya.

Suala la hofu lia limeelezwa na Bob Wangwe, mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), kuwa kilichotokea hofu ya watawala na kuwa hakuna utashi wa kutekeleza kipengele cha mageuzi katika falsafa za Rais Samia.

“Kilichopo ni kama danganya toto, hatukutarajia mambo yaliyokuwa yakitokea katika utawala uliopita yajitokeze tena awamu hii, kwa sababu Rais Samia alishajipambanua kuwa anataka kujenga nchi kwa utaratibu huu.

“Kilichotokea ni kama vile kusaliti maneno ya kujenga demokrasia ya kweli, demokrasia haiwezi kujengwa katika mazingira ambayo nguvu inatumika kuzuia haki za demokrasia za watu kufanya mikutano ya hadhara. Mambo haya yakiendelea yatazua hofu kwa wananchi hawataona umuhimu wa uchaguzi,” amesema Wangwe.

Ili kuondokana na changamoto hizo, Wangwe amemshauri Rais Samia kuzitafakari R nne, kuona kama kweli utekelezaji wake unalenga kuleta mageuzi katika demokrasia

Hata hivyo, msomi na mchambuzi wa siasa, Dk Richard Mbunda amesema kuna baadhi ya watu hawajaielewa falsafa za R nne za Rais Samia zinazolenga kuendesha siasa, nchi na kuboresha hali ya demokrasia.

“Kilichotokea Mbeya ni dhahiri kuna baadhi ya taasisi ambazo ni wadau muhimu wa siasa hawajazielewa.

“Natamani ili falsafa hizi zisionekane ni maneno, basi Rais afanye jambo atuonyeshe kweli anasimamia R nne kwa sababu Jeshi la Polisi haliwezi kuzua tu taharuki, hasa tunapoelekea katika uchaguzi. Nilitamani Rais achukue ‘action’ kwa watu wasiotumia vizuri au kutotekeleza wajibu wa kusimamia R nne.

“Kama umesikia viongozi wa chama tawala, viongozi wa dini na makundi mbalimbali wanaingilia kati na kuagiza waliokamatwa waachiwe huru, ni dhahiri kuna makosa sehemu. Kilichotokea jana  Mbeya kinakwenda kuharibu mwonekano au msingi mzuri uliowekwa kuhusu R nne kuanzia katika kikosi kazi,” amesema Dk Mbunda.

Dk Mbunda ameongeza “hatua hii inaathiri namna nchi inavyotakiwa kuendesha siasa za utulivu na maandalizi ya uchaguzi mkuu.”

Kwa upande mwingine, mchambuzi wa kisiasa, Dk Onesmo Kyauke amesema ingawa 4R si tatizo kwa asili, tatizo linajitokeza pale vyama vya kisiasa vinapokuwa vinachukulia kuwa vina uzito sawa na sheria za nchi.

“Wakati vyama vinakutana na masuala kama haya, vinapaswa kutafuta tafsiri ya kisheria ili kubaini kama mikutano yao au mikusanyiko yao inaruhusiwa. Vinapaswa kutumia mchakato huu kuelewa ambapo wanaweza kuwa wamekosea kama chama, badala ya kudhani kwamba 4R pekee zinaweza kutatua masuala ya kisheria,” alisema Dk Kyauke alipozungumza na Gazeti la The Citizen.

Dk Kyauke ambaye pia ni mhadhiri wa sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesisitiza nchi haipaswi kufanya kazi kulingana na falsafa ya kiongozi au mapenzi ya kisiasa, bali inapaswa kuzingatia sheria za nchi ambazo zinaeleza kwa uwazi mambo haya.

“4R zimeonyesha mapenzi ya kisiasa ya Rais katika maeneo fulani, kama vile kuruhusu Chadema kufanya maandamano, lakini hatupaswi kutegemea sana kanuni hizi na kusahau sheria na miongozo inayotutawala,” ameongeza.

Mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Paul Loisulie, amesema harakati za vijana katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kenya, zimeathiri sana mandhari ya kisiasa, mara nyingine zikileta kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri.

“Matamshi yaliyotolewa na viongozi wa Bavicha yalionyesha vitendo vyao vitakabili changamoto kwa Polisi. Tukiangalia mfano wa vijana wa Kenya (Gen-Z) na jinsi walivyohatarisha amani ya Kenya hivi karibuni, ilikuwa wazi kwamba polisi wangeingilia kati,” alisema.

“Hali katika nchi nyingine zilizokumbana na masuala kama haya, imesababisha kuongezeka kwa uangalizi wa polisi ili kuzuia dalili zozote za matukio kama haya hapa Tanzania.”

Amesisitiza kwamba 4R bado ni falsafa ya binafsi ya Rais na haijaeleweka au kupokelewa kikamilifu ndani ya chama chake (CCM) au hata na vyama vya upinzani nchini.

Akizungumzia sakata hilo, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Nuhu Mruma amewataka wadau wa siasa, vikiwemo vyama vya siasa na Jeshi la Polisi, kufanya kazi kwa mujibu wa taratibu, akisema kuna wakati kunahitajika ushirikiano kuliko “kubebwa na mihemko au kauli zinazolenga uchochezi”.

“Tuna njia nyingi za kufanya mambo yetu bila kutumia mifano ya sehemu zilizoleta machafuko, lakini kudai haki kuna njia zake za kisheria za kupita. Lakini wanaostahiki kutoa haki wasimame katika mstari kutoa haki pasipo ubaguzi wa aina yoyote ili kuepusha migongano.

“Upinzani siyo uadui wala si vita, kinachotakiwa ni kukaa na kukubaliana ili kila mmoja anadi sera zake kwa amani kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi. Lakini tusimame na falsafa ya R nne inayolenga busara zaidi, ili kusitokea kitu kitakachowanyima wengi haki ya kufanya siasa,” amesema Mruma.

Wakati wachambuzi hao wakiwa na mtazamo huo, mwenzao Rainery Songea amesema hoja ilikuwa kuzuia kongamano la Bavicha, jambo ambalo polisi wamefanikiwa, ingawa amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

“Kama watu wanakamatwa, basi wawe wamefanya makosa lakini watu wanafanya siasa huru na wamepanga kukutana halafu wanakamatwa badala ya kuachiwa kufanya jukumu hilo. Mbona CCM walifanya Zanzibar hakukuwa na tatizo au mbona viongozi wa chama tawala hawakamatwi,” amesema.

“Inabidi mazingira yatengenezwe ili kuwe na usawa kwa pande zote mbili za upinzani na chama tawala pasipo ubaguzi,” amesema Songea.

Jana Jumatatu Mwananchi lilizungumza baadhi ya wasomi walidokeza kuwa uamuzi wa Serikali kupiga marufuku kongamano hilo, huenda ikawa hofu ya  mabadiliko ya mwenendo wa siasa za ulimwengu, ambao umeshuhudiwa  kwenye mataifa mengi vijana wamewatikisa watawala.

“Hii hatua ya kuzuiwa inatokana na wasiwasi walionao viongozi juu ya uwezekano wa maandamano kutengeneza nafasi ya kisiasa ya kufanya wanayotaka kuyafanya,” alisema Dk Conrad Masabo, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom),

Hoja inayofanana na Dk Masabo, ilitolewa pia na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Mohamed Bakari aliyesema kuna hofu ya watawala kuepuka yaliyotokea katika mataifa kadhaa duniani.

Sakata lililopo kwenye mjadala sasa, halina tofauti sana na kauli ya Aprili 5, 2024 ya Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi, kuwa makundi mawili yanayosigana juu ya uhuru na haki yanapaswa kukutana na kukubaliana kwanza kabla ya kuingia kwenye uchaguzi.

Jaji Warioba alisema yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 yamevifanya vyama vya upinzani kupoteza imani na kuzidisha hofu juu ya kauli za viongozi wa Serikali na CCM kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na haki.

Related Posts