Matampi awaibukia Waangola | Mwanaspoti

KIKOSI cha wachezaji 22 cha Coastal Union na benchi lote la ufundi, alfajiri ya kesho Jumatano kimeanza safari kuifuata AS Bravo ya Angola huku kipa namba moja na timu hiyo, Ley Matampi akijumuishwa.

Coastal Union ambayo inaiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Jumamosi ya wiki hii inatarajiwa kupambana na Waangola hao katika mchezo wa hatua ya awali utakaofanyika kwenye Uwanja wa Tundavala uliopo Lubando nchini humo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub amesema kila kitu kuhusu maandalizi ya timu yao yamekamilika.

“Mchezo utachezwa Jumamosi, sisi kama viongozi kwenye masuala ya safari kila kitu kipo tayari na wachezaji 22 pamoja na benchi la ufundi wapo kwenye hali nzuri,” alisema kiongozi huyo.

Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma, akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kwa ujumla alisema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri tayari kwaajili ya kuipambania timu yao iweze kupata matokeo ugenini.

“Kikosi changu kipo tayari na nafurahishwa na upambanaji wao, ukiangalia mechi mbili tulizocheza hivi karibuni kuna mabadiliko makubwa, mchezo wa kwanza tulifunguka tukaadhibiwa, makosa niliyoyaona dhidi ya Azam FC niliyafanyia kazi,” alisema na kuongeza.

“Mchezo uliofuata wachezaji wangu walizingatia maelekezo, licha ya kupoteza lakini hatukufanya vibaya sana, natarajia watakuwa bora na imara zaidi kwenye mechi yetu ya Jumamosi dhidi ya wenyeji wetu AS Bravo ya Angola.

“Ni vizuri tunaanzia ugenini, tunaenda kutumia vyema mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani, lengo ni kwenda kupata matokeo mazuri ili kuja kumaliza mchezo nyumbani na hatimaye kutinga hatua inayofuata.”

Akizungumzia suala la Matampi, Ouma alisema bado ni mchezaji wa timu hiyo na kutoonekana kwake kwenye mechi mbili za Ngao ya Jamii ni kutokana na kuchelewa kujiunga na timu kwenye maandalizi lakini hivi sasa yupo tayari na ameanza mazoezi.

“Yupo pamoja na timu na ameanza mazoezi ni miongoni mwa wachezaji watakaosafari na timu,” alisema kocha huyo raia wa Kenya.

Related Posts