Mama mbaroni akidaiwa kumuua mwanaye kisa ugumu wa maisha

Mufindi. Mama wa watoto wawili, mkazi wa Mtaa wa Tanganyika, Kata ya Kinyanambo ‘A’ wilayani Mufindi, Sophia Mzena (39) anashikiliwa na Jeshi la Polisi  mkoani Iringa kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili kwa madai ya ugumu wa maisha.

Pia anadaiwa kumcharanga mapanga mtoto wake mwingine mwenye umri wa miezi minne anayeendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mji wa Mafinga.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Agosti 13, 2024, Mwenyekiti wa Mtaa wa Tanganyika, Samweli Matinya amesema tukio  lilitokea Agosti 10, 2024 saa 11:30 alfajiri.

Amesema siku ya tukio alipigiwa simu kwamba kuna mwanamke amewakatakata watoto wake wawili kwa panga katika mtaa wake.

Matinya amesema baada ya taarifa hiyo, alikwenda eneo la tukio na kukuta mwanamke huyo ameshakamatwa na watu waliowahi kufika nyumbani hapo.

“Nilikuta watu hao wanamnywesha maziwa wakidhani huenda na yeye kanywa sumu ili ajiue, nikawaambia tumpeleke hospitali haraka,” amesimulia mwenyekiti huyo.

Mbali na mama huyo, Matinya amesema watoto waliokuwa wamejeruhiwa nao walipelekwa hospitali wakiwa bado hai. “Lakini kwa bahati mbaya kwa kuwa walikuwa wametokwa na damu nyingi, yule mkubwa alifariki dunia wakati madaktari wakiendelea kumpatia matibabu.”

Amesema, “Mama yake aliwekewa chupa ya maji na baada ya muda alianza kuzungumza, nikamuuliza kwa nini amechukua uamuzi wa kuua watoto wake, akanijibu ni kutokana na hali ngumu ya maisha anayopitia,” amedai mwenyekiti huyo.

Akizungumzia na Mwananchi kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema watalitolea taarifa rasmi.

Hata hivyo, imeelezwa mama huyo anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.

Jacob Mwapinga, baba wa watoto hao amesema aliondoka nyumbani kwake Agosti 6, 2024 kuelekea mkoani Njombe kwa shughuli zake za kilimo na kumuacha mkewe salama na watoto na kwamba hakukuwa na shida yoyote.

“Tuliagana vizuri tu na watoto wangu walinisindikiza hadi stenda. Yeye nilimuacha akiwa amelala na watoto wadogo wawili, alitaka kunisindikiza lakini nikamuambia apumzike tu kwa kuwa ni asubuhi, tukaanga vizuri nikamuachia mahitaji muhimu na fedha kidogo za matumizi ya nyumbani,” amesimulia Mwapinga na kuongeza;

“Njombe nimekaa kama siku mbili, Jumamosi saa 12 asubuhi nikapigiwa na kupewa taarifa na majirani kwamba watoto wamekwenda kuwaambia mama yao amewajeruhi watoto.”

Hata hivyo, amesema hajui ni kitu gani kilichompata mkewe hadi akatekeleza unyama huo.

“Bado sijajua kitu gani kimemkumba mke wangu, kwa sababa amekuwa kama amerukwa na akili…, sijui pepo gani limempata. Ukimuuliza anaongea vitu visivyoeleweka, naomba Mungu anisaidie,” ameendelea kusimulia huku akibubujikwa machozi.

Alipoulizwa kuhusu hali ngumu aliyodai mkewe mpaka kufikia uamuzi huo, amesema hawakuwa na changamoto yoyote ya kifamilia kwa kuwa mahitaji yote muhimu alikuwa akimpatia.

“Kama ni shule, watoto wanasoma na mahitaji yao yote nayatimiza, hakuna kitu nilikuwa nakifanya bila kumshirikisha mke wangu,” amesema Mapinga.

Hata hivyo, amesema mtoto wake aliyenusurika mwenye miezi minne anaendelea vizuri na matibabu.

Awali akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Mafinga, Amata Haule amethibitisha kuwapokea watoto wawili wakiwa majeruhi, lakini mmoja alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

Dk Haule amesema wanaendelea kumtibu mtoto wa miezi minne hospitalini hapo na hali yake inaendelea kuimarika.

Baadhi ya majirani wamesema waligundua tukio hilo baada ya mtoto mkubwa wa mama huyo kukimbia na kupiga kelele za kuomba msaada.

Mmoja wa majirani, Elivida Mahesa (43), amesema mtoto huyo alifika nyumbani kwake akimuita kwa ajili ya kutoa msaada.

“Mtoto alifungua geti huku akiita mama mkubwa, mama mkubwa njoo uone nyumbani,'” amesema Mahesa.

Amesema walipofika nyumbani walikuta mama huyo amejifungia ndani, hivyo walilazimika kuvunja mlango na kuingia ndani ambako waliwakuta watoto wawili wakiwa wamejeruhiwa na damu zimetapakaa, huku mama yao akiwa chooni analalamika.

“Baada ya kufungua mlango, sikuweza kuingia kwa sababu watoto walikuwa na majeraha makubwa, baadhi yao vichwa vikiwa wazi. Mmoja alikuwa na damu sehemu ya kichwani, hivyo sikusogea nikatoa nje.

“Regina ambaye ni mtoto wa mama huyo, aliingia na kuchunguza hali ya wadogo zake, ndipo alitoka akiwa kama amechanganyikiwa na kusema ‘nitatangulie, nitatangulie,” amesimulia jirani huyo.

Related Posts